Tuesday 15 March 2016

CHAMA CHAONDOA KAPTURA KWENYE SARE INDIA

SareImage copyrightAFP
Image captionSare rasmi ya chama hicho sasa itajumuisha suruali ndefu
Chama cha mrengo wa kulia cha Wahindi cha Rashtriya Swayamsevak Sangh (RSS) kimetangaza kwamba kitaondoa kaptura za rangi ya kaki kwenye sare yake, baada ya kutumiwa kwa miaka 91.


Sare ya chama hicho, ambayo imejumuisha suruali kipande, za rangi ya kaki sasa itakuwa na suruali ndefu za rangi ya hudhurungi.
Uamuzi huo ulifanywa kwenye mkutano mkuu wa kila mwaka wa viongozi wa chama hicho.
Chama cha RSS, ambacho maana ya jina lake ni Chama cha Taifa cha watu Waliojitolea, ndicho kilichoasisi sera zinazofuatwa na chama tawala cha BJP.
Waziri mkuu wa sasa Narendra Modi aliwahi kuwa mwanachama wa chama hicho.
Image copyrightAFP
Katibu mkuu wa chama hicho Suresh Bhaiyyaji Joshi amewaambia wanahabari kwamba mabadiliko hayo yanatokana na hali kwamba chama hicho kinataka kutembea na majira.
Kuhusu rangi, amenukuliwa na shirika la PTI akisema sababu pekee ya kuondoa rangi ya kaki ni kwamba rangi ya hudhurungi hupatikana kwa urahisi na “inapendeza”.
Mabadiliko hayo yatatekelezwa katika kipindi cha miezi sita ijayo.
Chama cha RSS (ambacho pia hujulikana kama Sangh) kilianzishwa 1925 na kimewahi kupigwa marufuku mara tatu tangu uhuru.
Wapinzani wa chama hicho husema ni chama cha kugawanya watu, cha kupenda vita na kinaamini katika “ubabe wa Wahindi” na hueneza chuki dhidi ya Waislamu na Wakristo walio wachache.
Inakadiriwa kwamba hatua hiyo itasababisha hitaji la suruali ndefu karibu nusu milioni.
Image copyrightAFP
Mwaka 2010, chama hicho kilipobadilisha mishipi yake ya turubai na kuanza kutumia mishipi ya ngozi, kulitokea uhaba mkubwa sana wa mishipi. Ilichukua miaka miwili kutekeleza pendekezo hilo.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!