Saturday 2 January 2016

SAIKOLOJIA : Kukosa amani ya akili huweza kufanya maisha yasiwe ya furaha






Nilipowaza kuandika makala hii nilikuwa na wasiwasi kama wasomaji wangu wataelewa maana ya amani ya akili ni kitu gani hasa, kwa kuwa wamezoea kulitumia neno amani kuhusu jamii au taifa. Tumezoea kusikia watu wakisema nchi yetu ni ya amani.


Hata hivyo, nilipojaribu kuwauliza baadhi ya watu kuwa wanajua nini kuhusu amani ya akili walinirejesha kwenye neno amani. Walisema neno amani lina maana ya utulivu, salama au shwari. Waliongezea maelezo kwa kusema amani ni hali tuli, isiyo na fujo, ghasia, bughudha wala vurumai.
Kwa tafsiri hiyo nikaafikiana nao kuwa amani ya akili ni hali inayotokea wakati akili inapokuwa tulivu, iliyo salama, shwari na isiyo na wasiwasi au shaka yoyote. Mtu mwenye akili yenye amani anaonekana mwenye furaha, hana wasiwasi na anayefurahia maisha kikamilifu.
Je, hali ya kukosa amani ya akili inakubalika? Kuna kisa cha mtoto mmoja ambayo mara alipopata akili akaanza kuona kila kitu na hata akapelekwa shule mara alipata maradhi mabaya ya macho hadi akapoteza uwezo wa kuona. Aliendelea kuishi hivyo huku akivuta fikara ili akumbuke jinsi ulimwengu unavyoonekana na binadamu wenzake wanavyoonekana. Kadri muda ulivyoendelea kupita ndivyo alivyounda mawazo ya ajabu kuhusu jinsi watu wanavyoonekana. Kwa mfano alifikiri kuwa watu wote wanaonekana warefu na wembamba isipokuwa wachache ni wanene na wafupi na wana umbo kama la chupa. Wazo moja zuri kuhusu binadamu alilokuwanalo ni kuwa watu wote wanaonekana wenye nyuso za tabasamu na furaha wakati wote.
Baada ya miaka mingi siku moja yule mtoto wakati huo akiwa mvulana mkubwa wa miaka ishirini na tano alibahatika akapona na kuanza kuona tena. Jambo lililomstajabisha zaidi kuliko yote ni jinsi watu walivyoonekana wenye nyuso zenye uchovu, fadhaa, mawazo na mashaka. Wachache tu ndiyo walioonekana wenye tabasamu iliyoashiria kuwa wana akili zenye amani.
Kutokana na hali hii iliyomshangaza, akanikumbusha kuhusu rafiki yangu mmoja ambaye kila anayemtazama humuona kama mtu asiye na furaha na anayefikiri sana hadi tukamwita Bwana Mawazo.
Kila wakati ninapokutana naye nikamsalimu na kumuuliza kuhusu maendeleo yake hunijibu kwa kusema “Bwana maisha ya siku hizi ni magumu mno wala hatuna hakika kama tunaishi au hapana. Maisha yametufikisha mahali ambapo hata tunapofanya juhudi hatuna hakika tunafanya nini na tuna malengo gani na maisha yetu.”
Kwa hali yoyote ile iwayo maneno ya huyu rafiki yangu yanaashiria jinsi hali ya maisha ya binadamu wa leo yalivyo. Ni safari ndefu ya mapambano ya kutafuta na kukidhi matarajio ya maisha. Banadamu ana shauku ya leo kuwa hivi kesho kuwa vile. Leo kuwa na hiki na kesho kuwa na kile. Wanaume wa wanawake wanafanya kazi, wanapambana, wanahangaika na daima wanatamani kuwa na hadhi na fahari katika maisha na vitu vya hali ya juu. Wanatafuta mali, hadhi, uwezo, kutambulika, marafiki na washirika. Lakini ni wangapi wanafanikiwa? Je wanajua kuwa bila kuwa na amani ya akili hawataweza kufanikiwa katika maisha!
Hatuna budi kukumbuka kuwa licha ya mihangaiko yetu ya kutaka mafanikio, ulimwengu wa sasa wenyewe tu una misukosuko kuliko wakati mwingine wowote.
Kuna bibi mmoja niliyewahi kufanyanaye kazi ambaye aliamua kuhamia Marekani ambako hivi sasa amekaa miaka migi. Kila ninapomuuliza kuhusu miji miwili ya New York na Washington amewahi kunipa jibu lililonistajabisha sana. Anasema ingawa ameishi huko Marekani miaka mingi, lakini huwa hapendi kwenda kwenye miji hiyo miwili kwa sababu inatisha kwa wingi wa majengo marefu, wingi wa magari, wingi wa watu na pilikapilika na harakati za watu zilizopindukia. Anaongeza kuwa inapobidi aingie katika moja ya miji hiyo huingia na kutoka haraka. Hata hivyo, tangu anapoingia huingiwa na woga na wasiwasi ambao hubaki nao hadi anapotoka.
Hivi ndivyo hali ilivyo, ni ulimwengu wenye misukosuko inayotokana na harakati zinazokwenda kama saa. Katika hali hii, tunapojiongezea na wasiwasi tunaojiundia sisi wenyewe kutokana na shauku zetu ndiyo maana tunajifanya tushambuliwe na magonjwa kama vile maradhi ya moyo, shinikizo la damu, msongo wa mawazo, kiarusi na maradhi kadha wa kadha yanayohusiana na mfumo wa neva. Maradhi haya kwa kawaida hutokana na misisimko ya shughuli nyingi tunazofanya kwa mihemko na mifadhaiko na wala hayatokani na sababu za kimwili.
Kocha mmoja maarufu wa wanaspoti amesema “Watu hawafi kwa maradhi bali kutokana na muwako wa ndani ya miili yao” kukosa amani ya akili pia huathiri msimamo ulio sawasawa wa mtu na kumfanya ajichanganye yeye mwenyewe na hata kuathiri uhusiano wake na watu wengine. Aidha hali hii huweza kuathiri uwezo wa mtu wa kufanya maamuzi. Matokeo mabaya zaidi ni pale ambapo hali ya kukosa amani ya akili inavyoathiri uwezo wa mtu wa kujitambua yeye mwenyewe na maana ya maisha yake.
Tunawazaje kuiepuka hali ya kukosa amani ya akili?
Ili kuepuka kasoro kubwa ya maisha ya binadamu ya kukosa amani ya akili inabidi tuache kuendelea na imani kuwa katika maisha ni lazima tutekeleze yale yote tunayowazia kwa dhahania. Nayaita ya dhahania kwa sababu mara nyingi huwa ni kama ndoto. Hizi ni kama vile ndoto ya kuwa na mali nyingi, ndoto ya cheo kikubwa, ndoto ya kuwa na gari la fahari, ndoto ya kuwa na jumba la fahari, ndoto ya kutembelea nchi maarufu duniani na nyingine nyingi. Ndoto hizi hutufanya tufikirie kufanya mambo mengi na kuyafanya maisha yetu yawe na shughuli nyingi. Kila mara huwa tunaamini tutamaliza orodha ya mambo yote tunayofikiria kuyatekeleza na kuwa huru.
Kila tunapojiona tumekabiliwa na mambo mengi huwa tunajiaminisha kuwa hali hiyo ni ya muda tu na kwamba baada ya muda fulani haitatukabili tena. Huwa tunajifariji kwa kusema kama vile “Nikipata kazi nzuri wahangaiko yatakwisha, nikioa yatakwisha, nikijenga nyumba yatakwisha, nikinunua gari yatakwisha, watoto wangu wakikua yatakwisha.
Hali hii huendelea vivyo hivyo na kila wakati huwa tunagundua kuwa kuna jambo jingine la kukamilisha.



Pamoja na shauku zako zote, bila kujali wewe ni nani na uko wapi na nini unachofanya, kumbuka kuwa furaha yako na amani ya ndani ya nafsi yako ni muhimu kuliko kitu chochote kingine katika maisha yako. Ikiwa utajitamanisha kupata kila kitu unachokitarajia na kujituma kufanya kila harakati ili ukipate ni lazima hali ya afya yako itakuwa katika mgogoro. Hautakuwa na hali ya kujisikia mzima kikamilifu. Ni mambo machache tu muhimu ambayo tunapaswa tuyachukulie kama ni ya dharura. Tunachohitaji ni kujipanga vizuri katika namna ya kutekeleza mambo yetu bila kuwa na mihemko na kutekeleza mambo kwa kujikalifu.

By Abeid Sakara


No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!