RAIS John Magufuli ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu amemwongezea mwaka moja zaidi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Davis Mwamunyange ambaye alikuwa astaafu leo.
Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari Makao Makuu ya Jeshi hilo Upanga, Dar es Salaam, Mwamunyange alieleza kuwa “Mimi mwenyewe ilikuwa nistaafu kazi tarehe 31 Januari 2016, lakini Mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu ameamua kunibakiza katika utumishi jeshini kwa mwaka mmoja kuanzia tarehe 31 Januari 2016 hadi tarehe 31 Januari 2017”.
Pia, Jenerali Mwamunyange alisema Rais Magufuli amemteua Luteni Jenerali Venance Mabeyo kuwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi ; na pia ameteua maofisa wakuu wengine, kushika nyadhifa mbalimbali katika jeshi.
Akifafanua kuhusu uteuzi wa maofisa hao wakuu, Mwamunyange alisema Rais Magufuli amemteua Meja Jenerali James Mwakibolwa kuwa Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu, kuchukua nafasi ya Meja Jenerali Salum Kijuu, ambaye anastaafu kazi leo.
Kabla ya uteuzi huo, Mwakibolwa alikuwa ni Mkuu wa Tawi la Utendaji Kivita na Mafunzo Makao Makuu ya Jeshi. Rais Magufuli pia amemteua Meja Jenerali Yakub Sirakwi kuwa Mkuu wa Chuo cha Ulinzi wa Taifa (NDC), kuchukua nafasi ya Meja Jenerali Gaudence Milanzi, ambaye aliteuliwa na Rais kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Meja Jenerali Sirakwi alikuwa Mratibu Msaidizi Mkuu wa Baraza la Usalama la Taifa. Mwingine ni Brigedia Jenerali George Ingram, ameteuliwa kuwa Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Anga, kuchukua nafasi ya Meja Jenerali Joseph Kapwani anayestaafu kazi leo.
Brigedia Jenerali Ingram alikuwa ofisa mnadhimu katika makao makuu ya Kamandi ya Jeshi la anga. Brigedia Jenerali M.W. Isamuhyo ameteuliwa kuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa kuchukua nafasi ya Meja Jenerali Raphael Muhuga anayestaafu kazi leo.
Kabla ya uteuzi huo, Isamuhyo alikuwa Mkurugenzi Makao Makuu ya Jeshi. Magufuli pia amemteua Brigedia Jenerali Jacob Kingu kuwa Mkuu wa Shirika la Mzinga, kuchukua nafasi ya Meja Jenerali Charles Muzanila, anayestaafu leo.
Kingu alikuwa Mkuu wa Utawala na Mafunzo katika makao makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa. Katika uteuzi huo, Magufuli amemteua Brigedia Jenerali Robison Mwanjela kuwa Mkuu wa Chuo cha Tiba Lugalo, kuchukua nafasi ya Brigedia Jenerali Msangi anayestaafu leo.
Kabla ya uteuzi huo, Mwanjela alikuwa Mkuu wa Tiba Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo. Mwingine aliyeteuliwa na Rais ni Brigedia Jenerali George Msongole kuwa Kamanda wa Brigedi ya Tembo, kuchukua nafasi ya Brigedia Jenerali J.M Chacha ambaye anastaafu leo.
Brigedia Jenerali Msongole alikuwa ni Ofisa Mnadhimu makao makuu ya Jeshi. Brigedia Jenerali Sylevesta Minja ameteuliwa kuwa Mkuu wa Chuo cha Ukamanda na Unadhimu, kuchukua nafasi ya Meja Jenerali Ezekiel Kyunga anayestaafu leo.
Brigedia Jenerali Minja alikuwa Mkuu wa Utawala katika Chuo cha Ulinzi wa Taifa (NDC). Mwamunyange kwa niaba ya Rais Magufuli aliwapongeza maofisa wakuu wote, walioteuliwa kushika nyadhifa hizo na kuwatakia kila la heri katika nyadhifa hizo mpya.
No comments:
Post a Comment