Watu 11 akiwamo mama, mwanawe na mjukuu wake wamekufa papohapo na wengine 34 kujeruhiwa katika ajali ya basi la kampuni ya Simba Mtoto lililogongana uso kwa uso na lori.
Familia iliyopatwa na janga hilo ni ya mwandishi wa habari mwandamizi wa Redio ya Mlimani, Hamis Dambaya aliyefiwa na mkewe, Raya Said, mtoto wake Nargis Hamis na mama mkwe wake ambaye jina lake halikutambuliwa mara moja.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Tanga, Mihayo Msikhela alisema ajali hiyo ilitokea jana saa 1.15 asubuhi kwenye Kijiji cha Pangamlima wilayani hapa wakati basi hilo likitokea Tanga kwenda Dar es Salaam na lori likielekea Tanga.
Kamanda Mihayo aliwataja baadhi ya watu waliokufa kuwa ni kondakta wa basi hilo, Fred Venance, Mwalimu Mbwana Saada Ali, Raya Said, Nargis Hamis na Mohamed Said anayesemekana kuwa dereva wa lori hilo.
“Majina ya watu wengine waliofariki kwa ajali hiyo na majeruhi bado tupo katika harakati za kuwatambua, lakini majeruhi wamepelekwa Hospitali ya Teule ya Muheza kwa matibabu,” alisema Mihayo na kuongeza kuwa miili ya marehemu hao imehifadhiwa hospitalini hapo.
Alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa lori hilo aina ya Scania kuingia upande tofauti, hivyo kugongana uso kwa uso na basi hilo.
Mkuu wa Mkoa Tanga, Mwantumu Mahiza alifika mapema kwenye eneo la ajali na kushirikiana na wananchi kunasua miili ya abiria waliokufa na majeruhi.
Kazi hiyo ya kunasua miili hiyo ilifanyika kwa muda wa saa sita, kabla ya kufika gari la kupandisha mizigo kwa ajili ya kunyanyua kichwa cha lori kilichokuwa kimeharibika vibaya kikiwa na abiria ndani.
Mashuhuda wa ajali hiyo walisema walisikia kishindo na walipofika eneo la tukio walikuta magari hayo yamegongana huku baadhi ya abiria wakipiga kelele kuomba msaada.
Hospitalini
Wananchi walikuwa wamefurika katika hospitali hiyo kwa ajili ya kutambua miili ya watu waliokufa huku Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Estelina Sekilasi akisaidiana na wahudumu kuwapeleka majeruhi wodini kwa ajili ya matibabu.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment