Wednesday 3 February 2016

BAN KI MOON AIPATIA TANZANIA SH.BILIONI 220 KWA AJILI YA WAKIMBIZI


Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ametoa dola za Marekani milioni 100 (Sh. bilioni 220) kutoka katika mfuko mkuu wa kushughulikia dharura wa umoja huo (CERF), kwa ajili ya shughuli za misaada katika maeneo tisa yenye dharura duniani na yasiyo na fedha za kutosha. 
 
Katika msaada huo,  Tanzania imetengewa dola za Marekani milioni 11 (Sh. bilioni 24) kwa lengo la kushughulikia mahitaji ya wakimbizi kutoka Burundi.
 
Zaidi ya raia 126,000 wa Burundi wamekimbilia nchini tangu Aprili, mwaka huu, kutokana na machafuko ya kisiasa nchini kwao, huku wengine 64,000 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) wakiwa wako nchini. 
 
Tanzania kwa sasa ina zaidi ya wakimbizi 193,000, ikikadiriwa kuwa takribani wakimbizi 1,500 wanawasili nchini kila wiki na  huenda idadi hiyo ikafikia 230,000 hadi mwisho wa mwaka huu.
 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana na  Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini, Alvaro Rodriguez , msaada  huo utasaidia kwa kiwango kikubwa kutoa misaada ya kibinadamu kwa wakimbizi wa Burundi wanaoishi katika kambi za Nyarugusu, Nduta na Mtendeli katika mkoa wa Kigoma, pamoja na jamii za wenyeji ambazo zinahitaji kwa haraka huduma bora za maji safi, usafi,  afya, chakula na makazi.
 
 Pia alisema sehemu ya fedha hizo zitatumika kushughulikia mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu ambao umeathiri mikoa 19 nchini.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!