Wednesday 30 December 2015

VIBALI VYA KAZI KWA WAGENI KUKAGULIWA

 

Serikali meamua wakati wowote kuanzia mwezi huu kuanza kukagua vibali vya ajira za wageni nchini.
 
Hatua hiyo inafuatia baada ya siku 14 kumalizika zilizotolewa na serikali katika tangazo la utolewaji wa vibali vya kazi kwa wageni nchini.
Tangazo hilo lilisainiwa Desemba 14, mwaka huu na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Jenista Mhagama (pichani).
 
Katika tangazo hilo, Waziri Mhagama aliwataka waajiri wote nchini kwa muda wa siku hizo wawe wametekeleza matakwa ya Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni nchini Na. 1 ya mwaka 2015.
 
 “Katika taarifa tuliyoitoa mwezi huu, uliwajulisha waajiri wote wenye waajiri wa kigeni ambao wana vibali vya kazi za muda (Carry on Temporary Assignment) na wale wote wasiokuwa na vibali vya ajira vilivyotolewa na Kamishna wa Kazi nchini, kuwa wanatenda kosa. Kamishna wa Kazi amepewa mamlaka kutoa vibali vya ajira kwa wageni wanaotaka kufanya kazi nchini. Hivyo hakuna mamlaka nyingine yoyote inayoruhusiwa kutoa vibali vya ajira kwa wageni,” alisema Mhagama.
 
Aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati akizungumza na kikosi maalum kitakachoendesha operasheni hiyo chenye wajumbe kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uhamiaji na Wakala wa Usalama na Afya mahali pa kazi (OSHA), ikiwa lengo ni kufuatilia kama agizo lililotolewa na serikalil imefuatwa na kuhakikisha taratibu zinazopaswa kufuatwa katika utoaji wa vibali vya ajira zinazingatiwa.
 
“Serikali ilitoa siku 14 kwa waajiri wote wawe wametekeleza matakwa ya Sheria Na. 1 ya mwaka 2015 vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao,” alisitiza Mhagama.
 
Mwezi Machi, mwaka huu Bunge la 10 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni chini Na. 1 ya mwaka 2015 (The Non-Citizens (Employment Regulation) Act)).
 
Sheria ilianza kutumika rasmi tangu Septemba 15, mwaka huu. 
Sheria hiyo inaanzisha Mamlaka moja ya utoaji wa vibali vya ajira kwa wageni na mamlaka hiyo ni Kamishna wa Kazi.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!