HATUA anazozichukua Rais John Magufuli, katika kukabiliana na ufisadi ndani ya taasisi na idara za Serikali, zimeanza kuzaa matunda. Hatua hizo ambazo zinafahamika kama ‘kutumbua majipu’, pia zimeonesha kuungwa mkono na wasomi, wananchi, washirika wa maendeleo na mataifa mbalimbali ya nje.
Mathalani, kutokana na juhudi hizo za Rais, makusanyo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yameongezeka kutoka Sh bilioni 900 hadi Sh trilioni 1.3 kwa mwezi. Pia, Serikali imeboresha ukusanyaji wa mapato katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kwa kuhimiza matumizi ya mfumo wa kielektroniki.
Kwa upande wa reli, Serikali imetangaza kuwa itaanza kujenga reli ya kisasa (standard gauge) kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya Bara hivi karibuni, ili kuboresha usafiri kwa wananchi na kuongeza mizigo inayosafirishwa.
Hata hivyo, wizara iliyoathirika zaidi na hatua hizo za Rais ni Uchukuzi, ambayo katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Rais Magufuli hivi karibuni, Wizara ya Uchukuzi imeunganishwa na Wizara za Ujenzi na ile ya Mawasiliano; na sasa kutambulika kama Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Wizara hiyo ya Uchukuzi ilikuwa na taasisi zipatazo 13 zilizo chini yake. Hadi sasa Rais Magufuli ameshashusha rungu kwa taasisi tatu za juu, huku ikitarajiwa rungu hilo kuendelea kuzitafuna idara nyingine.
Taasisi ambazo zilikuwa chini ya Wizara ya zamani ya Uchukuzi ni Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO), Shirika la Huduma za Meli (MSCL), Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) na TPA.
Nyingine ni Shirika la Ndege (ATCL), Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA), Kampuni ya Reli (TRL), Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara), Chuo cha Bahari (DMI), Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) . Taasisi ambazo zimekamuliwa majipu yake hadi sasa ni TPA, RAHCO na TRL.
Tayari watendaji wakuu wa TPA na RAHCO, wamesimamishwa kazi na kuvunjwa bodi za wakurugenzi wa taasisi hizo; pamoja na bodi ya TRL na baadhi ya maofisa wake wa juu, wakiamuriwa kuchunguzwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Rais alitengua utezi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk Shaban Mwinjaka kutokana na kushindwa kwake kusimamia vyema taasisi hizo zilizo chini yake na pia alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Awadhi Massawe.
Bodi ya TPA ambayo ilianza kazi Juni 2, mwaka huu ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Profesa Joseph Msambichaka na wajumbe wake walikuwa Naibu Spika wa Bunge wa sasa, Dk Tulia Akson, Musa Ally Nyamsingwa, Donata Mugassa, Haruna Masebu, Gema Modu, Dk Francis Michael, Crescentius Magori, Flavian Kinunda nayo ilivunjwa.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa naye aliwashushia rungu watendaji wengine wa TPA kwa kuwasimamisha kazi, ambao ni viongozi watano wa sekta zilizotoa ruhusa makontena kutoka ndani ya bandari bila kulipa kodi pamoja na watumishi wanane wa bandari kavu, ambao walihusika na ukwepaji kwa makontena 2,387.
Wiki hii Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Miliki ya Rasimali za Reli (RAHCO), Benhadard Tito na kuivunja Bodi ya Wakurugenzi iliyokuwa ikiongozwa na Profesa Mwanuzi Fredrick.
Mkurugenzi wa Rahco, Benhadard Tito mbali na kusimamishwa kazi, lakini Rais Magufuli ameagiza kuchunguzwa kwa kina na Takukuru kufuatia ukiukwaji mkubwa wa taratibu za manunuzi, uliobainika katika mchakato wa utoaji wa zabuni ya ujenzi wa reli ya kati.
Majipu yaliyokamuliwa katika taasisi hizo tatu ,yamesababisha hadi taasisi zilizo chini ya wizara nyingine kama TRA iliyo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango na Takukuru iliyo chini ya Ofisi ya Rais,Tamisemi, Utumishi na Utawala Bora, nazo watendaji wake kuathirika kutokana na makosa yaliyofanywa na taasisi zilizokuwa Wizara ya Uchukuzi.
Rais Magufuli alimsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade kutokana na ubadhirifu wa mapato katika Bandari ya Dar es Salaam na pia alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah.
No comments:
Post a Comment