Thursday, 14 January 2016

POLISI DAR WASAKA MAJAMBAZI BENKI


JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limesema kuwa wapo baadhi ya wafanyakazi wa benki, ambao kwa namna moja au nyingine, wanashirikiana na majambazi kufanya uhalifu; na sasa linawasiliana na wamiliki wa taasisi za kifedha, kujiridhisha uhusika wao na uhalifu wa kutumia silaha.


Aidha, limesema mtu yeyote atakayetaka kusindikizwa na polisi kwenda kuchukua fedha nyingi benki, anaruhusiwa kwa kulipia Sh 10,000 au Sh 20,000.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda hiyo, Simon Sirro alisema wameanza kuweka ulinzi mkali katika benki mbalimbali, ikiwemo zilizopo eneo la Mlimani City na kwamba wanakagua pikipiki na watu wanaowatilia shaka.
Kamanda Sirro alisema wapo baadhi ya wafanyakazi wa benki, ambao kwa namna moja ama nyingine wanashirikiana na majambazi kufanya uhalifu, na kutokana na hilo, watawahoji wafanyakazi wa taasisi hizo za fedha ili kubaini ni nani wanaohusika katika njama hizo.
Alisema hiyo ni oparesheni maalumu iliyoanza rasmi na kwamba, uhalifu wa kutumia silaha unaoendelea katika maeneo mbalimbali ya jiji, unahatarisha maisha ya wakazi hao na unapaswa kudhibitiwa haraka. Alisema wananchi wanapaswa kutumia njia mbadala ya kuchukua fedha benki ili kuepuka uhalifu huo.
Alisisitiza kuwa unyang’anyi huo, hufanyika kwa kutumia pikipiki maarufu kama bodaboda na kwamba wameanza oparesheni ya kuwakamata wenye bodaboda hizo na kuwahoji.
“Tumeanzisha oparesheni maalumu dhidi ya pikipiki ambao wanavunja sheria barabarani na wanaojihusisha na masuala ya uhalifu jijini,’’ alisema Kamanda Sirro ambaye ameshika wadhifa huo kuanzia Januari mosi mwaka huu.
Hatua hiyo imekuja baada ya kuripotiwa kutokea kwa matukio kadhaa ya uhalifu, ambapo baadhi ya wananchi ambao ni wateja wa benki wameporwa fedha zao mara tu baada ya kutoka kuchukua katika benki. Baadhi ya benki zinazohusishwa na zile zilizopo katika eneo la Mlimani City katika Manispaa ya Kinondoni.
Kuhusu ukamataji wa pikipiki hizo, wamekamata pikipiki 150 kwa Mkoa wa Kipolisi Temeke, 241 Kinondoni na Ilala 249 ambazo baadhi yao zimelipiwa faini na nyingine zinachunguzwa kuona uhalali wa wamiliki wake.
Aliongeza kuwa jeshi hilo limemkamata Mganga wa Kienyeji, Simba Said (44) mkazi wa Vingunguti Koloni, ambaye ilidaiwa walipanga njama kufanya ujambazi maeneo ya Buguruni.
Alisema katika msako huo, jambazi mmoja alipigwa risasi na kukimbizwa katika Hospitali ya Amana ambako baadaye alifariki dunia na wengine walitoroka kwa kutumia pikipiki tatu.
‘’Wakati ufuatiliaji ukiendelea zilipatikana taarifa kuwa majambazi hao walikimbilia maeneo ya Tabata na kwamba Polisi walifanikiwa kukamata bunduki mbili na watuhumiwa wanane,’’ alisema Kamanda Sirro.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Ibrahim Mussa (40), dereva Mohamed Shaibu (20), mfanyabiashara Khamis Jaffari (44) na Abdulaziz Kikwanda (44) mkazi wa Buguruni. Wengine ni Juma Bakari (40), mkazi wa Majohe, Fitina Ramadhan (43), Dunia Rashid (50) na Khamis Omary (36) kinyozi mkazi wa Buguruni.
Aidha, Januari 7, mwaka huu maeneo ya Gongo la Mboto, alikamatwa Mkama Hassan (32), mkazi wa Mbagala Maji Matitu ambaye alikutwa na bastola aina ya Chinese iliyofutwa namba ikiwa na risasi saba. Alitoa mwito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa ili Jiji la Dar es Salaam liwe shwari.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!