Monday 25 January 2016

MOI YAMTEMA MGONJWA WA MAGUFULI"



Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) imeiarifu serikali kuwa imekamilisha kazi yake ya kumpatia matibabu mgonjwa Chacha Makenge, maarufu kama 'mgonjwa ma Magufuli'.

Habari kutoka ndani ya MOI zinasema hatua hiyo imechukuliwa baada ya hospitali hiyo kufanikiwa kumuondoa wodini ambako aling’ang’ania kuendelea kuishi kwa muda mrefu.

Makenge alibaki MOI licha madaktari kumruhusu kurudi nyumbani baada ya afya yake kuimarika.

Taarifa zilisema hospitali hiyo imepeleka ripoti kamili kuhusu kazi ilizofanya kumuhudumia mgonjwa huyo, ikiwamo kumpatia matibabu ya mgongo, chakula, malazi na gharama ya kumrudisha nyumbani kijiji cha Mugumu mkoani Mara.

Ofisa Habari wa MOI, Patrick Mvungi, alisema anachofahamu ni kwamba Makenge yuko wodi ya magonjwa ya akili na hali yake itakapoimarika atatakiwa kuhudhuria kliniki kila baada ya wiki mbili.

“Makenge tumempatia huduma zote, kila aliyemuona kipindi cha nyuma atathibitisha kwamba amepona matatizo yake, lakini baada ya kugundua ana matatizo ya kiakili tunaona busara wenzetu Muhimbili watusaidie,” alisema Mvungi.

Aliongeza kwamba madaktari wamethibitisha kuwa Makenge hana tena matatizo ya mgongo lakini  wataendelea kumfanyia uchunguzi.

Mvutano kati ya MOI na mgonjwa huyo uliibuka miezi miwili iliyopita baada ya Makenge kugoma kutoka wodini, licha ya hali yake kuimarika.

Umaarufu wa Makenge ulikuja baada ya kukutana na Rais John Magufuli, alipofanya ziara ya ghafla Novemba 9 mwaka jana MOI, na kumpatia mamalalamiko ya ukosefu wa huduma ya mashine za CT-Scan na MRI pamoja na wagonjwa kulala chini.

Rais Magufuli aliamuru mgonjwa huyo kupatiwa matibabu kwa gharama zake na aliagiza fedha zilizokuwa zitumike kwa ajili ya sherehe za kulizindua Bunge zinunue vitanda vya Hospitali ya Muhimbili.

Mwanzoni mwa mwezi Desemba, MOI iliingia gharama ya kumrudisha mgonjwa huyo nyumbani, ikiwa ni pamoja na kumnunilia tiketi na fedha za kujikimu njiani, lakini haikufanikiwa baada ya Mekenge kugoma kuondoka.

Januari 13 Hospitali hiyo ilifanikiwa kumuondoa wodini na kumpeleka kitengo cha magonjwa ya akili baada ya kupata kibali cha Mahakama ya Wilaya ya Ilala.

Licha ya kugoma kuondoka, Makenge alikuwa akifanya matendo ambayo yana dalili ya matatizo ya akili ikiwa ni pamoja na kuondoka asubuhi na kurudi MOI kulala usiku na kutolea madakatari na wauguzi lugha zisizo na staha.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!