Tuesday, 9 February 2016

MAJI MACHAFU SEKONDARI YA MANZESE KUIZALISHIA UMEME KILOWATI 50


Shule ya Sekondari Manzese, jijini Dar es salaam, iliyoko katika barabara ya Makanya, kwenye Kata ya Manzese imeonyesha kupiga hatua kubuni mradi endelevu wa kutumia gesi itokanayo na majitaka kuzalisha nishati na imenufaika na mradi mkubwa wa kuzalisha nishati endelevu ya Biogesi

Ingawaje si shule ya kwanza kufanya hivyo, lakini ukweli unaendelea kubaki kwamba, ni wenye manufaa, kwa maana kuwa, ni kigezo cha ubunifu na bado ni kipya katiia jamii.
Kuna baadhi ya shule zinatajwa kufanya hatua kama hiyo, ikiwemo moja katika Manispaa ya Ilala eneo la Pugu na nyingine Bagamoyo.
Mradi huo sasa unatekelezwa na Mamlaka ya MajiSafi na MajiTaka Dar es Salaam (DAWASA ) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuendeleza Nishati Asilia na Uhifadhi wa Mazingira (TaTEDO), pamoja na Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa UN- HABITAT.
Lengo la mradi huo, ni kuitumia changamoto ya uhifadhi wa majitaka na kinyesi kutoka vyoo vya shule hiyo, ili kupata gesi itakayosaidia upatikanaji umeme mbadala, kwa matumizi mbalimbali na kuboresha taaluma kwa wanafunzi.
Athari za ukosefu wa nishati ya umeme ni kikwazo kwa wanafunzi wanaosoma masomo hasa ya sayansi shuleni, kwani mahitaji ya ufundishaji wake na hususan maabara, inategemea mno umeme .
Pia, umeme una nafasi yake katika baadhi ya sehemu nyeti katika huduma za umma,kama vile hospitalini na mara nyingine, huduma hiyo inapokosekana, kunakuwepo matukio yanayokaribia kuhusiana na  vifo.
Mradi huo WA umeme utokanao Na kinyesi  umekuwa mkombozi, kwa kutunzaji mazingira katika shule hiyo ya Manzese, wanafunzi wananufaika kwa kujifunza kwa vitendo katika kutumia maabara, iliyounganishwa na mfumo wa nishati endelevu ya Biogesi.
MKUU WA SHULE ANASEMAJE?
Mkuu wa Shule ya Sekondari Manzese, Linus Mwakasege, anasema mradi huo umekuwa msaada katika matumizi ya nishati ya shule hiyo na kukuza taaluma kwa wanafunzi katika masomo yao.
Anasema, hivi sasa shule hiyo imegeuka kituo cha mafunzo kwa watu mbalimbali kuzuru kujifunza kwa ushuhuda, jinsi mitambo inavyofanya kazi.
Mwalimu Mwakasege anasema, hivi sasa 
shule yake ina wanafunzi 1400, hivyo matumizi ya gesi yatawasaidia wanafunzi kwenye masomo ya sayansi, kupitia maabara ya shule, imewekewa mifumo ya usambazaji gesi. Sasa ujuzi huo unafanyiwa kazi na shule zinginezo.
“Hivi sasa tunatumia gesi hiyo kwa kupikia, kwani maabara ipo katika hatua ya mwisho kukamilika na kufungwa mifumo maalumu ya kupokea gesi na kuanza kutumika,” anasema Mwalimu Mwakasege.
Anasema, kuwepo mradi huo kumepunguza matumizi ya umeme na kununua mafuta ya taa mara kwa mara kwa shughuli za kupikia na kuwa msaada kwa matumizi ya maabara pale itakapokamilika, kwani inahitajika gesi nyingi kwa ajili ya kuendesha maabara hiyo.
“Katika kukamilisha mifumo mzima wa matumizi ya gesi hii wafadhili walitupa ahadi kuwa watatuletea jenereta, ambayo inatumia gesi na sisi kuwa na mfumo wetu na hapo ndipo tutaachana kabisa na matumizi ya umeme wa Tanesco,” anasema.
VYOO VYA SHULE
Mwakasege anasema, vyoo vya shule hiyo vilikuwa vinatoa harufu iliyokuwa kero kwa wanafunzi, walimu na hata majirani wa shule hiyo.
Anasema, harufu ya vyoo ilikuwa imezoeleka katika maeneo ya shule hiyo, kutokana na vyoo hivyo kuanza kujaa na kusababisha wanafunzi wanapoingia kutoka na harufu katika nguo zao.
“Vyoo vyetu vilikuwa vinatuzidi kwa kujaa na kuzidi kwa harufu ya kinyesi hapo, ndipo wazo la kutafuta wafadhili kutusaidia katika mradi huu ndipo ulianza na kufanikiwa kupata msaada,”anasema Mwakasege.
Mkuu huyo wa shule anaeleza kuwa, mradi huo umesaidia kuongeza uelewa wa utunzaji wa mazingira kwa wanafunzi kwani wakati mradi unatekelezwa, wanafunzi walikuwa wanapewa elimu ju ya utunzaji mazingira na jinsi ya kutengeneza mitambo ya kuzalisha gesi asilia.
Anafafanua kuwa, mazingira ya shule hiyo hivi sasa ni ya kuvutia, kwani mbali na majitaka ya kinyesi kuzalisha umeme mbadala, pia maji hayo yamebadilishwa kuwa mbolea ya kumwagiliwa kwenye bustani ya shule.
Mwakasege anasema kuwa, vyoo vya shule hiyo vimekuwa visafi na hakuna harufu inayotoka, kwani mfumo huo unazuia harufu kutoka nje ya choo.
MANUFAA KWA MAJIRANI 
Anasema kuwa, wanategemea uzalishaji wa gesi hiyo ukiwa mkubwa, kuwaunganisha na wakazi wanaozunguka shule hiyo, kwa makubaliano maalumu kwa ajili ya matumizi ya nyumba zao.
“Hivi sasa gesi inayozalishwa inakidhi mahitaji yetu , lakini wataalamu wametushauri kwamba, endapo uzalishaji na matumizi yakiwa makubwa, kinyesi zaidi kitahitajika, hivyo tutalazimika kuunganisha vyoo vya wakazi kuingia katika mitambo yetu,” anasema Mwakasege.
Anaongeza kuwa, wanatarajia kufanya mazungumzo na wakazi wa eneo hilo, kuangalia uwezekano wa kushirikiana, ili kuitumia changamoto ya majitaka kuwa malighafi inayoweza kupunguza gharama za maisha,” anasema.
DAWASA YAELEZEA 
 Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka  ya Jiji la Dar es Salaam(Dawasa), Nelly Msuya, anasema kuna changamoto ya kuwepo majitaka katika jamii, hivyo kufanikiwa mradi huo, ni ukombozi mkubwa wa kudhibiti majitaka kwa faida ya jamii.
Anasema, baada ya kutambua kuwa zaidi ya asilimia 80 ya majisafi yanayotumika, hugeuka kuwa majitaka, kiasi hicho cha majitaka kisipodhibitiwa ipasavyo, neema hiyo ya ongezeko la majisafi inaweza isionekane. Anafafanua akisema:
“Kwa hivi sasa, Shule ya Sekondari Manzese, haitalazimika kufikiria majitaka hayo yaende wapi, baada ya kujaa? 
“Kwani, Dawasa imetoa suluhisho na imechukua jukumu la kuhakikisha maji hayo yanatumika kuzalisha gesi ambayo ni rafiki kwa mazingira na afya za wanafunzi.” 
Anasema, sanjari na ujenzi wa mtambo hiyo ya gesi, pia ni wakati kwa shule za sekondari kote nchini kuwekeza katika matumizi ya nishati endelevu ya biogesi, ili kulinda na kuhifadhi mazingira, hasa katika kipindi kilichopo cha mlipuko wa kipindupindu.
“Sisi kama Dawasa, tunauona mradi huu kama mkombozi kwa wanafunzi hawa na mfano wa kuigwa kwa shule nyingine zilizoko ndani na nje ya jiji la Dar es Salaam zinazokabiliwa na uhaba wa nishati ya umeme na gesi,” anasema.
Mwakasege anasema, matumizi ya gesi yataimarisha utoaji mafunzo kwa vitendo, kwa wanafunzi wanaosoma michepuo ya sayansi kupitia maabara ya kisasa, inayojengwa shuleni hapo.
KINGA YA KIPINDUPINDU
Msuya, anasema kuwa kutokana na kuwepo kwa ugonjwa wa mlipuko wa kipindupindu, mradi huo utakuwa kinga mojawapo, kwani unapunguza uchafu na kutunza mazingira.
Anayataja maeneo yaliyoathirika kwa kiasi kikubwa na kipindupindu, kuwa ni Manzese, Buguruni, Kigogo, Mburahati, Kinondoni Mkwajuni na Tandale, hivyo wakazi wake wakiwa na elimu ya kutekeleza mradi huo, wanaweza kupunguza kasi ya maambukizi ya ugonjwa huo.
“Shule ya Sekondari Manzese ambayo ipo katika eneo ambalo limeathirika na kipindupindu kwa kiasi kikubwa, mradi huo umesaidia kupunguza hofu ya maambukizi ya ugonjwa huo kwa wanafunzi, kwani inzi wanaotoka vyooni, ndio wanasambaza kwa haraka ugonjwa huo, lakini kwa hivi sasa vyoo ni visafi,” anasema.Nelly.  
Anaongeza, kwa kutambua umuhimu wa uondoshaji wa majitaka na kampeni za kukomesha ugonjwa wa kipindupindu Dawasa, ipo mbioni kujenga mitambo yenye uwezo wa kutibu lita milioni 241 za majitaka kwa siku katika manispaa zote tatu za Jiji la Dar es Salaam.
Mitambo hiyo itajengwa maeneo ya Mbezi Beach (Kinondoni), Jangwani (Ilala) na Kurasini (Temeke), ambapo wateja wakatakaounganishwa katika mfumo wa majitaka wataongezeka  kutoka 18,568 hadi 25,000 katika mwaka 2015/2016.
TaTEDO YANENA  
Naye Mratibu wa Mradi huo kutoka taasisi ya TaTEDO, Shima Sago, anasema kukamilika kwa mradi huo, utakuwa na faida nyingi kwa jumuiya shule na jamii inayoizunguka shule.
Shima anazitaja faida hizo kuwa ni pamoja na gesi hiyo itakuwa ya bei nafuu, kutokana na malighafi kupatikana shuleni hapo na nishati hiyo inajitosheleza kwa mazoezi ya wanafunzi maabara, kupikia kantini, kuwasha taa kwa ajili ya wanafunzi kujisomea na ulinzi wa mazingira ya shule. 
Shima anasema, faida nyingine ni kutibu majitaka yanayotoka vyooni na kuondoa athari ambazo ni chanzo cha magonjwa hatari kwa wanafunzi na jumuiya nzima inayoizunguka shule.
Aidha, Shima anasema kuwa, gesi itakayozalishwa katika mradi huo ni ujazo wa mita za ujazo 200, zitakazokuwa na uwezo wa kuzalisha umeme kilowati 50, unaotosha matumizi ya shule.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!