Sakata la makontena 329 yaliyotoroshwa kinyemela bandarini na kukwepa kodi ya zaidi ya Sh. bilioni 80 limezidi kuchukua sura mpya baada ya watu wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi kuongezeka na kufikia 47.
Miongoni mwa waliokamatwa wamo wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao mali zao zinachunguzwa ili kujua walizipataje pamoja na baadhi ya wamiliki wa makontena hayo.
Akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Diwani Athumani, alisema idadi ya waliokamatwa imeongezeka ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa.
Alisema tangu kutokea kwa tukio hilo walikuwa wanawashikilia watuhumiwa 12 ambapo watano wanatokea TRA, watano kutoka Bandari Kavu ya Azam na wawili wamiliki wa makontena, hivyo kuongezeka kwa idadi hiyo kunatokana na msako ambao bado unaoendelea.
DCI alisema katika awamu ya pili ya msako huo wamefanikiwa kuwakamata wafanyakazi wa TRA 27 na wanane wakiwa ni wamiliki wa makontena hivyo kufanya idadi ya watuhumiwa wanaoshikiliwa mpaka sasa kufikia 47.
Alisema kati ya watuhumiwa hao wanane walifikishwa mahakamani juzi na wengine wanaendelea na uchunguzi kubaini wahusika katika tukio hilo ili wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.
DCI alisema kadri ushahidi utakapotolewa kwa wakati utafanikisha watuhumiwa hao kufikishwa mahakamani mara moja.
Alitoa wito kwa wananchi ambao wana taarifa za mali zinazomilikiwa na watuhumiwa hao kutoa taarifa ili ziwasaidie katika uchunguzi wao.
Mwishoni mwa wiki iliyopita serikali ya awamu tano chini ya Rais Dk. John Magufuli ilibaini ubadhilifu wa ukwepaji wa kodi kwa makontena 329 ambayo yameisababishia hasara serikali kiasi cha sh. bilioni 80.
Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa ambaye alifanya ziara ya kushutukiza bandarini hapo alibaini makontena hayo kupitishwa bila kulipia kodi tangu Julai mwaka huu.
Kutokana na ubadhirifu huo, Jeshi la polisi liliagizwa kuchukua hatua kwa wale wote ambao wamehusika katika suala hilo la ukwepaji wa kodi.
Kufuatia sakata hilo Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade alisimamishwa kazi huku jeshi la polisi likiwashikilia na maafisa kadhaa waandamizi wa mamlaka hiyo akiwemo Kamishina wa Forodha, Tiagi Masamaki.
Hadi sasa tayari makampuni 43 yamebainika kuhusika katika kupitisha makontena hayo na makampuni manne yamelipa kodi ya Sh. Bilioni 5.2 kwa TRA.
NIPASHE.
NIPASHE.
No comments:
Post a Comment