Mwanamke wa kitongoji cha Buriba, kata ya Sirari, wilayani Tarime, anayejishughulisha na biashara ya kuuza kibanda cha duka, Sophia Manguye (46), amefanikiwa kuwanyang'anya majambazi watatu bunduki moja aina ya SMG yenye risasi 27, baada ya kupambana nao ndani ya kibanda chake cha biashara.
Majambazi hayo kabla ya kunyang'anywa bunduki, yalifanya uporaji katika vibanda kadhaa vya maduka na kufanikiwa kujikusanyia zaidi ya Sh. 180,000, pamoja na vocha za simu za mkononi kutoka maduka matatu tofauti.
Jambazi aliyeporwa bunduki hiyo na Sophia ni Gesanta Matinde (19), mkazi wa kijiji cha Kebeyo, kata ya Mbogi, ikiwa na risasi 27.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tarime/Rorya, Gemini Mushi, jana alisema tukio hilo la uvamizi na unyang'anyi kwa wafanyabiashara lilitokea juzi saa 2:00 usiku katika kitongoji cha Buriba, mji mdogo wa Sirari, baada ya majambazi watatu waliokuwa na silaha aina ya SMG namba UK 5115 kuwavamia wafanyabiashara hao.
“Awali majambazi hao waliingia duka la Zaituni Magasi lililopo jirani na la Sophia na kupora fedha taslimu Sh. 100,000 kabla ya kuingia dukani kwa Sophia na kupora 80,000 za mauzo, lakini hawakuridhika na kiasi hicho, hivyo kuingia ndani na kuanza kutafuta fedha nyingine,” alisema Kamanda Mushi.
Hata hivyo, Kamanda Mushi alisema wakati wakiendelea kupekua kutafuta fedha nyingine, mwanamke huyo alimvamia jambazi aliyekuwa na silaha kisha kumng’ang’ania kwa nguvu, huku akipiga kelele za kuomba msaada hadi walipojitokeza wananchi na polisi waliokuwa karibu kutoa msaada.
Kamanda Mushi alisema baada ya tukio hilo, majambazi wawili walifanikiwa kutoroka, huku mwanamke huyo akipata majeraha usoni na mikononi wakati wa kupambana na majambazi hao.
Alisema Jeshi la Polisi limempongeza mwanamke huyo kwa ujasiri aliouonyesha pamoja na wananchi waliojitokeza na kuongeza nguvu na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa na bunduki hiyo ambayo ingeleta madhara makubwa kwa wananchi.
Aliwaomba wananchi kushiriki ulinzi shirikishi kwa kutoa taarifa za uhalifu kwa jeshi hilo mapema kabla ya matukio.
Alisema kwa sasa wanaendelea kumhoji mtuhumiwa na wengine wawili waliotoroka wakitafutwa ili waweze kufikishwa katika vyombo vya sheria.
NIPASHE
No comments:
Post a Comment