Tuesday, 19 January 2016

"HOUSE BOY" AIBA BASTOLA YA MWAJIRI WAKE NA KUFANYIA UHALIFU


Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewakamata watu wawili, akiwamo mfanyakazi wa ndani wa kiume mwenye umri wa miaka 18, kwa tuhuma za kuiba bastola ya bosi wake na kushirikiana na mtuhumiwa mwenzake kuitumia katika uhalifu.


Kamanda wa polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema watuhumiwa hao walikamatwa Januari 9.

Alisema silaha hiyo inamilikiwa kihalali na Samweli Samwang’ombi, mkazi wa Bunju na kabla ya kuibwa alikuwa akiitunza katika moja ya vyumba nyumbani kwake, lakini baadaye aligundua kuwa mfanyakazi wake wa kiume ameiba na akatoa taarifa polisi.
“Mfanyakazi huyo aliitumia katika uhalifu akishirikiana na mwenzake,” alisema Sirro.
Alisema alipohojiwa alikiri kuiba bastola hiyo aina ya Compaq CZ75D yenye namba TZCAR 100416 iliyotengenezwa Jamhuri ya Czech na baada ya kuhojiwa alionyesha alikoificha eneo la Mtoni Kwa Azizi Ally, Temeke.
ambapo baada ya kufanya ufuatiliaji alikamatwa kijana mwingine mwenye umri wa miaka 24 mkazi wa Kilwa Road.
Akieleza namna kijana wa pili alivyokamatwa Kamanda Sirro alisema, “Kijana huyu baada ya kukamatwa alieleza kuwa kuna siku alikwenda kijana mmoja katika aneo la biashara yake hapo Mtoni na kununua soda. Baadaye kijana huyo alimtishia kwa bastola ili atoe fedha lakini alipambana naye kwa kushirikiana na wananchi na ndipo mhalifu huyo alipotelekeza silaha hiyo,” alisema.
Katika hatua nyingine, watu wawili wanashikiliwa kwa tuhuma za kujihusisha na mtandao wa kuuza dawa za kulevya hapa nchini huku wakiendelea kumhoji mtuhumiwa mwingine kwa tuhuma hizo hizo.
Kamanda Sirro alisema watuhumiwa hao walikamatwa na kilo tisa za dawa za kulevya aina ya heroine kutoka nchini Pakistan. Alisema mmoja wa watuhumiwa hao ni mkazi wa Tegeta Nyuki anayetuhumiwa kusafirisha dawa za kulevya na usafirishaji haramu wa binadamu.
“Huyu mtu anatuhumiwa kwa kumsafirisha mkazi wa Ununio na kumweka rehani huko Pakistan kisha akachukua dawa ya kulevya kwa mali kauli,” alisema
Aidha, alimtaja mtuhumiwa mwingine kuwa ni meneja wa kampuni moja ya Bureau De Change anayetuhumiwa kushirikiana na genge la wauzaji dawa za kulevya na kusafirisha kiasi kikubwa cha fedha kwa njia zisizo rasmi.
Kamanda Sirro alisema mwaka 2014 kiasi cha kilo 304.91 za hereone na kilo 68 za cocaine zilikamatwa na watuhumiwa 14501 ambapo miongoni mwao Watanzania walikuwa 14467. Mwaka 2010 alisema zilikamatwa kilogramu 123 za heroine.
Pia, Kamanda Sirro alisema Jeshi la Polisi limefanikiwa kukamata magari manne yaliyokuwa yameibwa maeneo tofauti ya jiji Dar es Salaam na mikoani.

MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!