Friday, 11 December 2015

WANAWAKE NANE WAINGIA BARAZA JIPYA LA MAWAZIRI

 
Idadi ya wanawake katika baraza jipya la mawaziri lililoundwa na Rais Dk. John Magufuli ni nane, ikilinganishwa na mtangulizi wake, Rais mstaafu Jakaya Kikwete, aliyewapa nafasi za uwaziri na na naibu uwaziri 15 kwa nyakati tofauti wakati wa uongozi wake wa miaka 10.
 
Katika Baraza la Mawaziri jipya lililotangazwa jana na Rais Dk. Magufuli wanawake walioteuliwa ni Mbunge wa Viti Maalum, Angela Kairuki, anayekuwa Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi, Utumishi na Utawala Bora, ambaye katika serikali ya Kikwete alikuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na pia aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria katika serikali hiyo.
 
Mwingine ni Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama, anayekuwa Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi Vijana, Ajira na Walemavu, ambaye katika serikali ya Kikwete alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Kuu, Sera, Uratibu na Bunge. Pia amewahi kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
 
Mwingine ni Mbunge wa Viti Maalum, Ummy Mwalimu, ambaye anakuwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ambaye katika serikali ya Kikwete alikuwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria. Pia amewahi kuwa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.
 
Pia yumo, Mbunge wa Nyasa, Stellah Manyanya, alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma na Mjumbe wa Kamati Teule ya Bunge la Tisa iliyoshughulikia sakata la Richmond na wakati wa serikali ya Rais mstaafu Kikwete.
 
Wengine ni Mbunge wa Ilemela, Angelina Mabula, wabunge wa Viti Maalum, Annastanzia Wambura na Dk. Susan Kolimba na Dk. Ashantu Kijaji, ambao wanaingia kwa mara ya kwanza serikalini kwa nyadhifa za Naibu Waziri. 
 
Katika Baraza la Kikwete wanawake walikuwa ni Dk. Mary Nagu, Dk. Asha Rose Migiro, Anne Malecela, Mwalimu, Kairuki, Prof. Anna Tibaijuka, Janeth Mbene, Sophia Simba, Dk. Tereza Huvisa, Saada Salum Mkuya, Samia Hassan Suluhu, Hawa Ghasia, Gaudensia Kabaka, Pindi Chana, Magreth Sitta, Zakhia Meghji na Marehemu Celina Kombani.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!