Pages

Saturday, 2 January 2016

KIPINDUPINDU CHATUA GEREZANI




Mahabusu wawili wa Gereza la Wilaya ya Musoma mkoani Mara, wamefariki dunia baada ya kukumbwa na ugonjwa wa kipindupindu
Mkuu wa gereza hilo, Shaku Humba alisema kuwa wafungwa saba na mahabusu watano walioripotiwa kuugua ugonjwa huo.


Hata hivyo hakuwataja majina marehemu hao akisema kuwa hana mamlaka kisheria hadi hapo taratibu zitakapokamilika.
Mganga Mkuu wa Manispaa ya Musoma, Dk Honorata Rutatenisigwa alisema mahabusu wanaogua ugonjwa huo wamelazwa katika kambi ya gereza hilo.
Dk Rutatenisigwa alisema usafi katika gereza hilo unaendelea kusimamiwa kwa karibu, huku unyunyiziaji wa dawa ya kuua wadudu na kutoa huduma ya kwanza kwa wengine ambao hawajakumbwa na ugonjwa huo ikiendelea.
“Kutokea kwa vifo hivyo vya mahabusu wawili kumefanya kuwa na jumla ya watu 11 waliofariki dunia kutokana na ugonjwa wa kipindupindu mjini Musoma,” alisema.
Wagonjwa hao walifariki kwa nyakati tofauti, baada ya kuugua ugonjwa huo uliolikumba gereza hilo Desemba 29, mwaka jana.
Alisema ugonjwa huo hadi unalikumba gereza hilo uliingia mjini hapa miezi miwili iliyopita.
Dk Rutatenisigwa alisema juhudi za kuudhibiti zinaendelea.
Tayari ugonjwa huo umeikumba mikoa yote ya Kanda ya Ziwa, Mwanza ukiongoza kwa kuathirika zaidi kutokana na idadi ya wagonjwa kuwa zaidi ya 900 katika wilaya zake zote pamoja na vifo zaidi ya watu 25.
Wilaya za mkoa huo ambazo zimekuwa zikiripoti kuwa wagonjwa mara kwa mara ni Ukerewe, Ilemela, Magu na Nyamagana.
Ili kukabiliana na ugonjwa huo, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, imepiga marufuku uuzaji ovyo wa vyakula.

MWANANCHI.

No comments:

Post a Comment