Friday 25 March 2016

KIFUA KIKUU JANGA LA TAIFA-UMMY MWALIMU

Wakati Tanzania ikiungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha siku ya Kifua Kikuu, serikali imeutangaza ugonjwa huo kuendelea kuwa  janga la kitaifa kutokana na kila mwaka watu 112,000 huugua na 12,000 hufariki dunia.
 
Kutokana na changamoto hiyo, serikali imeanza mchakato wa kuhakikisha utoaji wa huduma za Kifua Kikuu zinakuwa ni lazima kwa vituo vyote vya afya vya serikali na binafsi.
 
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alitangaza hatua hiyo jana wakati wa maadhimisho ya ugonjwa huo yaliyobebwa na kauli mbiu ‘Tuungane kutokomeza Kifua Kikuu’.
 
Mwalimu alisema takwimu za mwaka jana zinaonyesha ugonjwa huo bado ni tatizo na Shirika la Afya Duniani (WHO) linaendelea kuiweka Tanzania katika orodha ya nchi 22 duniani zenye wagonjwa wengi.
 
Alisema licha ya kutibika, lakini ndio ugonjwa pekee wa kuambukiza unaosababisha vifo vingi katika jamii na kwamba watu watatu wamekuwa wakifariki kila baada ya dakika moja.
 
“Takwimu zinaonyesha takribani watu 12,000 hufariki kila mwaka, hivyo bado ni tatizo kubwa baada ya miaka 10 tangu Tanzania ilipotangaza kuwa ni janga la kitaifa kama ilivyoainishwa katika Azimio la Maputo la mwaka 2005,” alisema.
 
Alisema kwa miaka 10 iliyopita, wastani wa wagonjwa wapya kwa mwaka ulikuwa ni 63,000.
 
Alisema takwimu zinaonyesha kiwango cha ukubwa wa tatizo la ugonjwa huo ni zaidi ya wagonjwa 295 kwa kila watu 100,000. 
Alisema kutokana na matibabu ya ugonjwa huo kuwa ni bure, wizara inaangalia uwezekano wa hospitali binafsi kuongeza nguvu ya utoaji wa huduma.
 
“Serikali tunatoa dawa na vifaa kwa hospitali binafsi ila mpaka sasa ni asilimia 10 ya vituo binafsi vinavyotoa huduma na ni asasi chache zinazojihusisha na harakati za mapambano katika mikoa na Halmashauri,” alisema na kuongeza:
 
“Natoa rai kwa wamiliki wa vituo binafsi vya afya kupanua zaidi wigo wa kutoa huduma hizi, dhamira yetu ni kila mwananchi apate huduma katika maeneo wanayoishi bila kikwazo.”
 
Alisema tathmini zilizofanywa na Idara za Afya na Elimu katika baadhi ya shule za mkoa wa Pwani zimebaini mabweni mengi yana vyumba vidogo na msongamano wa wanafunzi.
 
“Katika madarasa mawili ya shule moja walipatikana wanafunzi 16 kati ya 775 wenye kifua kikuu cha kuambukiza,” alisema.
Mwalimu aliwaagiza wakurugenzi wa halmashauri wafanye ukaguzi kwenye shule zote za bweni za umma na binafsi ili kubaini mazingira hatarishi.
 
Alisisitiza kuwa ukaguzi huo uende sambamba na uchunguzi wa kifua kikuu miongoni mwa wanafunzi wa shule za bweni za msingi na sekondari kwa kutumia fomu za uchunguzi wa ugonjwa huo ikifuatiwa na upimaji kwa wale watakaoonyesha dalili.
 
“Wale wahudumu wa afya ambao hupelekewa fomu na wanafunzi wanaotaka kujiunga na bweni ili wazijaze kama wanamagonjwa yoyote, nawaagiza kuanzia sasa waache tabia ya kujaza bila kupima, ninajua kinachofanyika,” alisema.
 
Aidha, alisema wizara yake imeanza mashauriano na Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi pamoja na Tamisemi ili kuweka mikakati endelevu ya udhibiti shuleni.
 
Aliitaja mikoa inayoongoza kuwa ni Arusha, Dar es Salaam, Kilimanjaro, Mara, Manyara, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Pwani, Shinyanga, Tabora na Tanga.
 
Alisema takwimu zinaonyesha mikoa hiyo inachangia zaidi ya asilimia 70 ya wagonjwa wote waliogundulika Bara na visiwani.
Mwalimu alisema kiwango cha wagonjwa wanaopata matibabu na kupona kimevuka lengo la kimataifa linalotaka kuponyesha kwa asilimia 85 na kuwa Tanzania wamefikia asilimia 91 mwaka juzi.
 
Alisema vifo miongoni mwa wagonjwa vimepungua na kufikia asilimia 50 kutoka asilimia 11 mwaka 2000 hadi kufikia asilimia 5.6 mwaka juzi.
 
Meneja Mpango wa Taifa wa Programu ya Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma, Dk. Beatrice Mutayoba, alisema mkakati wa WHO ni ifikapo mwaka 2035 ugonjwa huo uwe umetokomea.
 
Mkurugenzi wa Huduma na Tiba wizarani hapo, Dk. Margaret Mgando, alisema hali ya hospitali ya Kibong’oto ambayo ndiyo tegemeo ni mbaya na mchakato wa kuiboresha umeanza.
 
Alisema kwa sasa kuna upanuzi wa hospitali hiyo unaoendelea na wataongeza vifaa pamoja na kuifanya iwe na bodi ya kuiendesha.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!