Rafael Shilatu ambae ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nyamagana (Kulia) akizungumza katika hafla ya kumpongeza msanii Rich4D.
Na:George Binagi-GB Pazzo @BMG.
Chama cha Mapinduzi CCM kimekubali kumsafirisha kwa ndege Mwanamuziki Chipukizi Richard Stanford maarufu kwa jina la Rich4D, alietembea kwa miguu kutoka Jijini Mwanza hadi Jijini Dar es Salaam ili kumpongeza Rais Dkt.John Pombe Magufuli kwa kuwajumuisha Wasanii katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Mwenyekiti wa Chama hicho Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza Raphael Shilatu, alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita, katika hafla ya kumpongeza msanii huyo kwa matembezi yake baada ya kurejea Jijini Mwanza.
"Kwanza nimpongeze kwa matembezi yake ambayo ni ya kizalendo kabisa. Lakini niseme kwamba atakapopata fursa ya kwenda kuonana na Mhe.Rais, tutamsafirisha kwa ndege kutoka Jijini Mwanza hadi Jijini Dar na kumrudisha pia". Alisema Shilatu huku akimuomba Katibu Mkuu Mhandisi John Kijazi kumsaidia msanii huo ili aweze kuonana na Mhe.Rais Dkt.Magufuli.
Januari 16 mwaka huu Msanii Rich4D alianza matembezi yake kutoka Jijini Mwanza na kupita katika Mikoa Minane sawa na kilomita 1,200 hadi kufika Jijini Dar Februari 10, hii ikiwa ni siku 26 mfululizo za matembezi hayo ambayo mbali na kumpongeza Rais Dkt.Magufuli, pia yalilenga kuwasilisha kilio cha wasanii chipukizi wa Mikoani ambao wamekuwa wakikosa fursa mbalimbali ikilinganishwa na wasanii wakubwa walioko Jijini Dar.
"Kila Mkoa na Wilaya nilizopita nilipokelewa na
viongozi mbalimbali wakiwemo Maafisa Utamaduni na baada ya kufika Dar
nilipokelewa na Viongozi wa Serikali akiwemo aliekuwa Katibu Mkuu
Ombeni Sefue ambae aliniahidi kuonana na Mhe.Rais kabla mwezi wa mwili haujaisha kwani nilishindwa kuonana na rais baada ya kuambiwa yuko katika majukumu mengine ya Kitaifa".
Alitanabaisha Rich4D na kumuomba Katibu Mkuu mpya Mhandisi John Kijazi kuhakikisha ahadi aliyoiacha Sefue inatimia.
Msanii Rich4D akionyesha Vibali alivyokuwa navyo kabla ya kuanza matembezi yake.
Bonyeza HAPA Kutazama Picha za Mapokezi.
No comments:
Post a Comment