Mamia ya watu jana walijitokeza katika mazishi ya Abel Machanga, aliyefariki katika Hospitali ya Colombia Asia, India alikokuwa akipatiwa matibabu na maiti yake kuzuiliwa kwa mwezi mmoja.
Abel (24), alifariki dunia Desemba 31, mwaka jana na maiti yake kuzuiliwa hadi familia yake ilipolipa deni la Sh35 milioni ilizokuwa ikidaiwa, fedha zilizopatikana kutokana na michango ya Watanzania mbalimbali.
Akizungumza katika mazishi hayo, kaka wa marehemu, Christopher Machanga aliwashukuru Watanzania waliowezesha kupatikana kwa fedha za kurudisha mwili wa mdogo wake ili uzikwe nchini.
Christopher ambaye ndiye aliyekuwa na marehemu huko India alisema hakutegemea kama fedha hizo zingepatikana. Alisema madaktari wa India walianza kumshauri mdogo wake azikwe nchini humo kwa hofu kuwa mwili wake ungeharibika.
“Nimegundua Watanzania wana upendo kupita kiasi, sikutarajia kama tungefanikiwa kurudi na mdogo wangu akazikwa nyumbani,” alisema Christopher ambaye wakati uongozi wa hospitali hiyo ulipokuwa ukidai fedha hizo, ulizuia hati yake ya kusafiria. “Nashukuru sana vyombo vya habari ikiwamo gazeti la Mwananchi, mmefanya kazi kubwa hatimaye leo tunamlaza Abel sehemu ambayo tunaweza kuja kumtembelea hata siku nyingine.”
Akitoa salamu za Serikali, Diwani wa Kata ya Ukonga, Juma Mwipopo alisema Watanzania wameonyesha upendo wa hali ya juu, jambo ambalo linapaswa kuendelezwa bila kujali itikadi za vyama au dini. “Tukio hili limetupa funzo kubwa, niwasihi Watanzania tuendelee kuwa na moyo wa upendo bila kujali itikadi, tuendeleze umoja na mshikamano wetu,” alisema Mwipopo.
Simanzi zilitawala muda wote wa ibada ya mazishi huku mazungumzo ya jinsi mwili huo ulivyozuiliwa katika hospitali hiyo yakitawala na wengi wakilaani kitendo hicho na kuonyesha kushangazwa kwao na ukimya wa Serikali.
No comments:
Post a Comment