Tuesday, 2 February 2016

WANAOTOA LUGHA CHAFU KWA WAGONJWA "KUKIONA"



Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, imelitaka Baraza la Wauguzi na Wakunga kuchukua hatua dhini ya watoa huduma za afya ambao wanatoa lugha chafu kwa wagonjwa ili kurudisha nidhamu ya sekta ya afya nchini. 
 
Mwalimu alitoa agizo hilo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Faida Mohamed Bakari, aliyetaka kujua serikali inachukua hatua gani kwa wahudumu wa afya  ambao wanatoa lugha chafu za matusi kwa wagonjwa wanaopofika kutibiwa katika vituo vya afya na hospitali.
 
Mwalimu alisema watoa huduma za afya  ambao wamekuwa wakitoa lugha chafu kwa wagonjwa watawajibishwa, huku akiwataka wananchi kutoa taarifa wanapokutana na hali hiyo.
 
Waziri huyo alisema nidhamu imeshuka katika sekta ya afya nchini, kutokana na baadhi ya watoaji wa huduma kuwa na lugha chafu na kuahidi kurejesha sifa nzuri ya sekta hiyo kwa kuwawajibisha wasio na nidhamu.
 
Mwalimu alisema tangu alipoingia katika wizara hiyo aliweka  utaratibu wa watumishi wote wa sekta ya afya kuvaa vitambulisho vyenye majina, ili kumuwezesha mgonjwa kujua mhudumu anayemhudumia.
 
Aliwataka wagonjwa kuhakikisha wanasoma majina ya waaguzi wanaowahudumia ili watakapotoa lugha chafu ambazo haziendani na maadili ya kazi yao waweze kutoa taarifa mara moja sehemu husika.
 
Alisema ameandaa utaratibu wa kupokea malalamiko mbalimbali na kuyafanyia kazi kisha kuchukua hatua stahiki kwa wahusika ikiwa ni pamoja kuwafikisha kwenye Baraza la Waaguzi na Wakunga kwa hatua za kinidhamu dhidi ya wanaokiuka maadili ya utoaji wa huduma za afya.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!