Sunday 13 December 2015

WATOTO WAFARIKI BAADA YA KUTUMBUKIA SHIMONI -GEITA

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Peter

Watoto wawili wamefariki dunia baada ya kutumbukia kwenye shimo lililojaa maji ambalo lilichimbwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa ajili ya kusimika nguzo.


Kaimu kamanda wa polisi mkoani hapa, Peter Kakamba alisema jana kuwa watoto hao walitumbukia shimoni juzi saa 10:00 jioni katika Kijiji cha Lwantaba wilayani Chato.
Aliwataja watoto hao wa familia moja kuwa ni Paulina Mateso (3) na Pastory Mateso (2).
Alisema watoto hao walikumbwa na mkasa huo wakati wakicheza kandokando ya shimo hilo.
Katika tukio jingine, mwendesha bodaboda mmoja mkazi wa Mwatulole mjini Geita ameuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani na watu wasiofahamika.
Kamanda Kakamba alisema mtu huyo, Cyprian Mzee (23) alfariki dunia wakati akitibiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita.
“Kuhusu tukio la bodaboda kuuawa, mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai mkoa anafuatilia kujua undani wa tukio hilo,” alisema Kakamba.
Alisema Mzee anadaiwa kutekwa na watu wasiojulikana usiku kisha kumpiga na kumpora pikipiki yake.
Katibu wa Waendasha Bodaboda Mkoa wa Geita, Shabani Juma alisema hilo ni tukio la tatu kutokea kwa kipindi cha miezi mitano iliyopita.
Katika tukio jingine la hivi karibuni, mwendesha bodaboda alivamiwa nyumbani kwake na watu wasiojulikana na kuuawa.
“Haya matukio kwa kweli yanasikitisha...tunaomba polisi wachunguze mauaji hayo. Tunaishi kwa shida. Watu wanauawa, wauaji hawakamatwi,” alisema Juma.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!