Wednesday, 10 February 2016

MRAMBA, YONA WAFUNGUKA MAISHA GEREZANI.




Mawaziri wa zamani, Basil Mramba na Daniel Yona.
Mawaziri wa zamani, Basil Mramba na Daniel Yona, wanaotumikia kifungo cha nje kwa kufanya shughuli za kijamii, wamefunguka kuhusu maisha ya gerezani sambamba na sababu ya kuomba kutumikia adhabu hiyo.


Mramba na Yona, walihukumiwa kutumikia adhabu hiyo Februari 5, mwaka huu, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya  na kupeleka barua ya kuomba kutumikia kifungo cha nje kupitia wakili wao, baada ya kubainika kutenda kosa la matumizi mabaya ya madaraka.
Mramba ambaye alikuwa Waziri wa Fedha na Yona Waziri wa Nishati na Madini, jana walifika katika Hospitali ya Sinza Palestina, jijini Dar es Salaam na kuanza kutumikia adhabu hiyo  kwa kudeki eneo la baraza katika jengo la kinamama.
Mramba akizungumza katika eneo hilo, alisema: “Adhabu hii tunaifurahia kwa sababu tuliomba kuitumikia kupitia kifungo cha nje.”
Alisema hawaoni taabu kwa kuwa walizoea kufanya kazi nyingi enzi za ujana wao kama kilimo na ufugaji. 
Alifafanua kuwa waliona ni bora kutumikia kifungo cha nje kwa kufanya shughuli za kijamii kuliko kukaa tu gerezani bila kazi.
Alisema kifungu cha sheria kinachowapa adhabu wafungwa, hakielekezi vizuri aina ya utekelezaji wa adhabu hivyo kushauri  kielekeze adhabu kulingana na taaluma ya mtuhumiwa kama nchi zilizoendelea zinavyofanya.
 “Kwa mfano kuna wataalamu wengi wa afya kama madaktari wanaotumikia adhabu ya kifungo cha nje. Ni  vyema wakapelekwa kwenye hospitali kutoa huduma za matibabu kama zinavyofanya nchi zingine mfano Marekani, badala ya kuwafanyisha usafi. Sisi tunafanya kwa sababu ndiyo kazi tuliyopangiwa,” alisema.
WADEKI KIBARAZA KWA DK. 30
Mramba na Yona waliripoti katika hospitali hiyo majira ya saa 2:00 asubuhi na kuanza kuelekezwa maeneo ya kufanya kazi. Hata  hivyo walitumia nusu saa kudeki eneo hilo kuanzia saa 2:50 hadi saa 3:20 huku wakisaidiwa kubeba maji na Frank Mrema ambaye ni kijana wa usafi katika hospitali hiyo.
"Kazi hii kumbe lazima uwe na kaujuzi eeeh,” alisikika Mramba akimweleza Yona wakati wakipata shida ya kudeki eneo hilo.
Yona ambaye alionekana kuwa mjuzi wa kufanya kazi hiyo kwa haraka na wepesi kuliko Mramba, ambaye mara nyingi alikuwa akiomba kuelekezwa, aliendelea kudeki huku akisema kazi hiyo ya usafi ni kama sehemu ya jukumu la kazi anazotakiwa kuzifanya kila siku.
Naye Ofisa Mazingira wa Hospitali hiyo, Mariam Mongi, alisema Mramba na Yona waliripoti katika hospitali hiyo kwa wakati na walianza kuelekezwa eneo la kazi pamoja na kupewa watu wa kuwaelekeza.
“Unajua hawa ni wazee. Hatuwezi kuwapatia kazi ngumu za kuwachosha sana, hivyo leo walifanya kazi ya kudeki na kusafisha eneo la jengo la wazazi lakini pia kesho tutawapa kazi ya kusafisha vioo vya jengo la wazazi,” alisema.
Ofisa Kiongozi wa Huduma za Jamii wa Jiji la Dar es Salaam, Deogratius Shirima, alisema kazi hiyo wataifanya kwa siku tano za wiki kwa saa nne na watakuwa wakiripoti kwa mganga mfawidhi wa hospitali hiyo au kwa kiongozi aliyepangiwa kuwapokea kila siku.
Hatua hiyo inatokana na Mramba na Yona, kupitia mawakili wao kuwasilisha barua yenye kumbukumbu namba 151/DA/3/11/223 ya Desemba 5, mwaka jana katika mahakamani ya Kisutu kutoka magereza kuhusu kutumikia kifungo cha nje.
Kabla ya kubadilishiwa adhabu na kuwa ya kifungo cha nje, Mramba na Yona walikuwa wakitumikia kifungo cha miaka miwili kila mmoja gerezani baada ya kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishai serikali hasara ya Sh. bilioni 11.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!