Tuesday 29 December 2015

WALIOFUKIWA NA KIFUSI MGODINI CHUNYA WATAJWA


Watu wawili wanahofiwa kufa baada ya kufukiwa na kifusi wakati wakichimba madini kwenye mgodi wa dhahabu wa wachimbaji wadogo wadogo katika Kijiji cha Sang’ambi wilayani Chunya.
 
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi (SACP), Ahamed Msangi, alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 12:00 jioni.
 
Aliwataja watu ambao wanaohifiwa kufa kwa kufunikwa na kifusi ndani ya mgodi huo kuwa ni Christopher Wambura ambaye alikuwa akiishi kijijini hapo lakini akiwa ni mwenyeji wa Musoma mkoani Mara na Riziki Simkoko mkazi wa Mbozi.
 
Akisimulia tukio hilo, Kamanda Msangi alisema kuwa aliyebaini kuwapo kwa watu waliofukiwa na kifusi ndani ya mgodi huo ni binti mmoja ambaye hajafahamika aliyekuwa akienda kwenye kambi la wachimbaji hao wadogo kwa ajili ya kuomba shoka.
 
Alisema binti huyo alipofika kwenye kambi hiyo hakuwakuta wachimbaji hao, lakini akaona kamba mbili zilizokuwa zimeingia kwenye shimo la mgodi uliopo karibu na kambi hiyo huku kukiwa na udongo ulioonekana  umeporomoka.
 
Kamanda Msangi, alisema binti huyo aliamua kuwaita wachimbaji hao kwa sauti na ndipo aliposikia sauti za watu zikiitika kutokea ndani ya shimo ambalo limeporomoka.
 
“Kusikia hivyo ndipo msichana huyo akapiga kelele na watu wakakusanyika na kuanza jitihada za kuwaopoa ndani ya shimo hilo la mgodi,” alisema Kamanda Msangi.
 
Hata hivyo, alisema wakati wananchi wakijaribu kuwaokoa watu waliofunikwa kwenye kifusi, udongo mwingine uliporomoka na kutaka kufukia watu wengine, huku baadhi ya waokoaji hao pia wakijeruhiwa.
 
Kamanda Msangi alisema wananchi hao baada ya kuona hivyo walisitisha zoezi la kuwaokoa watu hao na ndipo walipopiga simu kwa Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Elias Tarimo, kwa ajili ya kuomba msaada.
 
Alisema mkuu huyo wa wilaya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Chunya, akishirikiana na kamati yake walielekea kijijini hapo huku pia wakipeleka tingatinga kwa ajili ya kusaidia shughuli ya uokoaji.
Kwa mujibu wa Kamanda Msangi, hadi jana jioni watu hao walikuwa bado hawajaopolewa ndani ya shimo la mgodi na kwamba shughuli za kufukua kifusi kwa ajili ya kuwaokoa zilikuwa bado zikiendelea.
 
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoani hapa, Abbas Kandoro jana alitembelea kijijini hapo na kushuhudia shughuli za uokoaji zikiendelea.
 
Akizungumza na wananchi kijijini hapo, Kandoro aliwaonya wachimbaji wadogo wadogo kutoendelea kuchimba kwenye migodi hiyo kwa kutumia zana duni katika kipindi cha mvua kwa madai kuwa wanahatarisha maisha yao.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!