Tuesday, 19 January 2016

SABABU ZA KIFO CHA BOSI TAA ZAJULIKANA


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mhandisi Suleiman Said, amefariki dunia akiwa katika mazoezi ya kuogelea jijini Dar es Salaam.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Lucas Mkondya, akizungumza na Nipashe alisema tukio hilo lilitokea jana saa 12:00 asubuhi wakati akiogelea katika ufukwe wa Bahari ya Hindi eneo la Feri.
Akielezea tukio lilivyotokea, alisema Suleiman alikwenda katika klabu ya bwawa la kuogelea la Tanganyika Swimming Club lililopo eneo la Feri jijini Dar es Salam.
Mkondya alisema baada ya kufika katika klabu hiyo, alianza kufanya mazoezi ya kurukaruka na kamba na baadaye alijitosa baharini na kuanza kuogelea akiwa na mwenzake, Godwin Vartalala.
Aliongeza kuwa wakati akiendelea kuogelea huku wakiwa waemekwenda umbali wa kina kirefu, ghafla Suleiman alimueleza mwenzake kuwa ameishiwa nguvu na kumuomba amsaidie kumtoa nchi kavu.
Kamanda Mkondya alisema Vartalala baada ya kuombwa msaada huo naye aliwasiliana na boti ndogo ili iwasaidie ambayo ilifika baadaye na kumchukua Suleiman kumpeleka nchi kavu.
Alisema baada ya hapo, ndugu wa Suleiman akiwamo kaka yake, Faiza Mohamed Suleiman, walijulishwa hali ya ndugu yao na baadaye alikimbizwa katika Hospitali ya Aga Khan kwa matibabu.
Alisema daktari wa hospitali hiyo walipompima walibaini kuwa Suleiman alikuwa tayari ameshafariki dunia ingawa hawakueleza sababu zilizosababisha kifo chake.
Mkondya alisema uchunguzi wa polisi umebaini kuwa marehemu kabla ya kufikwa na mauti, alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa shinikizo la damu na huenda ndiyo sababu ya kuishiwa nguvu wakati akiwa majini akiogelea.
MLINZI WAKE ASIMLIA ALIVYOAGWA
Mlinzi wa nyumba ya Suleiman, Hellena Thomas, akizungumza na Nipashe nyumbani kwa marehemu eneo la Upanga jijini Dar es Salaam, alisema bosi wake amekuwa na kawaida ya kwenda kuogelea kila siku saa 11:30 alfajiri na kurejea saa 1: 00 asubuhi kujiandaa kwenda kazini.
“Leo (jana), aliniaga kama kawaida yake kwamba anakwenda kuogelea Tanganyika Swimming Club, mara nyingi huwa anaondoka pekee yake,” alisema.
Hellena alisema akiwa nyumbani, alipewa taarifa kuwa bosi wake Suleiman amefariki dunia wakati akiogelea na kwamba mwili umehifadhiwa katika Hospitali ya Aga Khan.
Alisema baada ya taarifa hizo, mke wake na marehemu alijulishwa na mtoto anayesoma Shule ya Msingi ya Aga Khan na baadaye watoto wake wawili waliopo nchini Uingereza kwa masomo nao walijulishwa taarifa za msiba.
SIMANZI TAA
Kufuatia taarifa za kifo cha Mkurugenzi huyo, simanzi na majonzi vilitawala kwa wafanyakazi wa TAA ambao hawakuamini kilichotokea.
Baadhi ya wafanyakazi wakizungumza na gazeti hili walisema hawaamini kama kweli Mkurugenzi wao amefariki dunia huku wakimwelezea kuwa wamempoteza kiongozi mzuri ambaye alikuwa mtetezi wao hususan katika suala la maslahi na ajira.
“Kifo cha Mkurugenzi wetu kimetusikitisha sana. Sijui kama tutapata kiongozi kama yule ambaye alikuwa akitupigania katika suala la maslahi na ajira ambalo limekuwa tatizo kazini kwetu. Ni pigo kweli,” alisema mfanyakazi mmoja aliyeomba jina lake lisiandikwe gazetini.
Suleiman ambaye ameacha mjane na watoto watatu, alizikwa jana katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!