WAZIRI wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba ameiagiza Polisi wilayani Mvomero na Mkoa wa Morogoro kuwasaka na kukitia mbaroni kikundi cha ulinzi wa jadi kiitwacho Mwano kwa tuhuma za kuua mbuzi na kondoo wapatao 80.
Mifugo hao ni kati ya 200 waliokuwa wakimilikiwa na mwanamke mjane wa jamii ya wafugaji wa Kimasai, Ketepoi Nuru ama Christina Nuru, mkazi wa Kijiji cha Kambara wilayani Mvomero, Morogoro.
Waziri alitoa agizo hilo katika mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Dihombo, Kata ya Hembeti baada ya kujionea baadhi ya mifugo iliyokuwa imekatwa kwa mapanga, baadhi ikiwa imekufa na mingine ikiwa na majeraha.
Tukio hilo lilijiri Februari 8, mwaka huu baada ya kikundi cha Mwano chenye watu takribani 50 kuvamia nyumbani kwa mwanamke huyo na kuishambulia mifugo hiyo zizini kwa kuikata mapanga.
Mwigulu alisema kitendo kilichofanyika ni cha kinyama na hakifai kabisa kuvumiliwa. Kikundi hicho baada ya kuvamia nyumbani kwa mwanamke huyo na kuua na kujeruhi mifugo 80, inaelezwa kwamba walichukua wengine zaidi ya 50 kwa bajaji na pikipiki na kutoweka nao.
No comments:
Post a Comment