Friday, 15 January 2016

JE WAFAHAMU HISTORIA YA MKOA WA MARA?


Mkoa wa Mara ni miongoni mwa mikoa 30 ya Tanzania. Mkoa huu upo Kaskazini Mashariki mwa Tanzania, unapakana na Nchi za Kenya na Uganda kwa upande wa Kaskazini, Mkoa wa Kagera kwa upande wa Magharibi, Mikoa ya Mwanza na Simiyu kwa upande wa kusini na Mkoa wa Arusha kwa upande wa Mashariki. Kijiografia, Mkoa huu upo kati ya Latitudo 10 0’ na 20 31’ kusini mwa Ikweta na kati ya Longitudo 330 10’ na 350 15’ Mashariki mwa mstari wa Greenwich.



Kuitawala Mkoa umegawanyika katika Wilaya 6 ambazo ni Musoma, Bunda, Butiama, Serengeti, Tarime na Rorya. Aidha, Mkoa wa Mara umegawanyika katika Halmashauri 7, Tarafa 20, Kata 154, Vijiji 487 na Mitaa 57.
Historia ya Mkoa wa Mara inaanzia mwaka 1916 wakati huo eneo la kiutawala la sasa la mkoa (North Mara na South Mara) likijulikana kama Wilaya Ndogo ya Musoma (Musoma Sub District), Major J.M. Coote, akiwa Afisa Mfawidhi (officer Incharge) wa Utawala wa Kiingereza kuanzia tarehe 1/1/1917. Ikumbukwe kuwa wakati huo Musoma Sub District (Wilaya Ndogo), ilikuwa ni sehemu ya Wilaya ya Mwanza na hapakuwa na Mikoa. Kufuatia mabadiliko ya kiutawala yaliyofanywa wakati wa utawala wa Mwingereza, Wilaya Ndogo ya Musoma iligawanywa na kuwa Wilaya za North Mara na South Mara zikitenganishwa na mpaka wa asili wa mto Mara. Wakati huo Wilaya hizo zilikiwa sehemu ya Lake Province ikijumuisha Mikoa ya Mwanza, Kagera Shinyanga na Simiyu ya sasa. Baada ya Uhuru, majimbo yote yalibadilishwa kuwa Mikoa, hivyo Lake Province ikawa Lake Region hadi mwaka 1963, ilipoanzishwa Mikoa ya sasa ikiwa ni pamoja na Mkoa wa Mara na hivi karibuni Simiyu.
Mkoa wa Mara (pamoja na Mikoa ya Kigoma, Mwanza, Moshi na Ruvuma ulianzishwa tarerhe 01/05/1963 kwa maelekezo ya Waraka Na.  VPC.9/50/02 wa tarehe 07/03/1963) na kuifanya mikoa kuwa 13 kwa wakati huo. Bw. M.T. Spearing – Afisa Mfawidhi aliteuliwa kukamilisha taratibu (logistics) za kiutawala.Tangu wakati huo Makao Makuu yakawa Musoma mpaka sasa. Mkuu wa Mkoa wa kwanza alikuwa Mhe. Oswald Mang’ombe Marwa kati ya mwaka 1963 hadi 1965. Hadi sasa Mkoa umeongonzwa na Wakuu wa Mikoa 13 akiwemo Mkuu wa Mkoa wa sasa Mhe. John Gabriel Tuppa aliyeanza Septemba 2011. Katibu Tawala wa kwanza wakati huo akijulikana kama “Administrative Secretary – Mara”, alikuwa ni Bw. M.T. Spearing kati ya mwaka 1963-1964. Hivi sasa Mkoa umeongozwa na Makatibu Tawala 19 akiwemo Katibu Tawala aliyestaafu mwaka 2012 Bw.Clement F. Lujaji. Kati ya mwaka 1975 na 2010 zimeanzishwa Wilaya mpya za Serengeti (1974), Bunda (1978), Rorya (2007) na Butiama iliyotangazwa (2010).
Mkoa wa Mara ni chimbuko la Viongozi mashuhuri akiwemo Rais wa Kwanza na Muasisi wa Taifa hili Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere ambaye alizaliwa tarehe 13/04/1922 katika kijiji cha Butiama. Alifaliki akiwa katika matibabu kwenye hospitali, London Uingereza, tarehe 14/10/1999 na kuzikwa Mwitongo katika kijiji cha Butiama. Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ndiye muasisi wa Chama cha TANU 1954 – 1977, kilichoongoza harakati za Uhuru. Aidha, Mwalimu alikuwa Muasisi wa Chama Cha Mapinduzi kilichoanzishwa tarehe 05/2/1977 baada ya Vyama vya siasa vya TANU na AFRO SHIRAZI kuungana. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sasa ni Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.
Viongonzi wengine wa kitaifa ambao ni wazaliwa wa Mkoa huu ni Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba, Waziri Mkuu Mstaafu, Mzee Timoth Apiyo aliyekuwa Katibu Mkuu wa kwanza Ofisi ya Rais, Katibu Mkuu Mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi, Mhe. Wilson Mkama na Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania wa sasa Mheshimiwa Amina N. Makilagi, Mheshimiwa Charles Nyirabu Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania, Jaji Fredrick Werema, Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa sasa. Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Waziri wa sasa, Mhe. Stephen M. Wasira Waziri wan chi ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Mhe. Gaudensia Mugosi Kabaka, Waziri wa Kazi na Ajira, Mhe. Dkt Makongoro Mahanga, Naibu Waziri Wizara ya Kazi na Ajira kwa sasa. Mawaziri Wastaafu, Mhe. Prof Philimon Sarungi, Waziri, wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Balozi I.M Bhoke Munanka, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mhe.Dkt Wanyancha James Mnanka, Naibu Waziri, Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Mhe.Dkt Deogratius Mwita, Naibu Waziri wa Nchi (TAMISEMI).
Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro wa sasa, Lt.Col.(Mst) Issa Machibya. Wakuu wa Mikoa wastaafu, Joseph W. Butiku, na Balozi Nimrod M. Lugoe. Wakuu wa Majeshi Wastaafu Jenerali David Msuguri, Jenerali Mwita Kyaro na Jenerali Joseph Waitara. Mabalozi Wastaafu, Balozi Joshua Opanga, Balozi James Ndobho na Balozi Alex Mganda.
Eneo la Mkoa ni kilometa za mraba 30,508 sawa na asilimia 3.1 ya eneo la Tanzania Bara. Kati ya eneo hilo lote la Mkoa kilometa za mraba 10,942 ni eneo la maji sawa na asilimia 36 na kilometa za mraba 19,208 sawa na asilimia 64 ni eneo la nchi kavu.
Kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Taifa ya mwaka 1958, eneo la mkoa wa sasa lililokuwa linawakilishwa na Wilaya za North Mara na South Mara lilikuwa na watu 194,939. Sensa zilizofuatia zilionyesha kuwa mwaka 1967 ulikuwa na watu 544,125, mwaka 1978 watu 723,827, mwaka 1988 watu 946,418, mwaka 2002 watu 1,368,602 na mwaka 2012 ni watu 1,743,830. Kwa kufuata sensa hiyo, Mkoa ulikuwa na ongezeko la asilimia 2.5 kwa mwaka.
Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa wastani wa pato la mkazi kwa mwaka limekuwa likiongezeka mwaka hadi mwaka. Mwaka 2000 wastani wa pato la mkazi ilikuwa sh.222.704/=, mwaka 2006 sh.461,860/=, mwaka 2007 sh.494,014/=, mwaka 2009 sh. 600,388/= na mwaka 2012 sh.642,528/=. Kukuwa kwa pato kumetokana na jitihada za makusudi zilizofanyika katika kuboresha uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo. Aidha, pamekuwepo na mazingira mazuri yaliyowezesha sekta binafsi kuwekeza katika maeneo mbalimbali kama viwanda, utalii, biashara na uchimbaji madini.
Makabila makuu ya Mkoa Mara ni Wakurya, Wajaluo, na Wajita. Wakurya ni kabila kuu la Wilaya za Tarime na Serengeti ambapo Wajita ni kabila kuu la Wilaya ya Musoma na Bunda. Wajaluo ni kabila kuu la Wilaya ya Rorya. Makabila mengine yaliyopo Mkoani ni Wazanaki, Wangoreme, Wasuba, Waikizu, Waisenye, Waikoma, Wakwaya, Waruri, Washashi, Wanata na Wasweta. Historia inaeleza kuwa wakati wa ukoloni, Wilaya za North Mara na South Mara ambazo ndizo zinaunda Mkoa huu wa sasa, zilikuwa na tawala za machifu (Chiefdoms).

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!