Baadhi ya wananchi waliobomolewa nyumba zao kwenye maeneo ya mabondeni jijini Dar es Salaam, wameonekana wakihamia kwa kasi katika viwanja vyao huko Mabwepande ambavyo awali walivitelekeza.
Jana Nipashe ilishuhudia wananchi wakifanya usafi kwenye viwanja Mabwepande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, maeneo ambayo awali waliyatelekeza wakidai kuwa hawana fedha za ujenzi.
Otmar Haule, ambaye ni mmoja wa waathirika aliyekutwa kwenye kiwanja chake eneo walilolipa jina la Mlimani City, alisema amelazimika kuhamia huko baada ya nyumba yake kuwekwa alama ya X maeneo ya bonde la Kinondoni Hananasif.
Alisema nyumba yake iliyowekwa X ndiyo iliyomwezesha kupata kiwanja hicho mwaka 2014 Mabwepande baada ya kuvunjwa vyumba viwili kati ya vinne alivyojenga.
“Kipindi kile baada ya kuishi kwenye mahema na kuwa miongoni mwa wale waliopewa viwanja, nilikuja hapa kujenga msingi na kurudi kwenye nyumba yangu iliyovunjwa nikaikarabati na kuendelea kuishi lakini safari hii watu wa serikali wanaonekana hawana mchezo,” alisema. “Nakaa hapahapa.”
Alipoulizwa kwa nini hakuhamia huko tangu alipopewa kiwanja na serikali, Haule alidai kuwa hawakupewa vifaa vya ujenzi vya kuanzia kama wenzao.
“Wenzetu wa Mji Mpya maarufu kama ‘kwa Ridhiwan’, kila mmoja alipatiwa mabati manne, mbao sita na mifuko 100 ya saruji hivyo iliwawezesha kujenga, lakini huku kwetu hatukupewa kitu, tumeshafuatilia hadi tumechoka,” alisema.
Alikiri kuwa kiwanja hicho kimekuwa mkombozi kwake kwa sababu vinginevyo angekosa pakuishi.
Mjumbe wa maeneo hayo, Rashid Nampanda alisema kati ya kaya 12 zilizopo eneo lake, tano zilibaki bondeni kutokana na changamoto ya fedha za kujengea nyumba.
Alisema hadi jana hakuna aliyerejea lakini eneo lililopakana naye watu wameanza kurejea kwenye maeneo yao tangu wiki iliyopita na akaomba serikali itekeleze ahadi ya kuwapatia vifaa vya ujenzi kama wenzao.
Pia aliitaka serikali iharakishe zoezi la utoaji hati ya umiliki ardhi kama walivyoagizwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete wakati wa utawala wake.
Alisema juzi wajumbe watano wa mitaa hiyo yenye changamoto, walikutana kujadili changamoto hizo ili waziwasilishe kwenye mamlaka husika ili serikali ya awamu ya tano iwasaidie.
Naye mjumbe wa Mji Mpya, Sadati Shemboko alisema katika eneo lake waliorudi wakitokea mabonde ya Jangwani na Hananasif wanakadiriwa kufikia 30 hivi sasa.
Bisikina Mitandi (66), mmoja wa wazee wanaoishi huko ambaye amefanikiwa kujenga nyumba licha ya changamoto za maisha, alisema sasa ni mwaka wa tatu hajui mafuriko.
“Hapa hunitoi mwanangu nina amani, nalala usingizi mpaka naota, kule bondeni ilikuwa hakuna kusinzia mvua moja unajikuta upo juu ya bati, hivi Mungu atupe nini, watu wamepewa viwanja wameviacha na kurudi kule,” alisema.
No comments:
Post a Comment