Wednesday, 13 January 2016

NYUMBA ZA FAMILIA 40 MBALALI ZAZOLEWA NA MTO CHIMALA

Zaidi ya familia 40 katika kijiji cha Chimala kata ya Chimala Halmashauli ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, hazina mahali pa kuishi baada ya nyumba zao kubomolewa na mto Chimala uliokuwa umefurika kutokana na mvua kubwa iliyonyesha juzi.
 
Wakizungumza na waandishi wa habari kijiji hapo jana, wananchi hao walisema maji ya mto huo mbali ya kubomoa nyumba zao, pia yamesomba vyakula, nguo na vyombo mbalimbali pamoja na kubomoa mfereji unaopeleka maji kwenye mashamba ya mpunga.
 
Mmoja wa wananchi hao, Erasto Mbilo, ambaye ni miongoni mwa waathirika wa kubomolewa nyumba katika tukio hilo, alisema alikuwa katika  shughuli zake za kujitafutia riizki na ndipo alipopewa taarifa kuwa maji yamejaa ndani ya nyumba yake.
 
Alisema alipokwenda nyumbani, alikuta maji tayari yameshabomoa upande mmoja wa nyumba na kusomba kitanda pamoja na godoro lake. Alisema baadhi ya majirani zake walikwenda kumpa msaada kwa kutoboa upande wa pili wa nyumba yake ili maji yapate njia ya kutokea. Naye Khadija Kinywafu, aliyekuwa mpangaji katika nyumba inayomilikiwa na Rehema Mpwepwa, alisema wakiwa ndani, walisikia kishindo nyuma ya nyumba yao na alipotaka nje kuangalia kulikoni, alikuta maji yamezingira nyumba anayoishi.
 
“Nilikimbia kwenda kuwaokoa wanangu na kuwahifadhi katika nyumba ya jirani yangu,” alisema. Alisema katika nyumba yao, walifanikiwa kuokoa vitu vichache, lakini magunia mawili wa mahindi, magunia matatu ya mpunga na nguo zote vilisombwa na maji ya mto huo.
 
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Tembo Ringa, alisema mvua hiyo ilianza kunyesha juzi saa 10:00 jioni hasa katika milima ya Uwanji ambako ndiko chanzo cha mto Chimala.
 
Alisema muda mfupi baadaye, alipigiwa simu na baadhi ya wananchi wakimjulisha kuwa kijiji chake kimekumbwa na mafuriko. 
 
“Nilipoiona hali hiyo, niliwasiliana na  Diwani wa kata hiyo, Francis Mtega, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mbarali ambaye alifika eneo la tukio,” alisema. Alisema walikubaliana familia zote zilizoathiriwa na mafuriko hayo, zihifadhiwe katika ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya Chimala. Kwa mujibu wa Ringa, Diwani Mtega alitoa Sh. 170,000 kwa jili ya chakula na vyandarua kwa ajili ya waathirika wa tukio hilo wakati akiendelea kufanya mawasiliano na serikali ili itoe msaada zaidi.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!