Watu wanaosadikiwa kuwa majangili wameitungua helikopta ya doria inayomilikiwa na kampuni ya Mwiba Holdings na kusababisha kifo cha rubani wake ndani ya kitalu cha uwindaji kilichopo wilayani Meatu, Mkoa wa Simiyu.
Rubani wa helkopta hiyo, Rodgers Gower ni raia wa Uingereza, ambaye katika tukio hilo alikuwa ameambatana na raia wa Afrika Kusini, Nicky Bester, aliyenusurika.
Bester alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 11:30 jioni.
Akizungumza jana jijini hapa, Meneja Mkuu wa kampuni ya Legendary Expeditions inayomiliki kampuni ya utalii alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
“Nina simanzi sana na nimeshtushwa na tukio hili baya, naomba ni vyema mtupatie muda tuweze wa kutulia,” alisema.
Tukio hilo limemvuta Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe kufika Arusha jana akitokea kwenye vikao vya Bunge Dodoma, na kuendelea na safari ya Simiyu.
Akiwa katika ofisi za za Mwiba Holdings jijini hapa, Baster alikataa kuzungumzia kwa undani tukio hilo akisema hajapata ruksa ya kufanya hivyo kutoka kwa meneja mkuu.
Lakini habari zilizopatikana hapo zilisema chopa hiyo yenye namba za usajili 5 HFGF ilikuwa ikifanya doria katika eneo hilo baada ya kupatikana kwa mabaki ya tembo.
“Bester alinusurika katika tukio hilo na kujificha katika miti ambapo aliwapigia simu walinzi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), kwa msaada,” alisema ofisa mmoja katika ofisi za Mwiba Holdings.
Ilielezwa kuwa kabla ya kutokea kwa tukio hilo, walinzi wa kampuni ya Mwiba walikamata pikipiki mbili zinazodaiwa kuwa za majangili.
No comments:
Post a Comment