Monday, 28 December 2015

WASICHANA 2000 WAKIMBIA KUKEKETWA-TARIME

Wasichana wapatao 170 kutoka mugumu wilayani


Wasichana 2,118 wamekimbilia kwenye Kituo cha Kupinga Ukatili wa Kijinsia cha Masanga kinachomilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Mara wilayani Tarime ili kuepuka kukeketwa na wazazi wao.

Akizungumzia kuwapokea wasichana hao, katibu wa kituo hicho, Dickson Joseph alitaka Sheria ya Makosa ya Kujamiiana ipewe meno ili iweze kufanyiwa kazi na kumpa mtoto wa kike haki anaponyanyaswa.
“Tulianza kuwapokea wasichana hawa Novemba 15 kwa lengo la kuwapa elimu na hifadhi kwa wale waliotoka katika koo ya Warenchoka inayotekeleza ukeketaji,” alisema Joseph.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wasichana hao walisema katika kituo hicho wanapata mafundisho ya namna ya kukabiliana na mila hiyo potofu.
Alisema changamoto inayowakabili wasichana wengi ni kutokupokewa na familia zao pindi wanaporejea nyumbani.
Mmoja wa wasichana hao, Catheline Johanes alisema hali hiyo inasababisha wapoteze mwelekeo wa masomo yao, kwani wengi wao ni wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo.
Msichana mwingine, Angela Charles alisema Serikali inapaswa itoe elimu kwa jamii wakiwamo wazazi ili waachane na mila hiyo potofu kwa kuwa inasababisha matatizo wakati wa kujamiiana na kujifungua.
Alisema wazazi wanapaswa kufahamu kuwa ukeketaji una madhara na kwamba hakuna msichana aliyewahi kupata ugonjwa wa akili kwa kukataa kukeketwa.
“Tunawashauri watu waliokeketwa watoe elimu juu madhara ya ukeketaji ili watoto ambao watawazaliwa wasije kukeketwa,” alisema Johanes na kuongeza kuwa mila hiyo haina faida katika maisha.
Joseph alisema wazazi wamegawanyika katika makundi mawili, wapo wanaowapa ushirikiano ili kutokomeza ukeketaji na wengine hawatoi.
Alisema wasiotoa ushirikiano huwa wanatishia kuwatenga watoto wao pindi watakapokataa kukeketwa.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!