Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bibi Rosebud Kurwijila (Aliyesimama) akiwapungia wakulima waliojitokeza wakati wa hafla ya utiaji saini makubaliano ya mikopo kati ya TADB na wakulima wadogo wadogo wa mkoa wa Iringa, katika kijiji cha Igomaa, wilayani Mufindi mkoani Iringa.
Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), wakiwapungia wakulima waliojitokeza wakati wa hafla ya utiaji saini makubaliano ya mikopo kati ya TADB na wakulima wadogo wadogo wa mkoa wa Iringa, katika kijiji cha Igomaa, wilayani Mufindi mkoani Iringa.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bibi
Rosebud Kurwijila (Kushoto) akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Bibi Amina Masenza
(Kulia) wakifuatilia kwa makini matukio wakati wa hafla ya utiaji saini
makubaliano ya mikopo kati ya TADB na wakulima wadogo wadogo wa mkoa wa Iringa,
katika kijiji cha Igomaa, wilayani Mufindi mkoani Iringa.
Mkurugenzi
Mwendeshaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Thomas Samkyi
(Kushoto) akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Bw. Kasunga (Kulia).
Mkurugenzi
Mwendeshaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Thomas Samkyi
(aliyesimama) akizungumza wakati wa hafla hiyo.
Mkurugenzi
wa Mikopo na Biashara wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw.
Robert Pascal (Kulia) akimsikiliza Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Kisheria wa
Benki, Bibi Neema Christina John (aliyevaa miwani) wakati wa uhakiki wa fomu
zilizojazwa na moja kati ya vikundi vilivyofanikiwa kupata mkopo kutoka Benki
hiyo.
Mwanasheria
mwandamizi wa TADB, Bibi Salome Masenga (Kulia) akimuelekeza mmoja wa
wanakikundi waliopata mikopo kutoka Benki hiyo.
Picha zote kwa hisani ya TADB
Benki
ya maendeleo ya kilimo kuanzisha ofisi za kanda
Na Mwandishi wetu, Iringa
Benki
mpya ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imesema hadi kufikia miaka mitano
ijayo itakuwa imefungua ofisi sita za kikanda zenye lengo la kuwahudumia
wakulima nchi kote.
Mikakati
hiyo iliwekwa bayana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya benki hiyo, Bibi
Rosebud Kurwijila wakati wa hafla ya utiaji saini makubaliano ya mikopo kati ya
TADB na wakulima wadogo wadogo wa mkoa wa Iringa, katika kijiji cha Igomaa,
wilayani Mufindi mkoani Iringa.
Bibi
Kurwijila alisema kuwa TADB inalenga kutelekeza kwa vitendo Maelekezo ya
Serikali ya kupunguza changamoto zinazowakabili wakulima nchi kote.
Aliongeza
kuwa kwa sasa Benki inalenga kusambaa nchi nzima kwa kuanzisha Ofisi za Kikanda
ndani ya miaka mitano ijayo.
“Tunalenga
kuwafikia wakulima wote nchini kadri siku zinavyoendelea kwenda na kutegemea
mtaji unavyoongezeka ama upatikanaji wa fedha toka vyanzo mbali mbali ili
kuweza kuwawezesha kumudu shughuli zao za kilimo,” alisema.
Aliongeza
kuwa Benki inaleenga kuwajengea uwezo na kuanzisha Programu Maalumu ya Vijana
wajihusishao na shughuli za Kilimo cha kibiashara na kushirikiana na wadau
wengine kuhuisha shughuli za umwagiliaji na miradi ya kisasa ya umwagiliaji.
Malengo
mengine ni kutafuta fedha toka vyanzo mbalimbali zenye gharama nafuu kwa
minajili ya kuwakopesha Wakulima katika hatua zote za mnyororo wa ongezeko la
thamani kwenye mazao ya Kilimo na kupanua wigo wa utaoji mikopo toka Minyororo
Kumi na Minne (14) ya Mwanzo na kuhusisha pia mazao mengine ya Kilimo na pia
kuwaunganisha Wakulima na masoko ya ndani na nje ya nchi.
Akizungumza
katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mwendeshaji wa TADB, Bw. Thomas Samkyi amesema
kwamba Benki yake imedhamiria kuleta Mapinduzi yenye tija katika Sekta ya
Kilimo nchini ili kuchagiza na kusaidia kuwezesha Sekta ya Kilimo kutoka kilimo
cha kujikimu kwenda kilimo cha kibiashara ili kukuza uchumi na kupunguza
umaskini nchini.
Bw.
Samkyi alisema TABD imejizatiti kuchangia kwa kiasi kikubwa katika mapinduzi ya
kilimo kwa kuongeza tija na upatikanaji wa mikopo ya riba nafuu maalum kwa
sekta ya kilimo, kama njia ya kuleta Mapinduzi yenye tija kwa wakulima nchini.
“Benki
imejipanga kutoa mikopo yenye riba nafuu katika muda mfupi, wa kati na mrefu
kwa Wakulima wadogo wadogo, wa kati na
wakubwa, hususan kuziba pengo la upatikanaji wa fedha za kwenye mnyororo wa
ongezeko la thamani katika tasnia za kilimo, mifugo, uvuvi na mazao ya misitu
(ufugaji nyuki),” alisema Bw. Samkyi.
Mkurugenzi
huyo alisema kwamba kwa kuanzia walengwa wakuu wa TADB ni wakulima wadogo
wadogo, hatahivyo, hata wale wakulima wa kati na wakubwa watahudumiwa.
Bw.
Samkyi imejidhatiti katika kufanya tathmini ya kina katika mnyororo mzima wa
thamani ili kutambua mapengo na mapungufu yanayohitaji utatuzi kwa minajili ya
kuongeza thamani na ushindani kwenye masoko.
“Sera
ya TADB ni kutathmini mnyororo mzima wa thamani ili kutambua mapengo na
mapungufu yanayohitaji utatuzi, na ambayo utatuzi wake utaongeza tija na uwezo
wa ushindani kwenye masoko, na hivyo kukuza uchumi wa walio wengi na kupunguza
umaskini,” aliongeza.
Katika
hafla hiyo, jumla ya vikundi nane (8) vyenye jumla ya wakulima wadogo wadogo
857, vilimiza vigezo na kupewa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi
bilioni moja.
Kwa
mujibu wa Bw. Samkyi kabla ya kutoa mikopo hiyo, benki iliwatembelea na kutoa
elimu kwa wakulima jinsi ya kuimarisha vikundi vyao, ambapo jumla ya vikundi 89
vyenye jumla ya wanakikundi 21,526 vilifikiwa.
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mama Amina Masenza amewaasa Wakulima wote nchini
kutumia vizuri mikopo wanayopewa ili kuweza kutimiza malengo yao binafsi na ya
Serikali katika kusaidia upatikanaji wa utoshelezi na usalama wa chakula ambao
ni endelevu nchini Tanzania.
Mama
Masenza alisema kuwa wakulima wakitumia mikopo waliyopewa kwa malengo husika
watafika mbali na kuweza kuchagiza mikakati ya Benki hiyo katika kusaidia
Mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kilimo kibiashara ili
kukuza uchumi na kupunguza umaskini.
“Naamini,
wakati Benki ya Maendeleo ya Kilimo itapoanza kufanya tathmini ya mikopo hii
iweze kuona matunda ya uwekezaji wake hasa kwa nyie ambao mmeweza kubahatika
kupata fursa ya awali kabili kunufaika na huduma za TADB,” aliwasihi.
Mama Masenza aliwaomba wakulima hao kuwa Mfano Bora na wanaojitambua
vilivyo, hasa nia ya kutoka katika kiwango fulani cha maisha kwenda katika
hatua nyingine za juu zaidi kimaisha kwa kuongeza kipato na ubora wa kimaisha
kwa ujumla kupitia huduma za TADB.
“Nawasihi kutotumia pesa hizi kinyume na
malengo yaliyokusudiwa, kwani kwa kufanya hivyo, siyo tuu tunaiua Benki yetu
bali pia tunajimaliza wenyewe kiuchumi. Wito wangu kwenu ni kujipanga kwa dhati
ili kuweza kutimiza malengo makuu ya mikopo hii ambayo ni kuleta Mapinduzi
yenye tija katika Sekta ya Kilimo nchini kwa kusaidia upatikanaji wa fedha na
sera nzuri zitakazosaidia maendeleo ya kilimo nchini,” aliongeza.
Benki
ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ilizinduliwa Rasmi na Rais wa Awamu ya Nne wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, kwenye Kilele
cha Maadhimisho ya Siku ya Wakulima nchini, mnamo tarehe 8 Agosti 2015 mjini
Lindi. Uanzishwaji wa Benki hii ni utekelezaji wa malengo ya muda mrefu ya
Serikali, katika kuitikia wito wa wananchi na wadau wengine wa maendeleo ili
Tanzania iweze kupiga hatua endelevu za kimaendeleo.
No comments:
Post a Comment