Sunday, 27 December 2015

VYAKULA VYA KUEPUKWA UNAPOPUNGUZA UNENE


Hivi karibuni Shirika la Afya Duniani (WHO), limeonya kuhusu ongezeko la watu wenye unene wa kupitiliza, huku wakitaja hiyo kuwa ni sababu kuu ya kuwapo kwa watu wengi wenye maradhi ya moyo, kisukari na ini.


Pamoja na watu hawa kuhitaji kufanya mazoezi kupunguza uzito wa miili yao, mtaalamu wa chakula na lishe, Dk Pazi Mwinyimvua, anashauri kufanya mazoezi kurandane na aina ya vyakula unavyokula.
Anasema mazoezi bila kuzingatia mlo sahihi ni kazi bure na yanaweza kukomaza baadhi ya maeneo mwilini, badala ya kuujenga mwili na kuufanya uwe na afya.
Dk Mwinyimvua anavitaja vyakula hatari kula wakati wa kufanya mazoezi ya kupunguza unene, kuwa ni vyenye sukari nyingi na mafuta mengi.
Sukari
Anasema sukari ni chanzo kikuu cha kuongeza unene, hivyo ni vema mtu anayefanya mazoezi kwa lengo la kupungua kujiepusha na vyakula vya aina hii vikiwamo soda, bia na hata zile soda zinazoelezwa kuwa hazina sukari.
Utafiti uliofanywa na chuo cha mazoezi katika Jiji la Florida nchini Marekani na kusimamiwa na Profesa Ahmedialkarim Mehdadi , ulionyesha kuwa matumizi ya sukari huongeza hatari ya kuwa na mwili ulionenepa, usiokaa vyema na hatari ya kupata maradhi ya ini na moyo.
Baadhi ya vyakula na vinywaji vyenye sukari nyingi ni pamoja na soda, bia, keki, chokoleti,
Vyakula vyenye mafuta mengi
Dk Mwinyimvua anavitaja vyakula hatari na vinavyoweza kupoteza ndoto za kupunguza mwili kwa mtu anayefanya mazoezi, kuwa ni vyakula vya kukaanga kama kuku, viazi mbatata, sambusa.
Katika utafiti uliosimamiwa na Profesa Mehdadi, pia ulitoa jibu la madhara ya kutumia mafuta mengi mwilini ukieleza kuwa mafuta mengi huleta madhara kwa wagonjwa wa kisukari, kwa sababu huongeza nguvu mwilini na vikikaa pamoja vinashindana kutoa nguvu mwilini na kuwa chanzo kikuu cha unene.
Utafiti ulieleza kuwa madhara ya mafuta mwilini ni pamoja na mirija ya kusafirisha damu kuwa na mafuta na kusababisha kuifinya njia ya kupitishia damu, hivyo inabidi nguvu ya ziada itumike kusukuma damu hiyo ili isambae mwilini kama inavyotakiwa.
Nguvu hii ni hatari ikiongezeka na hata ikipungua kwani husababisha matatizo ya shinikizo la damu la kushuka na kupanda.
Profesa Mehdadi, akishirikiana na madaktari walibaini mafuta mengi husababisha tumbo kujaa kutokana na vyakula yenye mafuta mengi kuchelewa kusagwa, ikilinganishwa na visivyo na mafuta kutokana na kuzuia kutolewa kwa vimeng’enyo muhimu vya uyeyushaji na hivyo kuchelewesha kazi ya usagaji chakula.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!