HEBU fikiria. Mama yako kipenzi ambaye umemwacha kijijini baada ya kwenda kutafuta maisha na ambaye kila kipindi cha likizo unaungana naye na kufurahia chakula cha asili cha nyumbani unasikia ameuawa kinyama kwa kukatwa mapanga.
Ukiwa umetaharuki baada ya kusikia habari hiyo mbaya, unahoji sababu ya mauaji ya mpendwa wako, unaambiwa eti ni kutuhumiwa kuwa mchawi! Kwamba watoto wawili waliokufa pale mtaani; mmoja kwa kipindupindu na mwingine kwa malaria sasa kibao kageuziwa yeye kuwa ndiye ‘kipindupindu na malaria’ baada ya wazazi wa watoto hao kwenda kupiga ramli chonganishi kwa waganga matapeli!
Yaani miaka yote alipokuwa binti mdogo hadi mama mtu mzima hakuwa mchawi lakini baada ya kuzeeka tu na macho yake kuwa mekundu kutokana kupikia kuni zinazotoa moshi kwa muda mrefu sasa ni mchawi. Unabaki umeshika tama ukitamani kuwameza waliomuondoa duniani mama yako kabla ya muda lakini huna uwezo huo. Tatizo lajichimbia Licha ya juhudi mbalimbali za serikali na wadau wengine kufanyika ili kukomesha mauaji ya wazee katika mikoa ya Kanda ya Ziwa Victoria kutokana na imani za ushirikina, tatizo hilo limeendelea kujichimbia.
Kutokana na kuota mizizi, imefikia suala la mauaji ya wazee kuonekana kama jambo la kawaida na sio habari mpya, licha ya wanaopoteza ndugu, jamaa, marafiki na majirani kwa ujumla kubaki katika simanzi na majonzi makubwa. Ukweli kwamba tatizo la mauaji ya wazee bado liko juu, unadhihirishwa na takwimu kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani zinazoonesha kuwa kati ya mwaka 2012 na 2014 kulikuwa na matukio ya mauaji ya wazee takribani 1,100 yanayohusishwa na ushirikina katika kanda hiyo ya Ziwa Victoria pekee.
Hii ni mbali na maeneo mengine nchini ambako tatizo hilo si kubwa. Wadau kupambana zaidi Ingawa hali bado ni tete kama ambavyo takwimu zinavyoonesha, hii haijaweza kuzuia wala kuwakatisha tamaa wadau mbalimbali katika kuendelea na juhudi zao za kupambana na ukatili huo wa kinyama dhidi ya wazee wasio na hatia.
Ni kutokana na uzito wa suala hilo na katika kutekeleza kwa vitendo dhana ya kutokata tamaa hadi mafanikio yapatikane, Shirika lisilo la Kiserikali la HelpAge International Tanzania, kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani, waliona umuhimu wa kukutana na wadau mbalimbali mwishoni mwa mwaka jana ili kusaka mbinu za kukomesha mauaji haya.
Lengo lilikuwa ni kutathmini kwa kina juu ya juhudi zilizofanyika miaka ya nyuma katika kudhibiti mauaji ya wazee Kanda ya Ziwa, mafanikio yaliyojitokeza, changamoto na kuweka mikakati bora zaidi ya kuendeleza mapambano. Waandaji hao walichagua jiji la Mwanza kuwa kituo cha mkutano huo muhimu wa mwaka kwa ajili ya kukaa pamoja na kufanya mapitio ya mapambano dhidi ya unyanyasaji na mauaji ya wazee katika mikoa ya kanda ya Ziwa ya Mwanza, Geita, Shinyanga, Simiyu, Mara, Kagera na Tabora.
Mkutano huo wa siku mbili ulifanyika katika ukumbi wa Gold Crest kati ya Desemba 28 na 29 uliwashirikisha jumla ya wadau 60 kutoka kada mbalimbali, wakiwemo makamanda wa Polisi kutoka mikoa ya kanda hiyo, maofisa waandamizi kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani na maofisa kutoka Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Wengine walikuwa ni maofisa kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, wawakilishi wa wazee, mashirika yasiyo ya kiserikali yaliyo katika mapambano dhidi ya ukatili na mauaji ya wazee, wabunge pamoja na waandishi wa habari walio kwenye Mtandao wa kupambana na ukatili wa kijinsia na mauaji ya wazee. Doa kwa nchi Akifungua mkutano huo, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, John Mngodo alisema suala la mauaji ya wazee linaitia doa nchi yetu inayosifika kwa amani duniani kote.
Ni kwa kuliona hilo akataka juhudi za makusudi zichukuliwe ili kukomesha mauaji hayo ya kikatili yanayoliandama kundi hilo la jamii lisilo na kosa. “Ili kukomesha kabisa tatizo la mauaji ya wazee nchini hatuna budi kuhamasisha jamii yote kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa kuachana na imani potofu za ushirikina ambazo ndizo zinazochangia kwa kiasi kikubwa uwepo na kukua kwa tatizo hili katika Kanda ya Ziwa,” anasema Mngodo.
Aidha, Mngondo anasema Serikali itajitahidi kupitia Sera ya Taifa ya Wazee na Sheria mbalimbali zilizopo ili kuangalia iwapo kuna haja ya kuboreshwa zaidi kwa kuweka msisitizo katika kuthamini haki za wazee nchini. Matumizi ya sheria “Kuna hatua zaidi zinatakiwa kuchukuliwa ikiwemo kupambana na waganga wa jadi wanaopiga ramli chonganishi.
Tunatakiwa kuchukua hatua stahiki kwa wote wanaohusika na mauaji haya, kutoa elimu kwa jamii ili iachane na imani potofu za kuamini ushirikina katika kila jambo,” anasema. Anasema vita dhidi ya mauaji ya wazee na namna zote za ukatili kwa binadamu itafanikiwa tu iwapo kila mmoja atatimiza wajibu wake wa kufichua, kuelimisha na kutenda haki.
Mngodo pia anaiasa jamii kubadili mtazamo juu ya wazee na kwamba suala la kukabiliana na ukatili na mauaji ya kundi hilo si la Jeshi la Polisi peke yake bali ni la watu wote. Naye Mkurugenzi wa HelpAge International Tanzania, Smart Daniel, mbali na kuishukuru serikali kwa kuwa tayari kushirikiana na wazee katika mapambano hayo na kutoa uzito unaostahili, anawaomba wanahabari nchini kuandaa mtandao utakaowezesha kukomesha mauaji hayo kwa kutumia vyema umahiri wa taaluma zao.
Daniel anasema siku zote utamaduni wa Mtanzania umekuwa ni kuwaenzi wazee, hivyo vitendo vya kinyama dhidi yao, hasa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, vinaupaka matope utamaduni na sifa nzuri ambayo nchi imekuwa nayo kimataifa. Anasema katika kuwaenzi wazee, nchi mbalimbali duniani zinatoa huduma za afya, vipato na mazingira wezeshi kwa kundi hilo. “Kutokuwepo kwa Sheria ya Wazee hapa nchini kunawanyima wazee haki hizo. Wazee ni tunu ya taifa.
Tukiandaa vizuri maisha yao na kuwatumia vyema taifa litanufaika kwani nchi zinazowatumia ipasavyo wazee zinanufaika nao sana,” anasema. Mkurugenzi huyo wa HelpAge anaipongeza serikali kwa kuingiza wazee kwenye Wizara ya Afya, hali inayoonesha dhamira njema ya kutambua umuhimu wao katika jamii na kuwajali ipasavyo, jambo linalowatia moyo wazee.
Wazee kuonekana mzigo Wakijadili changamoto na madhila mbalimbali wanayokumbana nayo wazee, washiriki wa mkutano huo wanabaini kuwa wazee wengi ni waathirika wa vitendo vya unyanyasaji unaofanywa kwa makusudi na ndugu zao, jamaa wa karibu au hata jamii inayowazunguka. Kwamba hali hiyo huja baada ya kuwaona wao kuwa ni mizigo na kero kwao badala ya kuwaona ni tunu huku wazee wa jinsi ya kike wakiwa ni waathirika wakubwa wa mauaji hayo.
Inadaiwa kuwa kukosekana kwa elimu ya dini kwa wakazi wengi katika jamii ya Kisukuma ni sababu mojawapo inayotajwa kuchangia mauaji ya wazee kwa ujumla. Kufukuzwa, kunyang’anywa mali Madhila mengine yanayowasibu wazee ni kunyang’anywa mali, ardhi, mifugo, kupuuzwa, kutoheshimika, kutukanwa, kunyimwa chakula na mahitaji mengine muhimu ya kibinadamu, sambamba na kufukuzwa kwenye maeneo yao kwa tuhuma za uchawi.
Wanasema, madhila haya ni sawa na mauaji mengine ya kukatwa mapanga kwa kuwa yanaumiza nafsi. “Kuua si kukata mapanga tu. Kunyang’anywa mali, nyumba, mazao au kudharauliwa na kudhalilishwa ni aina nyingine mbaya mithili ya mauaji,” anafafanua Clotilda Kokupima, Katibu Mtendaji Shirika la Wazee la Kasulu mkoani Kigoma. Tusiwaite ‘vikongwe’ Theresia Minja ambaye ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Linda Jamii jijini Arusha anatoa angalizo mahsusi kwa vyombo vya habari nchini kuacha mara moja kutumia neno “vikongwe” kwa kuwa linadhalilisha, linawanyanyapaa na kuondoa utu wa wazee.
Minja anasema neno “vikongwe” linaonekana kama vitu na sio watu; na kwamba wananchi walipozoea kusoma ‘mauaji ya vikongwe’ wamejikuta wakipatwa na mtazamo mbaya. Anasema pia mauaji ya wazee yamekuwa hayapewi kipaumbele kama ambavyo yanapewa mauaji ya albino ambapo albino mmoja akiuawa habari inakuwa kubwa kuliko hata mauaji ya wazee 10.
“Mauaji ya wazee yanatakiwa yatofautishwe na mauaji ya watu wengine na yapewe umuhimu wa pekee kama yanavyopewa mauaji ya albino,” anasema. Mbunge wa Jimbo la Buchosa, Dk Charles Tizeba, anatoa sababu nyingine wazee kutendewa isivyo akidai kwamba wakati mwingine wao wanachangia hali hiyo. Anasema ukosefu wa upendo kwa wajukuu wao ni moja ya sababu ya kunyanyaswa kwao.
Hofu ya kutoa taarifa Mbunge huyo pia analinyooshea kidole Jeshi la Polisi akisema limekuwa kikwazo kingine katika kufichua wahalifu wa vitendo viovu wanavyofanyiwa wazee. “Kuna dhana iliyojengeka miongoni mwa jamii kuwa iwapo mtu atatoa taarifa yoyote ya uhalifu au mauaji Polisi, yeye anakuwa wa kwanza kurundikwa ndani kuisaidia Polisi.
Kitendo hicho kinawatia hofu wananchi kiasi kwamba hawako tayari kutoa taarifa kwa kuogopa ‘kuisaidia Polisi’,” anasema Dk Tizeba. Kisha anahoji: “Je, ndugu zangu Polisi mlishaifahamisha jamii kuwa ‘kuisaidia Polisi’ hakupo tena kwenye vituo vyenu?.” Dk Tizeba anasema kuna haja kubwa kwa Jeshi la Polisi kuhamasisha jamii ili iwe huru kutoa taarifa Polisi na kuondoa dhana ya kuwa ukitoa taarifa Polisi unajikuta ‘ukiisaidia Polisi’.
Mbunge wa Magu, Destery Kiswaga naye anashauri jamii ihamasishwe kuondokana na imani potofu na kuwa tayari kusaidia Polisi kwa kufichua ‘wakata mapanga’. Anashauri watoa taarifa nao wapatiwe ulinzi wa kutosha na kuwepo na utayari wa kisiasa kwa viongozi wa vyama vya siasa. “Wanasiasa tuache kuwakingia kifua wahalifu kwa kuogopa kunyimwa kura na wananchi,” anasisitiza.
Kupeleka watoto kwa wazee Mdau kutoka Karagwe mkoani Kagera, Livingstone Byekwaso, anasema wazee si wa kulaumiwa hata kidogo. “Tatizo liko kwa sisi wakazi wa mijini. Hatuwapeleki watoto wetu vijijini kwa mabibi na mababu zao. Sisi wenyewe tunawakwepa wazazi wetu hivyo kuwajengea dhana watoto wetu kuwa mabibi au mababu zao hawafai.
“Si hivyo tu, lazima tujue kadri binadamu anavyozeeka, akili yake inapungua, anapoteza kumbukumbu na kuanza kufanya mambo yasiyo ya kawaida. Lakini hiyo haina maana kwamba anakosa upendo kwa wajukuu wake,” anafafanua Byekwaso. Washiriki waazimia Katika mkutano huo washiriki waliazimia elimu ya kutosha kwa jamii kwa kuhusisha zaidi viongozi wa dini itolewe.
Iliaminika kwamba viongozi wa dini wana uwezo mkubwa wa kuwafanya watu waanze kuwa na hofu ya Mungu; hivyo kuachana na vitendo viovu kwa wazee. Maazimio mengine ni pamoja na kuanzisha miradi ya kupinga ukatili, kuomba Jeshi la Polisi lipatiwe rasilimali, uwezo, vitendea kazi na bajeti ya kutosha ili kuwezesha ufuatiliaji na upelelezi wa mauaji kwa haraka.
Kadhalika washiriki walitaka sheria inayohusu masuala ya wazee na kanuni zake ikamilike haraka na ianze kutumika na kwamba zawadi zitolewe kwa wananchi wanaokuwa tayari kutoa taarifa na ushahidi mahakamani. Washiriki pia walishauri wanasiasa waoneshe kwa vitendo utashi wa kuondoa tatizo la ukatili wa wazee katika jamii na ramli chonganishi zipigwe marufuku.
Meneja Miradi wa HelpAge, Joseph Mbasha anasema kuwa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 inaonesha kuna wazee milioni 2.5 nchini wenye miaka 60 na zaidi ambayo ni sawa na asilimia 5.6 ya idadi yote ya watu. Kati yao, milioni 1.3 ni wanawake na milioni 1.2 ni wanaume. Asilimia 80 ya kundi hilo wanaishi vijijini. Anasema kuwa hivi sasa kuna zaidi ya wazee milioni 900 duniani kote na kwamba ifikapo mwaka 2050 kutakuwa na asilimia 21.5 ya wazee, idadi ambayo itazidi watoto walio na miaka 14 kwa wakati huo.
Kutokana na ukweli huo na kwa kuzingatia usemi wa wanaharakati wa mapambano dhidi ya ukatili na mauaji ya wazee nchini “kama sio mzee leo, wewe ni mzee mtarajiwa wa kesho” basi kuna haja kubwa kuandaa misingi ya maisha bora ya kundi hili muhimu katika jamii hivi sasa.
No comments:
Post a Comment