Friday 15 January 2016

WAWEKEZAJI NCHINI 49 "KUKIONA"


MASHAMBA na viwanda 49 vilivyomilikishwa kwa wawezekaji mbalimbali nchini, vimebainika wamiliki wake wamekiuka masharti ya umiliki na wengine wamebadilisha matumizi yake bila idhini ya Msajili wa Hazina.


Hayo yamo kwenye taarifa ya Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru aliyoitoa hivi karibuni, iliyoorodhesha mashamba, viwanda na taasisi nyingine 337 vilibinafsishwa. Awali, Msajili huyo alitoa siku 30 kuanzia Novemba 18, mwaka jana, kwa wawekezaji wote walionunua viwanda na mashamba yaliyokuwa miliki ya serikali, kuwasilisha taarifa za sasa za utekelezaji wa masharti ya mikataba yao, vinginevyo serikali itarejesha umiliki wake.
Akitoa mrejesho wa mwitikio wa wawekezaji hao, mara baada ya muda waliopewa kumalizika Desemba 17, mwaka jana, Mafuru alisema hadi kufika Desemba 30, mwaka jana, ofisi yake ilikuwa imeshapokea taarifa za wawekezaji 177 kati ya hao 337.
Mafuru alisema kati ya idadi hiyo, ofisi hiyo imepitia baadhi taarifa za mashamba, viwanda vivutio vya utalii na maliasili, usafiri na sekta nyinginezo na hadi sasa taarifa 49 za miliki kwenye maeneo hayo, zimebainika kukiuka kiwango kikubwa masharti ya mkataba wa umiliki.
Akifafanua, Mafuru alisema masharti yaliyokiukwa ni pamoja na kubadilisha matumizi ya awali ya mashamba au viwanda husika, kukiuka makubaliano ya mkataba wa biashara na kutolipa tozo na riba husika. Alitaja miliki hizo ni za mashamba 10, viwanda 30 vivutio vya utalii sita, kampuni ya usafiri moja na sekta nyingine mbili.
Kwa upande wa mashamba, Mafuru alitaja ni shamba la Ludodolelo na Lupembe Tea Factory ya Njombe, Newala 1 Cashewnut Processing Factory na Mtwara Cashewnut Processing Factory ya Mtwara.
Pia Nachingwea Cashewnut Processing Factory na Kibaha Cashewnut Processing Plant ya Pwani, Rongai Dairy Farm mkoani Arusha, Masasi Cashewnut Processing Factory ya Mbeya na Mlangali Tea Estate la Iringa.
Viwanda hivyo 30 ni Mbeya Textile Mill, Mbeya Ceramic Co., Tanzania Bag Corporation (Moshi) (Mill1&11), Tanganyika Packers Ltd (Shinyanga Meat Plant), Ubungo Gaments Ltd, National Steel Corporation, Kisarawe Brick Manufacturers Ltd, Polysacks Co, Ltd na Tanzania Shoes Co. Vingine ni Ilemela Fish Processing Plant, Nyanza Engineering Foundry Co Ltd, Mang’ula Mechanical and Machine Tools Ltd, Mwanza Tanneries Ltd, MOPROCO, Sikh Sawmills (T) Ltd, Mkata Saw Mills Ltd, Tembo Chipboards Co Ltd na Hotel 77 Ltd.
Pia kuna Embassy Hotel, Ubungo Spinning Mill, Keko Pharmaceutical Industries Ltd, Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd, EX-NMC Rice Mills, Arusha Regional Trading Co. Stationary and Office Supplies (S&0), Fibre boards Afrika Ltd, Auto Mech Ltd, Arusha Regional Trading Co, TTA Rungwe na Biashara Consumer Service Co. Aidha, Mafuru alitaja vivutio vya utalii na maliasili vilivyokiuka mkataba wa uwekezaji kwa kiwango kikubwa kuwa ni Hotel ya Savoy, Hoteli ya Kunduchi Beach, New Mwanza Hotel, New Safari Hotel, Iringa Wood Pole Treatment Plant na Tanzania Publishing House.
Kwenye sekta ya usafiri, iko Kampuni ya Kagera Regional Transport na sekta nyinginezo ziko kampuni mbili ambazo ni CDA Zuzu Factory na Pugu Kailine Mines. Mafuru alisema kazi ya kupitia taarifa za miliki ya wawekezaji hao, inaendelea na kwamba taarifa zao zitawekwa hadharani baada ya kukamilika kwa ukaguzi huo ili kubaini iwapo wametekeleza masharti ya mikataba yao au la.
Alisema kupitia tangazo hilo la Desemba 31, mwaka jana, Ofisi ya Msajili wa Hazina haitawakumbusha tena wawekezaji hao kuhusu kuwasilisha taarifa hizo na badala yake hatua nyingine za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!