Thursday, 3 December 2015

WAPINZANI WPONGEZA UTENDAJI WA MAGUFULI

Mafundi wakiendelea na ujenzi wa Barabara ya
Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari amemshauri Rais John Magufuli kuipitia upya mikataba ya madini na kuifanyika marekebisho ili kuboresha maisha ya Watanzania.


Amesema rasilimali hiyo ndiyo inaweza kuwaletea maisha bora Watanzania badala ya kuelekeza nguvu kwenye ukusanyaji wa kodi pekee.

Profesa Safari na viongozi wengine wa vyama vya upinzani walitoa maoni yao jana kuhusu utendaji kazi wa Rais Magufuli tangu aapishwe Novemba 5, mwaka huu.
Alisema utaratibu aliouanzisha wa ukusanyaji wa kodi ni mzuri na utasaidia kuongeza makusanyo ya fedha zitakazotumika katika vipaumbele vyake, ikiwamo sekta ya elimu.
Alisema hata enzi ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere wanafunzi walisoma bure kwa sababu alipata fedha zilizotokana na madini ya almasi yaliyokuwa yakichimbwa kwenye mgodi wa Williamson Diamond wa mkoani Shinyanga.
Alisema nchi zinazoendelea kama Botswana ambayo ndiyo mfano wa kuigwa barani Afrika, inafanya vizuri kwa sababu ya kodi ya madini.
“Hizi kodi zinazokusanywa zitatusaidia kupata huduma za jamii, lakini maisha mazuri yatapatikana kwa kusimamia madini yetu vizuri,” alisema Profesa Safari.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Samson Mwigamba alisema chama hicho kimeridhishwa na kasi ya utendaji wa Rais Magufuli ya kufanya kazi nje ya mfumo wa CCM aliodai kuwa ni wa kulindana.
Alisema kitendo cha kumsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade kwa tuhuma za kushindwa kusimamia ukusanyaji wa mapato, inaonyesha kwamba yuko kwa ajili ya kazi na si kulindana.
Alisema Dk Magufuli ameweza kuchukua hatua hiyo kwa sababu hakuwa na mtandao uliomwingiza Ikulu.
“Hana deni kwa wanamtandao, ndiyo maana anachukua hatua za kupambana na ufisadi, tumsaidie na tumwombee aweze kutenda makubwa zaidi ya haya,” alisema Mwigamba.
Alisema kwa sasa anatakiwa pia kuweka mfumo bora wa kuzifanyia marekebisho sheria mbaya ili hata rais ajaye naye aweze kuzisimamia.
“Sheria zifanyiwe marekebisho ili kuzipa meno na si Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma pekee,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa zamani wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema kasi aliyoanza nayo Dk Magufuli si nguvu ya soda kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu.
Profesa Lipumba alisema hata alipokuwa waziri katika Wizara ya Ujenzi ya Serikali ya Awamu ya Nne, Dk Magufuli alikuwa akifanya kazi kwa kasi na umakini mkubwa.
Alisema anachopaswa kukifanya sasa ni kuwadhibiti watendaji wasio na maadili na kuweka mfumo mzuri wa utendaji kazi kwa viongozi wote kuanzia ngazi ya chini.
“Serikali inatakiwa kuweka mfumo wenye watendaji waadilifu watakaofanya kazi kwa kasi kama ya Rais ili tuweze kuyafikia mafanikio.
Tunajua kuwa Rais hawezi kusimamia kila mahali, bali akiwa na watendaji waaminifu, mambo yatakwenda kama anavyotaka iwe,” alisema Profesa Lipumba.
Katibu Mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK), Renatus Muabhi alisema licha ya kuwa Dk Magufuli ameanza vizuri, lakini anahitaji muda zaidi ili wananchi waweze kumpima.
“Ameanza vizuri, lakini tutamtendea haki kama tutampa siku 100 za kumpima kwa sababu bado hajaunda baraza la mawaziri ambalo ndiyo Serikali yake,” alisema na kuongeza:
“Marais wengi wanawekwa madarakani na matajiri ili waweze kufanikisha malengo yao, lakini rais wetu anaonyesha kwa vitendo kwamba si miongoni mwa marais wa aina hiyo.”
Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara alisema anachokifanya Rais Magufuli ni kile kilichokuwa kikipigiwa kelele na wapinzani.
Alisema ili aweze kufanikiwa zaidi, azifanyie kazi hoja za wabunge wa upinzani zinazozungumzia namna ya kudhibiti upotevu wa mapato na ubadhirifu wa mali ya umma.

MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!