Monday, 18 January 2016

ADC: TUTASHIRIKI UCHAGUZI WA MARUDIO ZANZIBAR



Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) kimesema kimejiandaa kushiriki uchaguzi mkuu wa marudio unaotarajiwa kufanyika Machi, mwaka huu visiwani Zanzibar.
 
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya chama hicho, Ayubu Kimangale, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.
 
Alisema wao kama chama cha siasa lengo lao ni kukuza chama kupitia chaguzi kama hizo, hivyo ni lazima washiriki kwa hali na mali.
Kimangale alisema wamejiandaa kusimamisha wagombea katika ngazi za urais, uwakilishi katika kila nafasi.
 
Aidha, baraza hilo la wadhamini limeteua viongozi wa muda baada ya wale waliokuwapo kusimamishwa kwa ajili ya kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma za kushindwa kuwajibika zinazowakabili.
 
Kimangale alisema uongozi huo wa muda utafanya kazi kwa kipindi cha miezi sita na baada ya hapo chama kitafanya uchaguzi wa kuchagua viongozi wapya.
 
Alisema viongozi waliosimamishwa ambao hawatakutwa na hatia wataruhusiwa kuwania nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo.
Miongoni mwa walioteuliwa kushika nafasi hizo kwa muda ni Jumapili Kaliki, nafasi ya Mwenyekiti, Khamisi Kombo, Makamu Mwenyekiti, Zamila Mrisho, Katibu Mkuu na Mvita Mangupili,  Naibu Katibu Mkuu.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!