Friday, 5 February 2016

WALIOMUUA RUBANI WAZIDI KUSAKWA


Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence  Milanzi, amesema serikali itahakikisha inawasaka majangili wote waliohusika kumua rubani Rogers Gower, raia wa Uingereza.
 
Wakati serikali ikitoa tamko hilo, mwili wa rubani huyo umesafirishwa kwenda Uingereza kwa ajili ya maziko.
 
Gower anadaiwa kuuawa Januari 30, mwaka huu, kwa kwa kupigwa risasi akiwa katika helikopta wakati wa doria ya kukagua tembo  katika maeneo ya pori tengefu la Maswa, mkoani Simuyu.
 
Akizungumza jana na waandishi wa habari mjini Dodoma, Jenerali Milanzi alisema serikali kwa kushirikiana na jeshi la polisi wanaendelea na msako wa kuwatafuta majangili hao ambao walimpiga risasi rubani huyo, hivyo kushindwa kuendesha helikopta hiyo.
 
"Napenda kuwahakikishia kuwa yule raia wa Uingereza alipigwa  risasi ndio maana alishindwa kuindesha helikopta. Kama ingekuwa imelipuliwa yule aliyekuwa naye asingekuwa hai.
 
"Kwa kweli tukio hili limetusikitisha sana na linatuumiza. Tunasema  tutawatafuta huko walikojificha kuwe mapangoni au mistune,  tutawasaka na tutawakamata,” alisema.
 
Kuhusu taarifa zinazozagaa katika mitandao ya kijamii kuwa katika eneo hilo tembo waliuawa, alisema jambo hilo si la kweli bali aliuawa tembo mmoja.
 
Juu ya mabaki ya hrlikopta hiyo kuendelea kuwepo katika eneo la ajali, alisema wameshindwa kuitoa kutokana na wachunguzi kuendelea na kazi yao.
 
Katika hatua nyingine, mwili wa Gower, ulisafirishwa jana kwenda Uingereza kwa maziko. Tangu alipouawa, mwili wake ulihifadhiwa katika chumba cha maiti cha Hospitali ya Mount Meru ya Mkoa wa Arusha.
 
Saa nne asubuhi jana, katika eneo la chumba cha maiti cha Hospitali ya Mount Meru, baadhi ya wafanyakazi wenzake kutoka Mfuko wa Hifadhi wa Friedkin, walionekana wakisukuma chombo maalumu kilichobeba jeneza la rubani huyo na kuuingiza kwenye gari tayari kwa kuusafirisha hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
 
Ofisa mmoja wa kampuni inayoshughulikia huduma za maziko ya Corona Funerals and Repatriation Services, Nora Christopher, alisema mwili wa Gower ulitarajiwa kuondoka KIA saa 11:40 jioni kwa ndege ya Shirika la Qatar hadi Uwanja wa Ndege wa Heathrow, Uingereza.
 
“Tupo hapa kuuchukua mwili wa Gower hadi KIA ambako utasafirishwa kwenda Uingereza kwa maziko,” alisema.
 
Mapema wiki hii, ofisa kutoka Mfuko wa Hifadhi wa Friedkin, Pratik Patel, ambaye alikuwa akifanya kazi kwa karibu na marehemu alisema ndugu wa marehemu tayari waliwasili jijini hapa kwa vikao vya kushughulikia maziko hayo.
L Imeandaliwa na Peter Mkwavila, Dodoma na John Ngunge, Arusha  
 

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!