Mvutano kati ya Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kutaka kubomoa nyumba anayoishi Mchungaji Getrude Rwakatare umezidi kushika kasi mahakamani.
Hali hiyo ilitokea jana, baada ya wakili wa familia ya Mchungaji Rwakatare, Emmanuel Agustino kupinga maombi ya NEMC ya kutaka kuongezewa muda wa kuwasilisha maombi ya mapitio ya hukumu ya maridhiano inayozuia baraza hilo kuchukua hatua yoyote dhidi ya nyumba hiyo.
Hukumu hiyo ya maridhiano ilitokana na kesi iliyofunguliwa 2012 katika Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi na Robert Brighton, ambaye ni mtoto wa Mchungaji Rwakatare aliyepinga kubomolewa kwa nyumba hiyo kwa madai kuwa imejengwa mahali pasiporuhusiwa.
Hukumu hiyo ilitolewa na Jaji Hamisa Kalombola Mei 11, 2015, pamoja na mambo mengine, alisema pande zote zilikubaliana kuwa, NEMC na wadau wake wasimbughudhi Brighton katika makazi hayo.
Hata hivyo, Desemba 29, 2015, NEMC ilifungua tena maombi ya kutaka kupatiwa kibali cha kuongezewa muda wa kuwasilisha maombi ya kufanya mapitio ya hukumu hiyo.
Katika maombi hayo namba 825 ya mwaka 2015, NEMC inadai kutoitambua hukumu hiyo na kwamba, uamuzi huo ulifikiwa na mwanasheria wake ambaye hakupatiwa idhini na NEMC.
Hata hivyo, wakati maombi hayo yalipotajwa mahakamani hapo Jumatatu wiki hii, Wakili Agustino kwa niaba ya mjibu maombi (Brighton), aliwasilisha hati ya kiapo kinzani dhidi ya hati ya kiapo cha NEMC kilichoapwa na Mkurugenzi wake Mtendaji, Bonaventure Baya akipinga maombi hayo ya NEMC.
Jaji John Mugeta anayesikiliza shauri hilo, aliamuru watoa maombi wawasilishe mahakamani hapo majibu ya kiapo kinzani cha mjibu maombi kabla ya Januari 20 na akapanga kusikiliza maombi hayo Januari 21, 2016.
MWANANCHI.
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment