Tuesday 26 January 2016

Magufuli atengua uteuzi bosi NIDA


RAIS John Magufuli ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu na wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Madeni Kipande kutokana na kukabiliwa tuhuma mbalimbali.


Maofisa wengine wanne wa NIDA pia wamesimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi wa namna Sh bilioni 180 zilivyotumiwa na mamlaka hiyo wakati wananchi waliopatiwa vitambulisho vya taifa na mamlaka hiyo ni wachache.
Maofisa waliosimamishwa kazi ni Mkurugenzi wa Tehama, Joseph Makani, Ofisa Ugavi Mkuu, Rahel Mapande, Mkurugenzi wa Sheria, Sabrina Nyoni na George Ntalima ambaye ni Ofisa Usafirishaji.
Akizungumza Ikulu Dar es Salaam, jana, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema kiasi cha fedha zilizotumiwa na NIDA ni kikubwa na Rais angependa ufanyike uchunguzi na ukaguzi jinsi zilivyotumika kutokana na kuwepo malalamiko kutoka kwa wananchi, kuwa kuna kasi ndogo ya utoaji wa vitambulisho vya taifa.
“Hivyo Rais ameelekeza Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) wafanye ukaguzi maalumu wa manunuzi yote yaliyofanywa na NIDA,” alisema Sefue.
Aliongeza kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imeagizwa pia kufanya uchunguzi kujiridhisha kama kulikuwa na vitendo vya rushwa.
Alisema Rais pia ameelekeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), afanye ukaguzi maalumu wa hesabu za NIDA, ikiwemo ukaguzi wa thamani ya fedha baada ya kuthibitisha idadi halisi ya vitambulisho vilivyotolewa hadi sasa.
Kuhusu Kipande, Balozi Sefue alisema RAS huyo hajathibitishwa kwenye cheo cha Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, kwani hajamaliza miezi sita. Hata hivyo, alisema Rais hakuridhika na utendaji wake wa kazi.
Kipande aliteuliwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete kushika wadhifa huo baada ya kuondolewa Mamlaka ya Bandari (TPA), ambako alikuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu.
Mabalozi warejeshwa nyumbani
Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa kuwarejesha nyumbani mara moja mabalozi wawili, ambao mikataba yao imeisha.
Mabalozi hao ni Batilda Buriani aliyeko Tokyo nchini Japan na Dk James Msekela aliyeko Rome, Italia.
Pia, Balozi Sefue alisema Rais amemrejesha nyumbani Balozi wa Tanzania aliyeko London, Uingereza, Peter Kallaghe. Balozi huyo anarejea wizarani ambako atapangiwa kazi nyingine.
Rais pia amemteua Mahadhi Juma Maalim kuwa Balozi wa kwanza wa Tanzania nchini Kuwait.
Kwa maana hiyo, vituo sita vya ubalozi viko wazi ambavyo ni London nchini Uingereza, Tokyo Japan, Rome Italia na Brussels Ubelgiji kutokana na aliyekuwa Balozi, Dk Deodorous Kamala kuchaguliwa kuwa Mbunge, Kuala Lumpar, Malaysia kutokana na Balozi Dk Aziz Mlima kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa na Brasilia, Brazil baada ya Balozi Francis Malambugi kustaafu.
Maagizo mazito kwa watumishi
Akizungumzia utendaji ndani ya Serikali, Sefue alisema lazima viongozi na watumishi wa umma wawahudumie wananchi kwa haki, weledi, uadilifu na heshima.
Alitaka kila ofisi ya Serikali iwe na dawati la kusikiliza shida za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.
Pia aliagiza kuanzia sasa watumishi wote wa umma, wavae majina yao ili iwe rahisi kwa mwananchi kumtambua anayemhudumia.
Alisema itakuwa rahisi mwananchi huyo kumsifu mtumishi huyo kwa kumhudumia kwa weledi na kwa uaminifu na kwa wakati na kumtolea taarifa yule anayefanya mambo ya hovyo.
Aliagiza kila kwenye ofisi ya mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya, wajenge uwezo wa kushughulikia shida za wananchi kwa ukamilifu na kwa wakati ili kutosababisha wananchi kufunga safari hadi Ikulu Dar es Salaam kumwona Rais.
“Kwa muundo wa Serikali yetu, hakuna sababu kwa mwananchi kufunga safari mpaka Ikulu kwa kuamini kuwa ni Rais tu anayeweza kumaliza matatizo yake, maana wawakilishi wa Rais wako kila pembe ya nchi yetu,” alisema Balozi Sefue na kuongeza “Wananchi wakifika Ikulu, ina maana hao wawakilishi wa Rais hawakutimiza wajibu wao.”
Wakati huo huo, Sifa Lubasi kutoka Dodoma anaripoti kuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Agustino Kalinga amevuliwa madaraka kwa kushindwa kusimamia utekelezaji wa maelekezo sahihi ya serikali kuhusu utoaji wa elimu ya msingi bila malipo.
Pia, Ofisa Elimu Vifaa na Takwimu, Josephine Akim amesimamishwa kazi huku Ofisa Elimu Msingi Manispaa ya Dodoma, Scolla Kapinga akipewa onyo kali.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene alisema hayo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini hapa. Aliwaonya wakurugenzi wote nchini, kusimamia vizuri maagizo ya serikali.
Alisema imebainika kuwa mkurugenzi huyo, ameshindwa kuwasimamia watumishi walio chini yake hadi kusababisha kuandikwa na kusambazwa kwa barua kwa walimu wakuu wa shule za msingi manispaa ya Dodoma, ambayo inatofautiana na maelekezo ya serikali yaliyopo kwenye mwongozo na ameshindwa kusimamia maagizo sahihi ya serikali.
Simbachawene alisema kusimamishwa kwa mkurugenzi huyo, kunafuatia ziara ya kushtukiza katika shule ya Msingi Dodoma Makulu na kubaini Ofisi ya Mkurugenzi Manispaa ya Dodoma imetoa barua Januari 17, mwaka huu kwenda kwa walimu wakuu yenye mada kuhusu maombi ya kibali cha kuchangisha michango katika shule za msingi.
Alisema lengo la barua hiyo, lilikuwa ni kuwataka wazazi kupitia mikutano wachangie ulinzi, umeme na maji.
Alisema uchangiaji huo ulioelekezwa katika barua ya mkurugenzi ni kinyume cha maelekezo na Rais John Magufuli, Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 ya kutoa elimu ya msingi bila malipo.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!