Juhudi za Rais John Magufuli kuimarisha ukusanyaji wa mapato nchini zimeonekana. Chungu kikubwa cha ukusanyaji wa mapato, Bandari, kimeanza kudhibitiwa ikiwa ni pamoja na kupekua kila mahali ambako ufisadi ulifanyika, na matunda yake yameonekana ndani ya kipindi kifupi alichokaa madarakani.
Wakwepa kodi wamebanwa na kulipa fedha walizotakiwa kutoa na tumeshuhudia watendaji wa Serikali waliohusika na ukwepaji huo wakifikishwa kwenye mikono ya sheria.
Miundombinu, hasa ya reli, ni chanzo kingine kikuu cha mapato katika sekta ya usafirishaji wa mizigo.
Siyo siri, kwamba Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) wakati huo likiitwa Shirika la Reli Tanzania (TRC) lilikufa kutokana na ufisadi na uzembe wa watendaji, ambao inaonekana dhahiri walikula njama za makusudi na wafanyabiashara wanaohusika na usafirishaji kupitia malori na mabasi. Lengo lao ni wafanyabiashara hao washike hatamu.
TRC maarufu kama reli ya kati pamoja na matawi yake ya Tanga-Arusha, Mwanza na Mpanda, imezorota tangu ilipobinafsishwa mwaka 2007. Hivi sasa njia za Tanga-Arusha na hata Mpanda zimekufa huku miti mikubwa ikiwa imeota katikati ya reli.
Usafirishaji katika Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) nao unasuasua huku ikikumbwa na migomo ya wafanyakazi kila uchao kutokana na malimbikizo ya mishahara.
Licha ya miundombinu ya barabara kuboreshwa na malori makubwa yako kwa wingi na kwenda kwa kasi zaidi tofauti na zamani, usafiri wa reli bado unapaswa kuwapo kwa sababu unaweza kuingiza mapato makubwa Serikali.
Mizigo mingi inayosafirishwa na malori, iwe ndani ama nje ya nchi, inaweza kusafirishwa kwa treni na kuondoa msongamano wa malori pamoja na makontena bandarini kama ilivyo sasa. Hii ni kwa sababu, treni moja linaweza kubeba hata makontena 50 yenye urefu wa futi 40 kwa mara moja.
Wakati wa kampeni za kuomba ridhaa ya Watanzania, Dk Magufuli aliahidi kusimamia ujenzi wa mtandao wa reli kama alivyofanya kwenye barabara wakati akiwa waziri.
Licha ya hivi karibuni kuwatimua kazi watendaji wa reli – Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (Rahco), Mhandisi Bernhard Tito na kuzivunja Bodi za Rahco na TRL, kutokana na tuhuma za ukiukwaji wa taratibu za ununuzi katika mchakato wa utoaji wa zabuni ya ujenzi wa Reli ya Kati, bado msimamo wa Serikali wa kuijenga reli hiyo na mitandao yake kwa kiwango cha kisasa uko pale pale.
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, jumla ya kilometa 5,000 za reli zitajengwa katika miradi kadhaa ambayo tayari imekwishapitishwa ili kuwezesha treni za abiria za mwendokasi, unaokadiriwa kufikia kilometa 120 kwa saa, kupita kwa urahisi huku zile za mizigo zikienda kwa mwendo wa wastani, kilometa 80 kwa saa.
Kabla ya kutimuliwa kwake, Mkurugenzi Mtendaji wa Rahco, Mhandisi Tito, alisema Reli ya Kati, kama zitakavyokuwa nyingine, itajengwa kwa kiwango cha standard gauge badala ya meter gauge za sasa.
Reli mpya ya Kati itakuwa na urefu wa kilometa 2,561, ikihusisha njia kutoka Dar es Salaam-Kigoma, Tabora-Mwanza, Kaliua-Mpanda, Kalema-Uvinza/Gitega-Msongati nchini Burundi na Isaka-Rusumo hadi Kigali, Rwanda.
Ujenzi wa reli hiyo utafanywa na China kupitia kampuni ya China Railway Construction Corporation Limited (CRCC).
Umuhimu wa reli hiyo, mbali ya kusafirisha abiria kwa uhakika na haraka, pia utasaidia usafirishaji wa mizigo katika maeneo ya kati na Nchi za Maziwa Makuu, hususan Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
“Tumekwishafanya upembuzi mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa reli mpya ya kati kwa kiwango cha standard gauge na upembuzi umekamilika kwa Dar-Tabora, Isaka-Kigali, Rwanda, na Keza-Msongati, Burundi. Upembuzi huu umefanywa na kampuni ya Canarail ya Canada,” alisema Tito.
Tito alisema, upembuzi wa njia ya Isaka-Mwanza umefanywa na kampuni ya Cowi ya Denmark ambayo pia imefanya kwa reli ya Tabora-Kigoma na Kaliua-Mpanda.
Kampuni ya Cowi pia inafanya ubunifu wa msingi wa reli mpya kutoka Mpanda hadi Karema Port kwenye Ziwa Tanganyika, wakati ubunifu wa ujenzi wa reli kutoka Uvinza-Msongati nchini Burundi umefanywa na kampuni ya HP Gauff ya Ujerumani.
Kwa upande mwingine, Reli ya Kaskazini, zamani ikijulikana kama Reli ya Usambara, ndiyo ya kwanza kabisa kujengwa Tanganyika, chini ya ukoloni wa Mjerumani. Ilianza mwaka 1891 hadi 1913 kabla ya kusimama kutokana na kuzuka kwa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, lakini baadaye ikamaliziwa na Waingereza mwaka 1929 hadi Arusha.
Reli hiyo mfu tangu 2007, sasa itajengwa tena kutoka Tanga hadi Arusha, kilomita 438, na baadaye Arusha hadi Musoma kilomita 670 na hivyo kuunganisha kanda ya Kaskazini na ile ya Ziwa Victoria.
Vilevile, kipande cha reli kutoka Ruvu hadi Tanga, kilomita 569, nacho kitatengenezwa. Kukamilika kwa Reli ya Kaskazini kutasaidia kukuza utalii katika eneo hilo maarufu hasa kwa Hifadhi za Taifa nyingi kama Mkomazi, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Tarangire, Ngorongoro na Serengeti.
“Lakini pia itakuza uchumi kutokana na kuwepo kwa machimbo ya magadi katika eneo la Engaruka pamoja na fosfeti kule Minjingu,” anasema Mhandisi Tito.
Ujenzi wa Reli ya Kusini kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay katika Ziwa Nyasa umbali wa kilomita 860, pamoja na tawi lake la kilomita 200 kwenda kwenye mgodi wa makaa ya mawe huko Mchuchuma na mgodi wa chuma huko Liganga ndio unaosubiriwa na wananchi wengi wa Kusini mwa Tanzania.
Mradi huo ambao uko katika hatua ya ubunifu wa ujenzi chini ya mshauri mwelekezi wa kampuni ya Dong Myeong Engineering Consultant ya Korea Kusini unatarajiwa kugharimu Dola 3.6 bilioni za Marekani, karibu sawa na Sh7.2 trilioni, na itajengwa na kampuni ya China Railway No. 2 Engineering Group (CREGC) ambayo ni kampuni tanzu ya China Railway Group Limited.
Umuhimu wa reli hiyo ni mkubwa kwani maeneo ya kusini mbali ya kuwa na utajiri wa mafuta na gesi, lakini pia kuna hazina kubwa ya madini iliyoko Mchuchuma na Liganga wilayani Ludewa. Mgodi wa makaa ya mawe wa Mchuchuma unakadiliwa kuwa na hazina ya tani 540 milioni wakati hazina ya chuma cha pua iliyopo Liganga inakadiliwa kuwa tani milioni 45.
Taarifa za Serikali Kuu zinasema ujenzi wa reli ya Mtwara-Mbamba Bay-Mchuchuma utafungua fursa za kimaendeleo katika Korido ya Maendeleo Mtwara (MDC) inayohusisha mikoa nane; yenye idadi ya watu 9,432,285, ambayo ni sawa na asilimia 22 ya Watanzania wote.
Reli hii pia itakuza mtandao wa biashara kati ya Tanzania na nchi za Malawi, Msumbiji na Zambia kwa kupunguza gharama za usafirishaji na kuboresha uchumi kwa bidhaa za ndani na nje.
Malawi kwa kiasi kikubwa inategemea njia mbili za reli zinazoiunganisha na bandari katika Bahari ya Hindi; reli ya Trans-Zambezia yenye urefu wa kilomita 269, ikitokea kwenye ukingo wa kusini wa Mto Zambezi hadi kwenye reli kuu ya kutoka Beira kwenda Zambia na reli ya kwenda bandari ya Nacala nchini Msumbiji.
Hivyo, endapo reli ya Mtwara-Mbamba Bay itajengwa inaweza kuisaidia Malawi na kuifanya itegemee Tanzania kupitishia bidhaa zake. Rasilimali za madini Kusini mwa Tanzania, hususan katika Korido ya Maendeleo ya Mtwara, ni nyingi kwa sasa na kwa mujibu wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), kampuni nyingi za kigeni zimeingia mikataba mbalimbali ya uchimbaji na utafiti.
Katika Pori la Akiba la Selous ambalo ni Urithi wa Dunia, tayari uchimbaji wa urani kwenye Mto Mkuju wilayani Namtumbo umekwishaanza tangu mwaka 2013 chini ya kampuni ya Uranium One inayomilikiwa na kampuni ya Atomredmetzoloto (ARMZ) iliyo chini ya Rosatom State Atomic Energy Corporation inayomilikiwa na serikali ya Urusi.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Uranium One iliyofanya utafiti katika eneo hilo, Chris Sattler, alikaririwa Juni 21, 2011 akisema kiwango cha uzalishaji wa urani kinaweza kuwa kati ya tani 1,900 na 2,700 kwa mwaka, lakini kwa wastani unaweza kuzalisha tani 1,600 za urani ya manjano kwa gharama ya Sh34,545 kwa paundi moja, hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi ya tatu kwa uzalishaji wa urani barani Afrika.
Wakati akizindua ofisi mpya za Tume ya Nguvu za Atomiki (TAEC) jijini Arusha, Mei 7, 2010, Rais mstaafu Jakaya Kikwete alisema Tanzania ilikuwa inaingia katika orodha ya nchi zinazozalisha kwa wingi urani duniani.
“Kama akiba yote tuliyonayo itatumiwa vizuri, Tanzania itakuwa nchi ya saba duniani kwa uzalishaji wa urani,” alisema Kikwete. Kwa ujumla, Tanzania ina akiba ya tani 20,769 za urani ghafi.
Kwa mujibu wa takwimu kutoka NDC, kuna maeneo yenye makaa ya mawe Mbamba Bay kwenye ukingo wa Ziwa Nyasa ambayo yana hazina ya tani 29 milioni ingawa iliyothibitishwa ni tani 2.4 milioni ambazo zinaweza kuchimbwa na wachimbaji wadogo na kuzalisha tani 75,000 kwa mwaka, hivyo kuzalisha Sh4.2 bilioni kila mwaka.
Takwimu hizo zinathibitisha kuwepo kwa makaa ya mawe Namwele-Nkomolo wilayani Sumbawanga, mkoani Rukwa wenye tani 1.5 milioni zilizothibitishwa na hazina ya tani 17.2 milioni ambazo zinaweza kuzalisha Shs. 19.8 bilioni kwa mwaka. Utafiti huo ulifanywa na kampuni ya Edenville Energy ambayo pia ndiyo iliyofanya utafiti katika maeneo ya Muze.
“Mradi wa makaa ya mawe wa Muze ambao unaweza kuzalisha umeme kwenye ukingo wa Ziwa Rukwa una akiba ya tani 3.41 milioni na hazina ya tani 56.59 milioni ambazo zinaweza kuzalisha 300MW za umeme. Pato la mwaka linakadiriwa kufikia Shs. 188.4 bilioni,” takwimu hizo zinaonyesha.
Watafiti wanasema kwamba, endapo Serikali itajenga kilometa hizo za reli na kuboresha huduma katika Reli ya Uhuru (Reli ya Tazara) yenye urefu wa kilomita 1,860 kutoka Dar es Salaam hadi New Kapri Mposhi kule Zambia, pato la taifa linaweza kuongezeka kwa usafirishaji wa abiria na mizigo.
Kinachohitajika ni mipango hiyo kukamilika na Serikali kuimarisha mapato yatokanayo na madini huku wananchi wakifaidika pia na kuimarika kwa miundombinu na biashara.
No comments:
Post a Comment