Sunday 13 December 2015

WAFANYABIASHARA KUPEWA BURE MASHINE ZA EFD


MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), inatarajia kuanza kutoa mashine za kielektroniki za kodi (EFD) bure kwa wafanyabiashara stahiki 200,000. Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, Dk Philip Mpango, alisema hayo jana wakati akizungumzia kukamilika kwa siku saba za wakwepa kodi, zilizotolewa na Rais John Magufuli.


Katika siku hizo saba zilizokwisha juzi, wafanyabiashara waliokwepa kodi kwa kutorosha makontena 329 yaliyokuwa katika bandari kavu ya Azam, walitakiwa kulipa kodi hiyo.
Akizungumzia uamuzi huo wa EFD, Dk Mpango alisema utoaji huo wa mashine bure, ni uamuzi wa kubadili utaratibu kwa kuwa utaratibu wa awali, wafanyabiashara walinunua mashine hiyo na kurudishiwa fedha zao wakati wa kulipa kodi.
Kwa mujibu wa Dk Mpango, uchambuzi wa wafanyabiashara wanaostahili kupewa mashine hizo, unaendelea nchi nzima kwa kuangalia ukubwa wa biashara ili wapewe mashine hizo kwa lengo la kuongeza wigo wa ukusanyaji kodi. Matumizi ya mashine hizo yalianza kutumiwa kwa awamu ya pili mwaka 2013, ikiwahusu wafanyabiashara ambao hawajasajiliwa kwenye VAT, lakini mauzo ghafi kwa mwaka ni Sh milioni 14 na zaidi.
Waliolengwa katika awamu hiyo walikuwa wafanyabiashara 200,000 wenye maduka ya vipuri, mawakili, maduka ya jumla, wafanyabiashara wakubwa wa mbao, migahawa mikubwa, maduka ya simu na vipuri vyake, baa na vinywaji baridi, studio za picha, huduma za chakula, wauzaji wa pikipiki, maduka makubwa ya nguo na biashara nyinginezo.
Katika mkutano na wafanyabiashara uliofanyika hivi karibuni, Rais Magufuli aliwashangaa TRA kwa kuacha kugawa bure mashine hizo na wao kubaki na kazi ya kukusanya mapato, kwani muda uliopotea na kodi ambayo haikukusanywa wakati wa mvutano na wafanyabiashara, ungetosha kununua mashine mpya na kuwagawia.
“Kama mnajua mashine hizi ni halali na ni zenu, wapeni bure kazi yenu iwe ni kukusanya kodi, ni hesabu rahisi sana isiyohitaji kwenda chuo kikuu, kwamba muda uliopotea na fedha hazifiki bilioni 12 zingetosha kununua mashine na kazi iwe ni kukusanya kodi,” alisema Rais Magufuli.
Katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, Jonson Minja alisema mashine za EFDs zitatumika kwa wafanyabiashara wote mwakani, kwa kuwa changamoto zilizosababisha mvutano baina yao na Serikali zimemalizika.
Tangu mwaka juzi kulikuwa na mvutano mkali baina ya wafanyabiashara na TRA, ambapo wafanyabiashara waligoma kutumia mashine hizo hadi Serikali itakaposhughulikia kero zao ikiwamo bei ya mashine, utitiri wa kodi, ukwepaji kodi na urasimu uliopo.
Wafanyabiashara kwa umoja wao waliitisha mgomo nchi nzima, kabla ya kuanza mazungumzo ya mara kwa mara na Serikali, ambayo wakati mwingine hayakufikia ukingoni, hatua iliyofanya baadhi ya viongozi wa wafanyabiashara kukamatwa. Imeandikwa na Theopista Nsanzugwanko na Ikunda Erick

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!