Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akijadiliana jambo na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Bw. Amos Makala walipokutana mjini Moshi kwa ziara ya ukaguzi wa miradi iliyo chini ya sekta ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Mkuu wa Wilaya ya Same Bw. Herman Kapufi akisisitiza jambo kwa wafanyakazi wanaofanya kazi katika kampuni ya Dott Services Limited inayojenga barabara ya Same-Mkumbara Km 96. Kulia ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa
wafanyakazi wa kampuni ya Dott Services Limited wakishangilia kwa furaha baada ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa kumtaka mkandarasi kuwalipa madai yao yote ifikapo Februari 26, mwaka huu.
Muoneano wa Jengo la Kituo cha Forodha cha pamoja (One Stop Border Post) kwa upande wa Tanzania lililopo Holili.
Ujumbe wa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa ukielekea katika kituo cha pamoja cha forodha (One Stop Border Post) kwa upande wa Taveta nchini Kenya.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akipata ufafanuzi wa namna ya kituo cha pamoja cha Forodha kinavyofanya kazi kutoka kwa Meneja Forodha kwa upande wa Taveta – Kenya Bw. Daniel Nyambaka.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akiagana na Meneja Forodha kwa upande wa Taveta – Kenya Bw. Daniel Nyambaka mara baada ya kukagua kituo hicho.
………………………………………………………………………………………………………
Serikali imesema iko mbioni kukamilisha mkataba maalumu wa ajira utakaotumiwa na makandarasi wote nchini katika kuajiri watanzania wazalendo kwenye miradi ya ujenzi inayosimamiwa na sekta ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasilino.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema hayo wakati akikagua ujenzi wa barabara ya Mkumbara-Same yenye urefu wa Km 96 mkoani Kilimanjaro.
Amemtaka mkandarasi Dott Services Limited kukamilisha hatua za mwisho za ujenzi wa barabara hiyo na kulipa stahili zote za wafanyakazi kwa mujibu wa mikataba.
“Nakupa mwezi mmoja kukamilisha ujenzi uliobaki wa barabara hii pia hakikisha kila mfanyakazi ambaye amemaliza mkataba wake analipwa stahili zake zote kwa muda usiozidi siku mbili”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Same Bw. Herman Kapufi kufatilia kwa makini madai ya wafanyakazi wazalendo ya malipo ya likizo, mafao ya NSSF, malimbikizo ya mishahara, matibabu na mazingira magumu ya kazi ili yalipwe sambasamba na madai mengine na hivyo kuondoa malalakimiko yaliyopo na yanayoweza kujitokeza mara baada ya kukamilika kwa mradi.
“Kuanzia sasa mameneja wa TANROADS wahakikishe kwenye ujenzi wa barabara na miradi iliyo chini ya wizara hii kazi ambazo watanzania wanaweza kuzifanya zisifanywe na wageni kwani hali hiyo huwanyima haki watanzania wenye ujuzi wa kuijenga nchi yao”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Naye Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) mkoa wa Kilimanjaro Eng. Marwa Rubirya amemhakikishia Waziri Mbarawa kuwa kwa sasa km 1,020 za mtandao wa barabara wilayani Same zinapitika na serikali imeanza kuongeza kiwango cha barabara za lami Wilayani humo ikiwemo ujenzi wa barabara ya Same-Kisiwani-Maore-Ndungu na Kihuriyo hadi Mkomazi.
Amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kwamba TANROADS itaendelea kuhakikisha barabara za milimani wilayani Same ambazo ni sawa na asilimia 75 ya barabara zote wilayani humo zinapitika wakati wote wa mwaka kutokana na umuhimu wake kwa shughuli za kiuchumi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Same Bw. Herman Kapufi amemuomba Waziri Mbarawa kuzipandisha hadhi barabara za Hedaru-Vunta-Miamba Km 41.2, Bangarara-Chome-Ikokoa Km 25.6, na Ndungu-Lugulu Km 8 ili zihudumiwe na TANROADS kutokana na umuhimu wake kiuchumi na kijiografia.
Katika hatua nyingine Waziri Mbarawa amekagua kituo cha pamoja cha forodha kilichopo Holili (Tanzania) na Taveta (Kenya) na kuona shughuli za usafirishaji na uchukuzi zinavyoendeshwa na kusisitiza umuhimu wa kituo hicho kufanyakazi kwa kushirikiana ili kuongeza mapato kwa nchi za Kenya na Tanzania.
No comments:
Post a Comment