Thursday, 4 February 2016

BARNABA ANAVYOISHI NA MSANII ALIYEDHANIWA KUFA

Mulla na Barnabas
MOJA ya kazi kubwa ya mwanamuziki, Elias Barnabas (Barnaba Boy) mwenye uwezo mkubwa wa kutumia ala za muziki ni kusaidia vijana wenye vipaji vya muziki ili viwe ajira zao za kudumu kama afanyavyo yeye.


Njia kubwa ya kuwafikia vijana wengi ni mpango wake wa kufungua darasa la muziki kupitia mtandaoni ambalo litakuwa na masomo ya mafunzo ya muziki kwa ngazi mbalimbali ambayo yatamwezesha mtu yeyote popote alipo aweze kujifunza muziki kadri awezavyo bila kusafiri kufuata masomo hayo mbali na sehemu alipo.
Wazo la kufanya hilo alikuwa nalo muda mrefu, lakini liliongezeka baada ya kugundua kwamba wapo vijana wengi wanatoroka wanakoishi kwenda mikoa mikubwa yenye studio na wasanii wengi wakiamini watapata wanachotafuta lakini hawapati.
Mfano mzuri ni kijana Isaya Mwogoti (Mulla), aliyetoroka kwao Wilaya ya Njombe kuja kutafuta maisha ya muziki jijini Dar es Salaam.
Akielezea historia ya kijana huyo, Barnabas anasema historia yake huwa inamtia hamasa na nguvu ya kusaidia vijana wengi zaidi kadri awezavyo.
“Mulla alitoroka Njombe akiwa na mwenzake, walikuja Dar kutafuta maisha, walikuja wakiwa na shilingi laki tatu, lengo lao kuu likiwa ni kumtafuta prodyuza ili warekodi wimbo wakiamini ungewatoa na kuwa na maisha bora, lakini tofauti na hivyo walipofika Ubungo walikutana na tapeli akawapeleka kwenye magofu akiwadanganya kuwa ndiyo studio.
“Alipowafikisha hapo aliwataka wamsubiri ili awaletee maji, baada ya kuwaletea akawataka wamsubiri tena ili akawaletee chakula, maana walionekana kuwa na njaa, wakamkabidhi zile laki tatu walizopanga kwa ajili ya kurekodia pamoja na mizigo yao ya nguo yule tapeli akapotea nayo hakurudi tena,’’ anaeleza Barnaba historia ya Mulla.
Barnaba anaeleza kwamba vijana hao waliendelea kujipa moyo, walisubiri hapo hadi giza likaingia ndipo wakaamini kuwa wametapeliwa, lakini wakiwa katika harakati za kutafuta sehemu ya kulala ili kesho yake wajue cha kufanya wakakutana na mama mkubwa wa Barnabas, alipogundua kuwa wana matatizo akaingiwa na huruma akawachukua hadi kwake.
Asubuhi alipowahoji wote walionyesha nia ya kufanya muziki, akaamua aendelee kuishi nao huku akitafuta namna ya kuwasaidia zaidi, lakini rafiki wa Mulla hakuwa na uvumilivu, akamshawishi Mulla ili watoroke hapo, lakini Mulla alikataa, huku akimweleza mwenzake huyo kwamba anaona hapo ndipo sehemu sahihi ya kuanzia maisha yao ya muziki, lakini mwenzake hakukubaliana naye, usiku ulipofika akatoroka na kumuacha Mulla.
Asubuhi Mulla akamweleza mama yake huyo anayeishi naye namna alivyoshawishiwa atoroke akakataa, aliendelea kuishi hapo na kufanya shughuli za ndani za hapo lakini baadaye mama huyo alipoona Mulla anapenda sana muziki akaamua kumkutanisha na  Barnaba.
“Mama alinieleza yote kuhusu Mulla, nikamchukua na kuishi naye nyumbani kwangu, lakini mwanzo nilimchukua kama mfanyakazi akawa anasafisha nyumba na kuosha magari yangu, nilichokula na familia yangu naye alikula, alivaa na kuishi vizuri bila manyanyaso,
“Kila nilipopata muda wa kuzungumza naye alisema anataka kuwa mwanamuziki wa kurap, lakini alikuwa mdogo wa miaka 15-16, nilimuonea huruma sana maana alikuwa mshamba mno, ndipo nikaanza kumchukua na kwenda naye kwenye shughuli zangu za muziki, akawa anafurahia sana kuwa karibu nami, baadaye nikakutana na msanii mwingine, Ice Boy, huyu ni mwenyeji, aliwahi kuwa na Young Killer, akaniomba nimsaidie ili afikie sehemu nzuri kimuziki, nami nikamwambia naye amsaidie Mulla kuchangamka asiwe kwenye mawazo na unyonge kila wakati,’’ anaeleza Barnaba.
Anasema aliishi na wasanii hao kwa miaka mitatu, baadaye siku moja Mulla alipokuwa maeneo ya Kinondoni kwa mshangao mkubwa na bila kutarajia alikutana na kaka yake waliyepotezana miaka mitatu, wote walijikuta wakishangaana kwa muda.
“Walipokutana kaka yake akaita ‘Isaya, si ulikufa wewe’, maana jina lake ni Isaya Mwogoti, akajibu ‘sikufa kaka’, wakakumbatiana, machozi yakawatoka maana kwao walijua amekufa, hivyo walishafanya msiba wake na kuanua matanga kwamba Isaya (Mulla) amekufa.
Baada ya hapo Mulla alimchukua kaka yake hadi kwa Barnabas wakazungumza kisha wakampigia simu mama yao wakamweleza kuhusu Isaya (Mulla) kuwa hai na anaishi kwa Barnaba, mama yao alipokea kwa mshtuko taarifa hizo, lakini baadaye akakubaliana na ukweli kwamba mwanawe hakufa, lakini alisikitika kwamba kwa mila zao wakishamaliza msiba hata mtu akionekana hai hawezi kurudi katika familia hiyo, hivyo wakawataka Barnaba na mama yake mkubwa kuwa wazazi wa Mulla.
“Hivyo ndivyo ilivyokuwa, tukakubali kuwa naye, nami kwa sasa ndiyo baba mlezi wa Isaya (Mulla) na mama yangu mkubwa ndiye mama yake mlezi na yule wa Njombe anabaki kuwa mama yake mzazi.
“Lakini ninachoshukuru kwa sasa mambo kidogo yanamuendea vizuri, kwani ameshaanza kumtumia mama yake mzazi fedha, ameanza kuona matunda ya mwanawe kupitia muziki anaofanya na wiki ijayo wimbo wake wa kwanza unaoitwa ‘Njiwa’ utaanza kusikika vituo mbalimbali vya redio ndani na nje ya nchi,’’ anamaliza kueleza Barnabas, ambaye kwa sasa ana jumla ya wasanii wanne, wa kike wawili, wa kiume wawili, prodyuza na mtaalamu wa mitambo.
Mulla anaishukuru familia ya Barnabas kwa namna walivyoweza kuishi naye na kukuza kipaji chake cha muziki, huku akiomba familia nyingine kutowatenga wala kuwanyima misaada watoto wenye vipaji pindi wanapohitaji msaada wao wa hali na mali.
“Mi nashukuru naona kama Mungu aliniongoza nikutane na familia ya Barnaba na kupitia familia hii ndiyo kipaji changu kitaonekana, nawashukuru sana kwa kuwa wiki ijayo wimbo wangu wa ‘Njiwa’ niliomshirikisha bosi wangu na baba yangu mlezi, Barnaba utaanza kusikika vituo mbalimbali vya redio,’’ anaeleza kwa furaha Mulla.
MTANZANIA.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!