Jengo la ghorofa 16 lililopo Mtaa wa Indira Gandhi, wilayani Ilala limeanza kubomolewa na mafundi wa Kampuni ya Patty Interplan baada ya kupewa kazi hiyo na Manispaa ya Ilala.
Maandalizi ya ubomoaji wa jengo hilo yalianza wiki iliyopita kwa mafundi kufunga nguzo maalumu za kurahisisha ubomoaji na kufunga barabara zinazozunguka jengo hilo.
Mmoja wa mafundi ambaye alikataa kutaja jina kwa kuwa siyo msemaji, alisema ubomoaji wa maghorofa huanzia juu na kuteremka chini. “Kama unavyoona ghorofa ya 16 ndiyo tunamalizia kuibomoa, kesho (leo) tutakuwa tumeimaliza na tutaanza kubomoa ghorofa ya 15,” alisema.
Alisema wameanza kubomoa ghorofa ya juu na wataendelea kushuka hadi chini.
Kampuni hiyo ilipewa kazi ya kubomoa jengo hilo kwa gharama ya Sh1 bilioni zitakazolipwa na mmiliki wake, Ali Raza Investment. Serikali iliamua jengo hilo livunjwe baada ya kujengwa chini ya kiwango. Hatua hiyo ilikuja baada ya jengo lake pacha kuanguka na kuua watu 37 na wengine 18 kujeruhiwa.
Baada ya ubomoaji kusuasua, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alitoa siku 18 kwa uongozi wa Manispaa ya Ilala kubomoa jengo hilo akisema litasababisha maafa.
MWANANCHI.
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment