Friday 29 January 2016

WATU 20 WAHOFIA KUFA MAJI KIVUKO CHA KILOMBERO.


Watu zaidi ya 20 wanaofiwa kufa maji baada ya Kivuko cha Mto Kilombero II kinachounganisha wilaya za Kilombero na Ulanga, mkoani Morogoro kuzama, huku walionusurika katika ajali hiyo wakieleza tukio hilo lilivyotokea.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paul, jana alithibitisha ajali hiyo iliyotokea juzi saa 1:30 usiku, wakati  kivuko hicho kikitokea Ulanga kuelekea  Ifakara kwa kupigwa dhoruba kali.
 
Alisema watu wengine wawili walikuwamo katika Kivuko hicho ambao walikuwa ndani ya magari yaliyokuwa katika kivuko hicho hawajaonekana hadi jana na kuwataja kuwa ni, Dustan Wasira, mfanyakazi wa benki ya CRDB na mwingine ambaye hajafahamika jina lake na kwamba juhudi za kuwatafuta zinaendelea pamoja na miili mengine ambayo inadhaniwa ipo ndani ya kivuko hicho kilichozama.
 
Wakizungumza na Nipashe eneo la tukio jana, baadhi ya watu walionusurika katika  ajali hiyo walidai kuwa ndani ya kivuko hicho kulikuwa na watu wanaokadiriwa kufikia 60 na kati yao 40 waliookolewa na wengine kujiokoa wenyewe, huku 20 hawajaonekana hadi jana.
 
Walisema upepo mkali ndio sababu iliyopelekea kivuko hicho kusombwa na hatimaye kuzama majini.
 
Mmoja wa walionusurika, Habiba Ngakongwa, alisema wakiwa katika kivuko hicho walipofika katikati ya mto upepo mkali ulitokea ghafla na chombo kuanza kupoteza mwelekeo lakini nahodha alijitahidi kukiongoza hadi kufika ukingo wa pili, lakini hali ilizidi kuwa mbaya kuzidiwa na kupelekea kupinduka na kuzama majini.
 
"Sikumbuki vizuri lakini nadhani ilikuwa majira ya saa 1:30 usiku tulikuwa tukitoka Ulanga mashambani na tulipofika katikati ya mto hali ilibadilika na upepo mkali ulianza sambamba na mvua, ndipo wahusika walipotupa maboya na tulivaa na baadae tulisombwa na kisha kuanguka nami nilijiokoa huku nikiwa na mtoto,” alisema Habiba.
 
Naye Said Kibaba alisema kama sio juhudi za nahodha wangekufa watu wengi, kwani alijitahidi kukiongoza kivuko na kuwapa moyo abiria. “Tulikaa katika maji kwa nusu saa hatimaye kivuko kilianza kuzama nasi kuokolewa,” alisema.
 
Mwingine, Said Omary, alisema walipanda kivuko hicho saa 1:30 usiku ikiwa ni safari ya mwisho, huku kikiwa kimebeba abiria wasiopungua 60, lori moja aina ya fuso lenye magunia ya mpunga na Landcruzer mbili ikiwemo ya benki ya CRDB.
 
Alisema wakati wanakaribia kufika kulitokea mvua kubwa ikiambatana na upepo mkali na gafla kivuko hicho kilisombwa na kugeuka na kuzama kwenye maji.
 
Alisema baadhi ya abiria waliruka majini, huku magari hayo matatu yakisombwa na maji na kupelekwa pasipojulikana.
 
Naye Saimon Mtokambali aliyeokolewa na wavuvi alisema kuwa, watu wasiopungua 15 waliokolewa na wavuvi hao na wengine watano waliogelea wenyewe hadi nchi kavu.
 
Kwa upande wake, Mkuu wa Kivuko hicho, Mhandisi Fadhil Haroub, alisema kilikuwa katika safari ya mwisho kutoka upande wa Ulanga kuelekea Ifakara na walipofika katikati ulitokea upepo mkali na walijitahidi kukiokoa lakini ikashindikana na hatimaye kugonga nguzo za daraja la muda kisha kusimama na kuzama.
 
Alisema ndani ya kivuko hicho kulikuwa na magari matatu likiwamo Fuso lililobeba mchele na Landcruiser mbili,  bajaj, bodaboda na baiskeli kadhaa na vyote vimezama na kutojua idadi ya watu waliofariki. 
 
Akizungumzia tukio hilo, Waziri  wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, aliyefika eneo la tukio, alisema vikosi vya uokoaji na vya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na wananchi vinaendelea na kazi ya uokoaji.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!