Tuesday, 9 February 2016

MAHAKAMA YAPEWA SH.12.3 BILIONI ZA KUANZA KESI ZA WAKWEPA KODI.



Siku chahe baada ya  Rais Dk. John Magufuli kuitaka Mahakama kumaliza kesi 442 za wakwepa kodi, ambazo zinaweza kuipatia serikali Sh. trilioni moja, mhimili huo umepewa Sh. bilioni 12.3 za kujiendesha.
 
Kutokana na kupewa fedha hizo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, amesema ana imani zitasaidia uendeshwaji wa kesi ikiwa pamoja na zile zinazohusu ukwepaji kodi.
 
Akizungumza wakati wa kilele cha Siku ya Sheria nchini, alipokuwa mgeni rasmi kwa mara ya kwanza katika uzinduzi wa Mwaka wa Mahakama, Rais Magufuli alisema mahakama ilikuwa inapewa bajeti ya Sh. bilioni 41, lakini mwaka 2015/2016 ilishuka hadi Sh. bilioni 12 ambazo hadi sasa haijapewa. 
 
“Kiongozi lazima ufikirie wapi pa kupeleka fedha na wapi pa kunyima, watu wa mahakama mnafanya kazi ya Mungu, nawaahidi ndani ya siku tano nitakuwa nimewapa Sh. bilioni 12 zote.
 
“Sina tatizo la masilahi ya wafanyakazi wa mahakama, katika bajeti ya mwaka huu nitawapa fedha nyingi kuliko bajeti zote zilizopita, fedha zipo,” alisema.
 
Alisema pia kwamba kuna kesi 442 za ukwepaji kodi ambazo kama zingeamuliwa serikali ingepata Sh. trilioni moja, ambayo ingeweza kununua ndege sita.
 
Alimwuomba Jaji Mkuu kuzimaliza kesi hizo na kama zitamalizika kati ya fedha hizo, ataipatia Idara ya Mahakama Sh. bilioni 259 na Sh bilioni 750 zilizobakia zitanunuliwa ndege sita na wafanyafakazi 250 wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) waliopo sasa wataondolewa.
 
Akikabidhi hundi ya Sh. bilioni 12.3 jana, Dk Mpango alisema: “Fedha hizi ni za maendeleo ili zisaidia mahakama kufanya kazi na kuondoa mrundikano wa kesi zikiwamo kesi za kodi, ambazo tunaamini nyingi zitaamuliwa kutusaidia upande wa seriklali kupata mapato.”
 
Naibu Katibu  Mkuu  Wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju, alisema  sasa kesi hizo zitasikilizwa baada ya Rais kutekeleza ahadi yake kwa kuipatia mahakama aliyoahidi wakati wa maadhimisho ya sheria  Februari 4, mwaka huu.
 
Mpanju alisema walipokea maombi ya fedha kutoka kwa mahakama hiyo ya kuhusu uhaba wa fedha za kuendesha shughuli zake unaoikabili.
 
 “Tunamshukuru Rais kutekeleza ahadi yake aliyoiahidi kwa wakati. Hii  inaakisi ile kaulimbiu yake ya hapa kazi tu. Tunaamini fedha hizi pamoja na mambo mengine zitasaidia kusikiliza kesi za wakwepa kodi,” alisema Mpanju.
 
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Idara ya Mahakama, Hussein Katanga, alisema fedha hizo zitasaidia mahakama katika miradi yake mbalimbali ikiwamo ya ujenzi wa mahakama nchini.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!