Wednesday 24 February 2016

MWANAMKE MBARONI KWA KUSUKA MIPANGO YA UJAMBAZI


Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limemkamata mwanamke anayedaiwa kuwa kinara wa kusuka mipango ya  kufanikisha wizi wa fedha za wateja katika benki mbalimbali.
 
Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, alisema jana kuwa mwanamke huyo (jina linahifadhiwa kwa sababu za kiuchunguzi), anashikiliwa na watuhumiwa wengine wanne ambao walikuwa wakishirikiana kufanikisha wizi huo.
 
Sirro aliwataja watuhumiwa wenzake kuwa ni Mohamed Hassan (21) maarufu kama Kidali, mkazi wa Vingunguti Spenko, Adam Salum (23) mkazi wa Buguruni kwa Madenge,  Hamis Ally (20) na Bakari Hamis (19) wote wakazi wa Buguruni kwa Mnyamani.
 
Alisema watuhumiwa hao ambao wamekuwa wakifanya unyang’anyi wa kutumia silaha, walikamatwa Alhamis iliyopita eneo la Buguruni kwa Mnyamani.
 
Kamishna Sirro alisema mwanamke huyo amekuwa akienda benki na kukaa humo kama mteja kisha kuangalia mteja anayetoa kiasi kikubwa cha fedha na kuwasiliana na watuhumiwa wenzake ili kufanikisha uporaji.
 
“Amefanikisha matukio mengi ya unyang’anyi wa kutumia silaha katika benki tofauti. kazi yake ni kukaa ndani ya benki kama mteja na kuangalia wale wanaotoa fedha nyingi kisha kuwasiliana na wenzake wa nje,” alisema.
 
Aliongeza kuwa: "Yapo matukio mengi ambayo ameyataja kuwa aliyafanikisha kutendeka. Tunaendelea na uchunguzi.”
 
Alisema watu hao walikamatwa baada ya polisi kupata taraifa kutoka kwa msiri wao kuwa kuna majambazi yanajiandaa kuvamia maduka eneo hilo.
 
"Watuhumiwa walikiri kufanya matukio mbalimbali ya uhalifu wa kutumia silaha. Mojawpao ni tukio lililotokea Februari 14, mwaka huu, huko Ivan Min Supermarket. Juhudi za kuitafuta silaha waliyoitumia zinaendelea", alisema.
 
Kamishna Sirro alisema mwishoni mwa wiki iliyopita, wamefanikiwa kuzikamata silaha mbili aina ya SMG iliyokatwa mtutu yenye namba 56-1-2803795 ikiwa na risasi 24 kwenye magazini.
 
Nyingine aliitaja kuwa ni bastola aina ya Browning yenye namba A 671123 na TZ CAR 98580 ikiwa haina risasi kwenye  na magazini ambayo haina risasi.
 
Alisema silaha aina ya SMG ilipatikana baada ya kukamatwa watu wawili wanaodhaniwa kuwa majambazi, waliokuwa wakikimbia baada ya kufanya uporaji wa Sh. milioni 12.
 
Alisema fedha hizo ambazo ni mali ya David Isack (32), mkazi wa Mafinga mkoani Iringa, ambaye wakati wa tukio, alikuwa akitoka benki ya NMB tawi la Airport kuzipeleka benki ya DTB, jengo la Quality Plaza, barabara ya Nyerere, Dar es Salaam.
 
Alisema wakati yuko njiani, alivamiwa na watu watano waliokuwa kwenye pikipiki mbili aina ya Boxer na kumpora begi lenye fedha kisha kupiga risasi mbili hewani.
 
Alisema baada ya polisi kupata taarifa hizo, waliwafuatilia ndipo majambazi hao waliposhuka kwenye pikipiki na kukimbia kwa miguu.
 
“Tumefanikiwa kuwakamata wawili wakiwa na pikipiki zao zenye namba MC. 729 ATZ na MC.557 AZK. Wengine tunaendelea kuwasaka,” alisema.
 
Kuhusu bastola aina ya Browning, Sirro alisema ilipatikana eneo la Kiwalani kwa Gude, baada ya polisi kupata taarifa za kuwepo kwa watu wamekaa kichakani ambapo baada ya kuwafuatilia walikimbia na kuidondosha.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!