Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Democratic Alliance (Tadea), Lifa Chipaka, anawaomba wasamaria wema msaada wa fedha ili atibiwe maradhi ya figo yanayomsumbua kwa muda mrefu sasa.
Akizungumza kwa shida na Nipashe nyumbani kwake Mbezi kwa Msuguri Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam, Chipaka alisema aligundulika kuwa na ugonjwa huo alipopelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Temeke baada ya uchaguzi mkuu mwaka jana na kuanza matibabu.
Hata hivyo, alisema kwa sasa ameshindwa kurudi hospitali kuendelea na matibabu kutokana na ukosefu wa fedha.
“Naomba wasamaria wema mbalimbali wanisaidie nipate matibabu katika hospitali yoyote iliyo karibu. Ninaamini wakinisaidia nikapata matibabu, nitarudi katika hali yangu ya kawaida,” alisema kwa shida Chipaka.
Kwa upande wake, mke wake, Ruth Kunambi, alisema mume wake ameugua kwa muda mrefu maradhi hayo na kwamba tangu alipojulikana kupatwa ugonjwa huo mwaka jana katika Hospitali ya Wilaya Temeke, hajatibiwa tena.
Alisema hali ya mumewe imekuwa ikibadilika badilika na nyakati za usiku huwa mbaya zaidi.
Amewaomba wasamaria wema watu binafsi, mashirika na kampuni, kujitoa kumsaidia mumewe ili kuokoa maiha yake.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment