Bunge la 11 limeweka historia ya aina yake baada ya zaidi ya askari 50 kuingia ndani ya ukumbi na kuwatoa kwa kuwabeba wabunge wa upinzani kutokana na kukataa amri ya Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, ya kuwataka watoke kwa hiari.
Chanzo cha tukio hilo ni kutokana na kauli ya serikali kwamba Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), halitarusha moja kwa moja vikao vya Bunge, jambo lililopigwa tangu kwenye kikao cha asubuhi na kusababisha kiahirishwe.
Baadaye, baada bunge kurejea jioni na mwenyekiti kusoma uamuzi wa kamati ya uongozi, wabunge wa upinzani walianza kuomba mwongozo.
Baada ya wabunge kadhaa kuomba mwongozo na wengi zaidi kuendelea kujitokeza, Chenge aliwataja baadhi ya wabunge wa upinzani na kuwataka waende nje kwa madai kuwa walikuwa wanafanya fujo, jambo lililosababisha wenzao wote kusimama na kupinga amri hiyo.
Baada ya bunge kuahirishwa kwa dakika 10, zaidi ya polisi 50 na wengine wa usalama wa taifa pamoja na askari kanzu, waliingia ndani ya ukumbi wa bunge na kuwataka wabunge wote wa upinzani watoke ndani ya ukumbi wa Bunge.
Hatua hiyo ilipingwa na wabunge hao, na kuanza kubishana kwa takribani dakika 30 na hata askari walipoingia baadhi yao walianza kuzozana nao. Hali ilipozidi kuwa mbaya, wabunge wanaume walivua tai zao na kuendelea kubishana na wenzao.
Mbunge wa kwanza kuanza kukunjwa na askari hao ni wa Kilombero, Peter Lijualikali, ambaye alishikwa na askari wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) na kutolewa kwenye kiti chake mpaka eneo inapowekwa siwa.
Wabunge wengine walivyoona hivyo, waliingilia kati na kumtoa huku mbunge huyo akivua koti lake na kutunishiana misuli na askari hao.
Wabunge wengine waliorushiana ngumi na askari ni Halima Mdee (Kawe), Mwita Waitara (Ukonga) na John Heche (Tarime Vijijini).
Heche kwa upande wake alidai kuwa, askari hao walimpiga mkononi na kitu kizito na alipokwenda hospitalini aliambiwa arudi kesho kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Baada ya kutoka katika ukumbi wa Bunge, Mbunge wa Viti Maalumu, Sabrina Sungura, alianza kuangua kilio akisema amedhalilishwa kwa kuvuliwa nguo na askari hao. Alisema alivuliwa hijabu yake na kuibiwa cheni na hereni zake.
Mbunge wa Liwale, Zuberi Kuchauka, alidaiwa kupigwa na kuumizwa vibaya hali iliyosababisha apumzishwe kwenye zahanati ya Bunge wakati Mbunge wa Micheweni, Juma Kombo, akidai kupigwa na kuvuliwa nguo.
Katika tukio hilo lililodumu kwa takriban dakika 40, wakiwa katika ukumbi wa Bunge, askari mmoja alionekana kuwarushia wabunge maneno makali.
“Nakwambia uheshimiwa wako huko huko, mimi hapa nitakuchapa sasa hivi,” alisikika askari huyo akisema maneno hayo.
Mdee alisema licha ya kichapo walichopata wabunge wengi wakiwa ndani ya ukumbi wa Bunge, pia walipigwa walipotolewa nje.
“Ukishatoka pale ukumbini kabla hujafika nje, kuna eneo ambalo watu hawaoni ndipo kulikuwa na askari wengi wanapiga watu,” alisema.
Mbwa watumika
Katika mlango wa kutoka nje ya ukumbi huo, kulikuwa idadi kubwa kubwa ya askari wengine wakiwa na mbwa.
Askari hao walifunga mageti ya kwenda kwenye ukumbi huo pamoja na ule wa Pius Msekwa, hali iliyofanya waandishi wa habari kushindwa kwenda eneo walilokuwa wakitokea askari hao.
Waandishi watimuliwa
Baada ya hali kuwa mbaya zaidi kwenye ukumbi wa Bunge, maofisa wa usalama wa taifa na watumishi wa Bunge nje ya ukumbi waliwakataza waandishi kupiga picha.
Hata wale walioonekana kujaribu kupiga picha kwa kutumia simu, walinyang'anywa na maofisa wa usalama wa taifa na kuzifuta.
Kauli ya Bunge
Baada ya Bunge la jioni kurejea, Chenge alilieleza Bunge kuwa Kamati ya Uongozi imekaa na kukubaliana kuwa Mwenyekiti wa Bunge alikuwa sahihi alipokataa kuahirisha mkutano wa Bunge ili kauli ya Nape ijadiliwe.
Alisema kamati hiyo pia imeona hakuna haki ya bunge iliyovunjwa kwa mujibu wa haki, kinga na madaraka ya bunge, hivyo hoja ya kujadili hotuba ya Rais iendelee kama ilivyokuwa imepangwa.
“Endapo kuna mbunge ambaye hataridhika na uamuzi huu, ni haki yake kutumia kanuni kuwasilisha malalamiko yake kwa Katibu wa Bunge,” alisema Chenge.
Baada ya kauli hiyo, Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, aliomba mwongozo kwa kuhoji kwa nini suala hilo limejadiliwa na Kamati ya Uongozi badala ya ile ya kanuni au kiti cha Spika. Chenge alimjibu kuwa hakuna kanuni iliyovunjwa kwa hatua iliyochukuliwa.
Baada ya jibu hilo, Mbunge wa Babati Mjini pia wa Chadema, Paulina Gekul, aliomba mwongozi kwa kutumia kanuni ya 49 (2), ambayo inakataza kauli za mawaziri zinazotolewa bungeni zisizue mjadala.
Akijibu hoja hiyo, Chenge alisema: “Wakati namjibu Zitto nilisema kama yeye anaona kauli yake imeibua mjadala ambao kanuni haziruhusu, ndiyo msingi huo ambao nimesema alete huku.
Kanuni ya 52 (2) ambayo hoja hii ilitolewa na waziri mkuu jana, huwezi tu ukaisitisha kwa namna hiyo, ndiyo maana nasema tuheshimu kanuni hizi, nawasihi sana tuendelee na mjadala.”
Heche naye aliomba mwongozo na kusema kutorusha matangazo hayo moja kwa moja ni kuvunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano, ibara ya 18, inayozungumzia uhuru wa kupata habari na kutoa, na Chenge kusema kwa jinsi ambavyo kanuni zinamruhusu atatoa mwongozo huo baadaye.
Baada ya jibu hilo, wabunge wengi zaidi wa upinzani walisimama kutaka kupewa mwongozo na kiti, hali ambayo ilisababisha wenzao wa CCM kuwaambia watoke nje.
Baada ya kelele kuzidi, Chenge aliyekuwa amepokea kikaratasi kutoka kwa mmoja wa wasaidiza wake, alisoma majina ya Lissu, Ester Bulaya (Bunda Mjini), Godbless Lema (Arusha Mjini) na Gekul na kuwataka watoke nje ya ukumbi wa Bunge.
Hali hiyo ilifanya wenzao waanze kuzomea zaidi, hatua iliyomfanya Chenge ahairishe Bunge na kuamuru askari waingine kuwatoa.
KIKAO CHA ASUBUHI
Zilikuwa dakika 25 kwa Chenge, kukalia kiti cha Spika kwa mara ya kwanza akiwa mwenyekiti wa Bunge, zilizowasha moto ndani chombo hicho cha kutunga sheria pale hoja ya serikali ya kuachana na matangazo ya moja kwa moja yanayorushwa na TBC, ilipowachefua wapinzani na kusababisha kikao cha asubuhi kuvunjika.
Hali ya hewa bungeni ilichafuka baada ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, kutoa kauli ya serikali juu ya TCB kutorusha matangazo ya moja kwa moja ya majadiliano ndani ya Bunge kwa kile alichosema ni gharama kubwa kwa shirika hilo.
Alisema TBC ilianza kurusha matangazo hayo mwaka 2005 na kwamba kabla ya hapo ilikuwa ikiyarekodi na kisha kuyarusha usiku kwenye kipindi kilichoitwa ‘leo katika bunge’ kipindi alichosema kilikuwa kikionyesha mambo muhimu yaliyotokea bungeni.
Alisema kwa sasa gharama za kurusha matangazo hayo zimepanda na kufikia Sh. bilioni 4.2 kwa mwaka kwa mikutano minne ya Bunge, hivyo TBC itakuwa hairushi tena matangazo na badala yake itakuwa inarekodi na usiku kurusha vitu muhimu vilivyotokea kwa muda wa saa moja.
Baada ya kauli hiyo, hali ya hewa ilibadilika baada ya wabunge wa upinzani kusimama kutaka mwongozo wa spika.
Mbunge aliyeanza kusimama ni Zitto Kabwe wa Kigoma Mjini (ACT- Wazalendo), ambaye alisimama kwa kutumia Kanuni ya 69 inayohusu kuahirishwa kwa Bunge.
Chenge alimtaka Zitto aketi kwa maelezo kwamba kwa utamaduni wa Bunge, kauli za mawaziri zikishatolewa huwa hazijadiliwi.
Hali hiyo ilifanya kuwapo kwa kurushiana maneno kati ya wabunge wa upinzani na kiti cha spika kwa upande mmoja na wabunge wa CCM wakirusha maneno kwa wabunge wa upinzani.
Baada ya Chenge kushikilia kauli yake hiyo, Halima Mdee alisimama na kumwambia: “mbona una papara, si usikilize?”
Malumbano hayo yaliendelea mpaka pale Zitto alipokubali kusoma kanuni hiyo na vifungu vyake viwili kama alivyoelekezwa na kiti kisha kutoa hoja yake na kusema TBC si shirika la kibiashara na kutorusha matangazo hayo ni kuwanyima wananchi fursa.
“Hotuba ya Rais tunayoijadili ilionyeshwa moja kwa moja, iweje muhimili wa Bunge unapoijadili isionyeshwe moja kwa moja ili wabunge wajadili na watoe maazimio,” alisema Zitto.
Ndipo Chenge aliposimama na kusema: “Nimemsikiliza kwa makini Zitto kwa hoja yake ambayo msingi wake unaanzia Kanuni ya 49 inayohusu kauli za mawaziri.
“Kwa mujibu wa mazoea yetu kauli za mawaziri hazijadiliwi bungeni lakini hilo halizuii mbunge kuleta hoja binafsi kupitia katibu kwa taratibu ambazo zimewekwa.
“Uamuzi wangu kwamba kama Zitto unaona kuna umuhimu wa hoja hizo kuletwa, naomba ulete taarifa hiyo kwa taratibu hizo. Uamuzi wangu ni kwamba kuahirisha mjada wa Rais haitakuwa uendeshaji bora wa shughuli za Bunge. Naagiza meza tuendelee.”
Kauli hiyo ilionekana kuwakera zaidi wabunge wa upinzani ambao walisimama kwa wingi na kuanza kusema lazima hoja ya Zitto isikilizwe huku wakirushiana maneno.
Kutokana na hali hiyo, Chenge alisimama tena na kuwaambia wabunge hao kuwa kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, kiti cha spika hakiwezi kupewa taarifa kama ambavyo baadhi ya wabunge walikuwa wakiomba.
Baada ya kauli hiyo, majibizano yalihama na kuwa kati ya Chenge na Halima Mdee.
Halima: Mwenyekiti hoja kuhusu haki za Bunge.
Change: Halima nakusihi uketi.
Halima: Hoja kuhusu haki za Bunge
Chenge: Nakusihi uketi
Halima : Naomba unisikileze basi.
Chenge: Halima nakusihi uketi.
Halima: Hoja kuhusu haki za Bunge Kanuni ya 55 kifungu cha pili.
Baada ya kauli hiyo, wabunge wa upinzani walitulizana na baadhi yao kuwataka wenzao waketi hali iliyompa nafasi Chenge kuendelea na kikao.
“Samahani sana wabunge, tukienda hivi kwa kulazimishana yale tunayotaka hatutaenda. Nimemwomba Zitto anayetaka kutoa taarifa kufuata utaratibu.
"Halima unataka kuleta hoja ya haki za Bunge, unataka Bunge tukusikilize, alichosema zitto nimesema mkalete hoja binafsi, zitazungumzwa na Bunge hili. Mimi nataka tujielekeze kwenye shughuli muhimu zilizo mbele yetu,” alisema Chenge.
Baada ya kauli hiyo, Halima alisikika akisema:“Hakuna shughuli muhimu zaidi ya wananchi kutusikiliza tunazungumza nini.” Wabunge wengine wa kambi ya upinzani walisikika wakipaza sauti kwa kusema ‘usituburuze’
Baada ya kauli hizo kuzidi, Chenge alisema: “Sitaki kufika kutumia mamlaka ya kiti”.
Kauli hiyo ilionekana kuwakera zaidi wabunge wa upinzani ambao wengi waliwasha vipaza sauti na kuanza kusema: “Tumia mamlaka ya kiti”, usituburuze, usitutishe, tumechoka kuburuzwa, huwezi kuzuia TBC kienyeji hivyo.”
Naye Mbunge wa Konde, Khatib Said Haji, alisikika akisema: “Sisi hatutongozani humu, lazima wananchi wasikie tunachozungumza ni nini.”
Baada ya kauli hiyo, Chenge alimsihi tena Halima kuketi kwa maelezo kwamba yeye ndiye aliyeanzisha hoja hiyo na watu kusimama.
Kutokana na wabunge hao kukubali kuketi, Chenge alisema hoja iliyowasilishwa na wabunge hao ni nzuri na nyeti hivyo anasitisha vikao vya Bunge ili Kamati ya Uongozi ikae na kulipitia kisha Bunge lingerejea baada ya saa sita na nusu mchana.
Kauli hiyo iliwafurahisha wabunge wa upinzani ambao walianza kuimba, Chenge, Chenge, Mtemi, Mtemi, huku wenzao wa CCM wakiwa wamenyamaza kimya.
Saa 6:30 ilipofika, Chenge alirudi tena na kuahirisha Bunge mpaka saa 10 jioni kwa maelezo kuwa Kikao cha Uongozi kinaendelea.
Maoni ya Wabunge
Waitara alisema serikali kuchukua uamuzi huo ni kukiuka demokrasia na kwamba juzi walipomuuliza Nape sababu za TBC kutokurusha matangazo hayo alisema ni kwa sababu ya kuharibika kwa mitambo.
Alisema kwa namna moja CCM wanatumia njia hiyo ili kama njia ya kuibia wapinzani majimboni kwao, na kwamba hawana mchango wowote na kazi yao bungeni ni kulala.
Naye Devotha Minja, alisema serikali haina sababu ya msingi ya kuizuia vyombo vya habari kwa kuwa ni haki ya wananchi kusikiliza wawakilishi wao.
Pia, baadhi ya wabunge wa CCM, walipinga hatua hiyo ya serikali wakisema lazima kuna jambo inataka kulificha.
CCM waweka msimamo
Baada ya kuahirishwa kwa Kikao cha Bunge, wabunge wa CCM walikutana kwenye kikao cha ndani na mmoja wa wabunge walioudhuria alisema walimbana Nape kwa taarifa yake hiyo kwa kumweleza kuwa alikosea namna alivyoiwasilisha.
“Tumemwambia angetakiwa aje na hoja nzito zaidi ya kwamba kama Bunge linadaiwa na TBC tuone namna ya kulipa. Lakini tumesema matangazo ya moja kwa moja yaendelee ingawa kwa sasa ni vigumu kwa sababu tunadaiwa.
Kama ni kubana matumizi, wabunge wabanwe kwenye mambo ya magari na posho zingine ili matangazo ya moja kwa moja yaendelee. Tumekubaliana kila mtu achangie kutokana na hoja itakavyoletwa hiyo jioni,” alisema mmoja wa wabunge wa CCM.
WADAU WA HABARI WAPINGA
Wadau mbalimbali wa habari nchini wamepinga vikali hatua ya serikali kutangaza uamuzi wa TBC kutorusha tena vipindi vya Bunge, katika jitihada zake za kupunguza gharama, huku wakieleza iko ajenda ya siri nyuma ya jambo hilo linalolenga kuwanyima wananchi haki yao kikatiba.
Wadau hao walisema hatua hiyo haina afya kwa demokrasia ya nchi na ni kurudisha utawala wa kiimla na kijima katika nchi ambayo ilishatoka kwenye mfumo huo.
Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti, wameitaka serikali kufikiria upya juu ya uamuzi huo kwa kuwa kodi za Watanzania ndizo zinatumika na wana haki ya kujua kile wanachokizungumza wawakilishi wao katika mhimili huo muhimu.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga, alisema nchi yoyote inapimwa kwa masuala ya uwazi na ushirikishwaji kama mambo yake yanatangazwa au ni siri, kigezo cha uongozi, jamii na kwa kiasi gani Bunge lake linatangazwa.
Alisema kama kigezo ni kupunguza gharama hakina mashiko kwa kuwa TBC ni mali ya umma inayolipiwa kodi na wananchi ili kuwafikishia taarifa na vipindi mbalimbali ambavyo vyombo binafsi haviwezi kurusha.
Naye Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa, alisema uamuzi huo ni wa kushtusha kwa kuwa nchi ilishafikia jitihada za kuweka uwazi ili wananchi wapate taarifa kwa mujibu wa Katiba.
Alisema vipindi vya moja kwa moja viliwezesha wananchi kuwaona wawakilishi wao na kwamba si vizuri kuchuja wanayoyazungumza kwa niaba yao. Aliwaomba wabunge bila kujali itikadi zao kupinga jambo hilo kwa kuwa linaathari kwao na wasipofanya hivyo wananchi wana haki ya kuwaona ni wasaliti.
Mwanazuoni wa Sayansi ya Siasa na Utawala, Prof. Mwesiga Baregu, kwa upande wake alisema uamuzi huo wa serikali ni ishara ya kurudisha nchi katika utawala wa kiimla, kubana demokrasia iliyojengwa kwa muda mrefu.
Alisema Watanzania wanatakiwa kuanza kudai haki, kupinga hatua hiyo kwa kuwa ni kuminya utoaji, utafutaji na uhuru wa habari hasa kwa kupitia sheria zilizoanza hivi karibuni kama Sheria ya Makosa ya Mtandao.
Alisema iwapo inafikiriwa kuwa demokrasia ni ghali, Watanzania wasubiri kushuhudia ubabe katika demokrasia.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Deus Kibamba, alisema hatua hiyo ni mwendelezo wa kuwanyima Watanzania taarifa ambayo ni kinyume cha ibara ya 18 ya Katiba.
Alisema ibara hiyo inasema, kila mtu ana haki ya kupata taarifa, kuzipokea na kuzisambaza bila kujali mipaka wakati wowote.
MBOWE, MBATIA WAZUNGUMZA
Baada ya kutolewa bungeni, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alikutana na waandishi wa habari na kusema sababu ya gharama iliyotolewa na serikali bungeni ilibadilika wakiwa kwenye kikao cha kamati ya uongozi na badala yake ikasema uamuzi wa kuzuia matangazo ya vikao vya Bunge moja kwa moja umechukuliwa ili watu wafanye kazi badala ya kuangalia Bunge.
Mkutano huo na waandishi wa habari pia uliudhuriwa na Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe na Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia.
“Kwenye kamati ya uongozi nyie hamkuwapo mimi nilikuwapo na Zitto pamoja na Mdee. Baada ya Zitto na Mdee kutoa hoja zao, mjadala ukahama kutoka kwenye fedha na kusema uamuzi huo umechukuliwa ili Watanzania wafanye kazi kwa sababu kwa kuangalia televisheni watu hawafanyi kazi na kwamba watu wengi hawaangalii televisheni mchana ila wanaangalia usiku.
Tulipinga hoja hiyo kwa kusisitiza huu ni mpango wa serikali ambao ulianza kabla ya uchaguzi, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.
Leo ni miezi mitatu tangu tumalize uchaguzi lakini hata sisi haturuhusiwi kufanya mikutano, kitendo cha kusema TBC wao ndiyo tu warekodi na baadaye waamue nani arushwe na nani asirushwe hewani siyo haki,” alisema Mbowe.
Alisema wamekataa hoja hiyo, lakini cha kushangaza Mwenyekiti wa Bunge na makatibu wao wakakimbia kiti na kuacha askari waliendeshe.
Alisema wamepata taarifa kuwa, lengo la serikali ni kuzuia mjadala wa Zanzibar, hoja za uchaguzi mkuu na maamuzi mabovu yaliyofanywa na serikali ya awamu ya tano yasiwafikie wananchi.
“Tulikuwa tumejiandaa kutumia hii ‘forum’ (jukwaa) kuonyesha wananchi upande wa pili kwa kile kilichofanyiwa na serikali hii ya Magufuli”.
Mbowe pia alisema baadhi ya wabunge wameibiwa simu zao, saa, pochi na vitu vingine vya thamani.
Kwa upande wake, Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia, alisema anachokifanya Rais John Magufuli ni kutaka kuibana demokrasia ili aonekane anafanya kazi, lakini hawatakubaliana na hali hiyo na kwamba watapigania demokrasia hadi tone la mwisho ili kuona haki inatendeka.
Imeandikwa na Fredy Azzah, Beatrice Shayo, Dodoma, Salome Kitomari na Chrstina Mwakangale, Dar
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment