Saturday, 16 January 2016

UTAMBUE UGONJWA WA AKILI UNAOSABABISHA TABIA YA WIZI


Wizi ni kitendo cha mtu kujitwalia kitu kisichokuwa chake kwa njia ya kificho na kujimilikisha isivyo halali ili kukitumia au kukiuza kama ni chake. Ingawa mara nyingi tunashuhudia vitendo vya wizi katika jamii, lakini ni mara chache watu kuhusisha vitendo hivi na ugonjwa wa akili.

Watafiti na wachunguzi wa magonjwa ya akili wanabainisha kuwa baadhi ya vitendo vya wizi katika jamii, vinasababishwa na ugonjwa wa akili ujulikanao kwa lugha ya kitabibu kama Kleptomania.
Takwimu za afya ya jamii zinaonyesha kuwa, ugonjwa huu wa akili unaathiri asilimia 0.7 ya watu katika jamii. Hii ina maana kuwa katika nchi kama Tanzania ambayo kwa sasa ina watu wapatao milioni 47.4 kwa mujibu wa makadirio ya takwimu za Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), takribani watu 332,000 wana tatizo la ugonjwa wa akili unaosababisha tabia ya wizi. Baadhi ya takwimu zinabainisha kuwa miongoni mwa watu wanaokamatwa kutokana na wizi, wengi kufikia kiasi cha asilimia 24 wana tatizo la ugonjwa huu. Tatizo hili la afya ya akili husababisha wagonjwa wengi kupata kipigo kutoka kwa wananchi wenye hasira kali na kwa bahati mbaya wagonjwa wengine hupoteza maisha kutokana na kipigo.
Wengine wengi hushtakiwa na kufungwa magerezani badala ya kupelekwa hospitalini kwa ajili ya kupata matibabu. Katika utafiti mmoja uliochapishwa mwaka 2009 katika jarida la Psychiatric Quarterly toleo namba 80(4), ilibainika kuwa kati ya watu 101 waliogundulika kuwa na tatizo hilo, asilimia 68.3 walikamatwa na polisi na asilimia 20.8 walikamatwa, kushitakiwa na kufungwa gerezani.
Ugonjwa huo unaweza kuwa chanzo cha hali mbaya ya uchumi wa mgonjwa mwenyewe, familia yake, taasisi, jamii na taifa kwa ujumla kutokana na upotevu wa mali, na mzigo wa gharama kwa vyombo vya huduma za afya na sheria kushughulikia watu hawa na kuwatunza kabla na baada ya kuhukumiwa. Ugonjwa huu pia unaweza kusababisha kuvunjika kwa ndoa na migogoro ya kifamilia na kijamii.
Kwa kiasi kikubwa ugonjwa huu unaathiri zaidi wanawake kuliko wanaume kwa uwiano wa 3:1 na mara nyingi tatizo hili huwakumba vijana na watu wazima wenye umri chini ya miaka 35 ambao ni sehemu ya nguvu kazi ya taifa. Watu wazima wenye umri wa miaka 50 na kuendelea pia wanaweza kuathirika na tatizo hili la afya ya akili.
Kibaya zaidi kuhusiana na tatizo hilo la kiafya ni kwamba, wagonjwa wenye tatizo hili hawaendi hospitalini kupata tiba kutokana na ukweli kwamba wengi huona aibu au hawajitambui kuwa wanaumwa.
Hali hiyo kwa kawaida husababisha wizi usiokuwa na faida yoyote kwa mwizi mwenyewe. Tabia hii haitokani na hali ngumu ya maisha au upungufu wa kipato bali chanzo chake ni tatizo la akili kushindwa kujitawala dhidi ya tamaa kali ya vitu inayojirudiarudia. Wagonjwa wenye tatizo hilo wanaweza kuwa na kazi au biashara inayowaingizia kipato kizuri lakini bado wakawa na tatizo hili la wizi.
Wengi wanaiba hata vitu vidogovidogo kama kalamu za benki, pini za ofisini, chupi za wapenzi wao, bilauri (glass) kwenye sherehe, vijiko hotelini, vitu katika maduka kama supermarket au nguo zinazoanikwa majumbani na kwenda kuvificha au kuvirundika majumbani mwao bila kazi yoyote.
Wengine baada ya kuiba wanaweza kuteketeza, kuharibu, kugawa bure, kurudisha kwa siri au kutupa vitu walivyoiba.
Watu wenye tatizo hilo hupata furaha au hisia za kutua mzigo wa kisaikolojia unaowatesa moyoni baada ya kufanya wizi.
Wezi wa namna hii hawachagui kitu cha kuiba kwa sababu wanafanya hivyo si kwa kupata faida bali ni kutokana na hali ya ugonjwa.
Wengi wanapoulizwa kuhusu jinsi wanavyojisikia wakati wa kuiba, wanasema kuwa hupata hisia kama wanaota ndoto wanapotenda kitendo hicho. Jambo ambalo ni la kipekee kwa wagonjwa hawa ni kwamba katika tabia yao ya wizi hawashirikiani na wengine bali hufanya hivyo peke yao.
Chanzo cha tatizo
Ingawa chanzo halisi cha ugonjwa huu wa akili hakifahamiki vizuri, baadhi ya wanasayansi wanasema kuwa matatizo yanayoathiri sehemu ya mbele ya ubongo yanaweza kuwa chanzo.
Wachunguzi wengine wanabainisha kuwa tatizo hilo linaweza kusababishwa na majeraha ya kichwa yanayoambatana na kuumia kwa ubongo.
Utafiti uliofanywa na timu ya watafiti wa Chuo Kikuu cha Tel Aviv, Israel na kuchapishwa mwaka 2004 katika jarida la Clinical Neuropharmacology toleo namba 27(5), unaonyesha kuwa majeraha ya kichwa yanayosababisha ubongo kuathirika yanaweza kusababisha tatizo hilo. Wataalamu wengine wanadai kuwa chanzo cha tatizo hilo chaweza kuwa ni maumivu ya ubongo na maumivu ya kisaikolojia ambayo yanawapata watoto wadogo kutokana na manyanyaso au ukatili wa wazazi na walezi wakati wa utoto.
Mambo mengine ambayo yanahusishwa na chanzo cha tatizo hilo ni athari mbaya za matumizi makubwa ya dawa za kulevya, matumizi makubwa ya pombe, degedege na kifafa, hasa wakati wa utoto.
Watafiti wengine wanadai kuwa hali hii inaweza kutokea kama kutakuwa na upungufu wa kemikali ya serotonin inayozalishwa na ubongo ambayo kazi yake kubwa ni kurekebisha hali ya hisia na mihemuko.
Matokeo ya utafiti wa Jon E. Grant wa Chuo Kikuu cha Minnesota pamoja na wenzake yaliyochapishwa mwaka 2006 katika jarida la Psychiatry Research: Neuroimaging toleo la 147(2-3), nayo yanaonesha kuwa wizi unaotokana na ugonjwa wa akili unahusiana kwa karibu na kupungua kwa ukubwa wa nyama nyeupe ya ubongo (white matter) katika sehemu ya chini ya ubongo wa mbele.
Jinsi ya kuwasaidia wagonjwa
Jamii inapaswa kutambua kuwa si kila mwizi anafanya hivyo kwa makusudi, bali kuna ndugu zetu wanaoiba kutokana na matatizo ya afya ya akili. Kwa sababu hiyo basi ni vyema kujiepusha na mazoea ya kujichukulia sheria mkononi na kuwaua wezi kwa kisingizio cha hasira kali. Ni vyema kuwapa msaada na kuepuka tabia ya kuwadhalilisha watu wenye ugonjwa huo katika jamii.
Kwa wazazi na walezi, ni jambo la busara kujiepusha na manyanyaso ya watoto wenye tabia ya udokozi inayojirudiarudia kwani unaweza kukuta kwamba watoto hawa wanakabiliwa na tatizo hilo. Kwa madaktari na wahudumu wa afya ni muhimu kuuliza wagonjwa wenye tabia ya udokozi kuhusu hisia zao wakati wa kuiba ili kubaini tatizo hili mapema na kutoa msaada wa kitabibu kabla hali haijaleta madhara zaidi.
Watu wenye tatizo hilo pia wanashauriwa kuwaona wataalamu wa magonjwa ya akili mapema ili kupata msaada wa kitabibu kabla hali haijawa mbaya zaidi.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!