Wednesday 27 January 2016

KESI YA BOMOA BOMOA YASIMAMISHWA KWA SIKU 60



Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi, imetoa uamuzi wa kusimamisha mchakato wa bomoabomoa kwa siku 60 kwa wakazi wa mabondeni zaidi ya 600, ili wajitathimini kama wanaweza kufungua kesi ya msingi dhidi ya serikali.
 
Uamuzi huo ulitolewa jana mahakamani hapo jijini Dar es Salaam mbele ya Mwanasheria wa Serikali, Grace Mbunda na Wakili wa waombaji, George Mwalali na Jaji Penterine Kente, kuhusu maombi ya wakazi hao ya kupinga kubomolewa nyumba zao pamoja na kutaka kufungua kesi ya msingi.
 
Awali, Jaji Kente alisema uamuzi wa maombi hayo utatolewa kwa njia mbili kutokana na mgawanyiko wake, ukiwamo wa kutoa amri kwa Manispaa ya Kinondoni, Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (Nemc), kutobomoa nyumba hizo.
 
Katika uamuzi huo uliochukua takribani saa moja, Jaji Kente alisema baada ya kupitia hoja za pande zote mbili, mahakama imekubali ombi la wananchi hao kufungua kesi ya msingi, lakini limekubaliwa kwa masharti.
 
Alisema kutokana na ugumu uliopo katika shauri hilo, mahakama imetoa siku 60 zitakazoisha Machi 27, mwaka huu kwa ajili ya walalamikaji hao kuangalia uwezekano wa kufungua kesi dhidi ya serikali.
 
Jaji Kente alieleza kuwa hatua ya kutoa uamuzi huo inatokana na mahakama kufuata misingi ya haki za binadamu kutokana na wakazi hao kushindwa kutimiza baadhi ya masharti yaliyotolewa.
 
Akibainisha masharti hayo, Jaji Kente alisema la kwanza ni kuhusu waombaji hao kama wanaonyesha wana kesi dhidi ya serikali, pia kama kuna uzito wa kufungua kesi hiyo kwa misingi ya haki kwamba inaangukia wapi sambamba na waombaji hao kama watapata hasara isiyopingika.
 
Baada ya kueleza hayo, alisema kuwa katika masharti yote waombaji hao wamekidhi sharti la mwisho la kwamba kama watapata hasara isiyopingika kutokana na kuvunjiwa nyumba zao.
 
“Katika hayo, suala kubwa ni hilo la kupata hasara kutokana na kupoteza nyumba na mali, lakini pia tunaweza kujiuliza kutokana na hoja za serikali kama nyumba ni muhimu kuliko binadamu,” alisema.
 
Pia, alieleza kuwa inajulikana kama mchakato huo utasababisha maumivu makali kwa watu hao kutokana na kukosa makazi na kwamba itaumiza sana kuona familia za kipato cha chini zikiwa zinahangaika kwa kuvunjiwa nyumba.
 
Kuhusu serikali mara baada ya kuisha kwa siku hizo 60, Jaji Kente alisema inaweza kuendelea na mchakato huo mara baada ya kuisha kwa siku hizo, Machi 27, mwaka huu.
 
“Serikali inaweza kuendelea na mchakato wake kama kawaida endapo kama kesi ya msingi haitafunguliwa, kikubwa ifuate misingi ya haki na sheria katika utekelezaji wake,”alisema Jaji Kente.
 
Awali, katika usikilizwaji wa shauri hilo, Wakili Mkuu wa Serikali, George Malata, aliiomba mahakama kutosikiliza maombi ya wakazi hao kwani hawakuzingatia masharti.
 
Alidai kwamba, katika maombi ya wakazi hao saba wanaowawakilisha wenzao 674, ilipaswa waombaji hao wajulikane idadi yao kwa ujumla na kuonyesha uhalali wa uwakilishi wao kama waliwachagua.
 
 “Shauri hili liliwasilishwa mahakamani hapa Januari 8, mwaka huu na waombaji kupitia mawakili wao waliomba liwekwe zuio la kutobomolewa nyumba zao, lakini tangu  kuwasilisha kwa maombi hayo hadi leo (jana) hii…hawajaleta majina yao wala mahakama haiwatambui kwa sababu hakuna nyaraka zozote wala maridhiano kama wamekubaliana,” alieleza.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!